UN: Utalii umeajiri asilimia 10 ya watu duniani
- Wadau watakiwa kufanya uwekezaji unaojali mazingira, uchumi na kunufaisha jamii.
- Wananchi watakiwa kuendelea kutembelea vivutio vya utalii.
- Kukosa ujuzi, rasilimali, kunawakwamisha vijana kutumia fursa za utalii duniani.
Dar es Salaam. Leo Septemba 27, 2023 Tanzania imeungana na mataifa mengine ulimwenguni kuadhimisha siku ya utalii duniani sekta inayotajwa na Umoja wa Mataifa (UN) kuwa imeajiri asilimia 10 ya watu duniani.
Hii ina maana kuwa katika kila watu 10 ulimwenguni basi mmoja kati yao ameajiriwa au amejiajiri katika sekta ya utalii.
Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2022, sekta ya utalii ilichangia asilimia 21 ya pato la Taifa pamoja na asilimia 25 ya fedha za kigeni.
Soma zaidi: Mapato vituo vya makumbusho ya taifa yaendelea kupaa Tanzania
Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki aliyekuwa akitoa salamu za maadhimisho hayo amesema siku hii ni fursa kwa wadau wa utalii kutafakari upya mchango na umuhimu wa utalii kwa jamii hususan katika kuleta maendeleo na kutunza mazingira.
“Nichukue fursa hii kuwahimiza wadau wa utalii,kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi sambamba na kuimarisha uwekezaji unaojali mazingira, uchumi na kuinufaisha jamii,” amesema Kairuki.
Aidha, Kairuki amewarai Watanzania kuendelea kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini ambapo kwa mwaka 2022, Tanzania ilirekodi watalii milioni 1.4 ambapo kati yao watalii 787,742 ni wa ndani.
Soma zaidi: Guteress: Shughuli za kibinadamu zinahatarisha uwepo wa ‘spishi za kipekee’
Maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika Riyadh, Saudi Arabia yakiwa na a kauli mbiu isemayo “Utalii na Uwekezaji Unaojali Mazingira”
Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UNWTO) linasema uwezekano wa uwekezaji-kijani kufikia malengo ya maendeleo endelevu ni muhimu, kwa kuwekeza katika watu, miundombinu, ubunifu na teknolojia.
Hata hivyo UN imeonya kwamba, asilimia 50 ya vijana katika maeneo ya utalii wanashindwa kutumia fursa za utalii kutokana na kukosa rasilimali pamoja na mafunzo kuhusiana na fursa za utalii.
Je unaitumiaje sekta ya utalii hapo ulipo? Umejiajiri au umeajiriwa tuandikie maoni yako kupitia info@nukta.co.tz au tupigie 0677088088.