Kilimo kinavyosaidia kuokoa kivutio maarufu cha utalii Tanzania

November 17, 2021 3:40 pm · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni msitu maarufu wa Magoroto uliopo Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
  • Kinatumia mapato kutoka kwenye kilimo cha viungo na mifugo kuendelea na uhifadhi. 
  • Serikali yasema itaendelea kuimarisha sekta ya utalii Tanzania.

Tanga. Mita chache baada ya kuingia katika msitu wa Magoroto baadhi ya wafanyakazi wanaonekana katika mashamba yaliyopo pembezoni wakichambua marundo ya iliki na karafuu ziilivyovunwa katika eneo hilo.

Tofauti na miaka miwili iliyopita, wafanyakazi hawa ndiyo watu pekee waliopo katika msitu huu mashuhuri kwa utalii katika mkoa wa Tanga. 

Kipindi hicho cha nyuma, kabla ya kuingia ugonjwa wa virusi vya Corona (Uviko-19), majira ya saa tano asubuhi ilikuwa ni kawaida kuwakuta watalii wengi wa ndani na nje wakifanya utalii.

Kwa sasa hakuna tena waongoza watalii wanaowaelekeza wageni zaidi ya sauti za ndege na zile zinazosikika kwa mbali kutoka kwa wafanyakazi hao waliopo mashambani.

Msitu wa Magoroto uliopo wilayani Muheza ni miongoni mwa vivutio vya utalii nchini vilivyoathiriwa zaidi na Uviko-19 tangu Machi 2020 kutokana na mazuio yaliyokuwepo ya wageni kusafiri nje ya mataifa yao au kufanya shughuli zenye makundi ya watu wengi.

Hali hiyo ilipunguza kwa kiasi kikubwa watalii wa kimataifa kwenda kutembelea vivutio vya utalii duniani ikiwemo Tanzania.

Magoroto ni kivutio cha watalii wanaopenda kupanda milima, kutazama mimea adimu, kuona au kununua bidhaa za utamaduni na asili, kutembelea mashamba ya zamani ya mawese na kuogelea katika ziwa lililopo katika eneo hilo. 

Kama ilivyokuwa kwa vivutio vingi vya utalii ulimwenguni, msitu huo uliopo kilomita 37 kutoka jijini Tanga, ulifungwa na kusitisha huduma kwa miezi mitatu mfululizo tangu Machi 2020 wakati Tanzania iliporekodi kisa cha kwanza cha mgonjwa wa Corona. 

Uongozi  wa Kampuni ya Amboni Sisal Properties inayosimamia msitu huo unasema kuwa kabla ya Uviko-19 walikuwa wanapata watalii hadi 3,000 kwa mwaka.

 Mwonekano wa msitu wa Magoroto wilayani Muheza. Shughuli za utalii katika eneo hili ziliathirika baada ya Uviko-19 kuingia Tanzania Machi, 2020. 

 

Hata hivyo, baada ya kufungua tena Juni 2020 hawakuweza kufikisha hata watalii 1,000 waliotembelea mpaka Juni mwaka huu. Hii ina maana kuwa ndani ya mwaka mmoja, kivutio hicho kimepoteza watalii zaidi ya 2,000 ambao wangeleta mapato yanayosaidia pia shughuli za uhifadhi. 

Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UNWTO) linaeleza kuwa idadi ya watalii wa kimataifa ilipungua kwa asilimia 73 mwaka 2020 huku kwa miezi mitano ya mwanzo ya mwaka 2021, watalii wamepungua hadi milioni 147 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2020.

Mwaka 2020 Tanzania ilipokea watalii 620,867 ikiwa ni pungufu mara mbili ikilinganishwa na watalii milioni 1.5 wa mwaka 2019, kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) iliyotolewa mwaka 2020 pamoja na changamoto zilizoendelea kuikabili misitu, janga la Corona pia limesababisha kukosekana kwa fedha za kutosha kugharamia utunzaji wa misitu hiyo barani Afrika. 

Kupungua kwa shughuli na mapato ya utalii duniani, hata hivyo, hakukuzuia baadhi ya vivutio vya utalii kuendelea na shughuli zake za uhifadhi ukiwemo msitu wa Magoroto. 

Uhifadhi wa msitu wa Magoroto na vivutio vyake hutegemea mapato ya watalii lakini wawekezaji wake hawakuacha shughuli za uhifadhi ziathirike baada ya kuamua kutafuta vyanzo vingine vya mapato. 

Katika kuhifadhi mandhari ya asili ya eneo hilo lililopo katika mwambao wa milima ya Usambara, Magoroto wanatumia mapato yatokanayo na kilimo. 

“Tuna biashara za aina mbili zinazoweza kutuingizia kipato. Moja ni biashara ya utalii lakini pia kilimo,” anasema Meneja wa Msitu wa Magoroto, Jeremiah Mchechu.

Mchechu anasema kilimo hicho cha viungo na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa ya kisasa aina ya “Friesian” kumewasaidia wasifunge utalii kama ilivyo katika vivutio vingine na kuhakikisha msitu unaendelea kuhifadhiwa ikiwemo ulinzi wa maliasili zilizopo. 

“Katika kilimo tunalima viungo kama iliki, pilipili manga, karafuu, vanila pamoja na mifugo ambayo katika kipindi hiki ambapo biashara (utalii) iko chini tunatumia vyanzo hivyo kutunza msitu huu,” anasema Mchechu. 

Mchechu anasema viungo hivyo huviuza katika maeneo mbalimbali ya Tanzania hasa katika masoko makubwa na hivyo kuwa na uhakika wa kipato na ajira kwa wafanyakazi wake wakati utalii ukianza kuimarika taratibu. 

Hali ilivyokuwa tete

Licha ya msitu huo, wenye ukubwa wa ekari 591 na ziwa la maji safi kuendelea kujiendesha hasa katika utunzaji wa mazingira yake, wafanyakazi zaidi ya 20 waliokuwa wanatoa huduma za utalii walipoteza ajira kwa muda hadi ilipoanza kurejea taratibu na kuwekeza zaidi kwenye kilimo. 

“Ile hali iliniathiri kwa upande wangu kutokana niko nyumbani na sina kazi, na nina watoto ambao wanasoma na wananitegemea ada. Sikuweza kuzoea kwa haraka,” anasema Merina John moja ya wafanyakazi wa msitu wa Magoroto.

Hata hivyo, Merina na wenzake wamerudi tena kazini huku wakiwa na matumaini makubwa kuwa sekta ya utalii itaimarika na watapokea watali wengi zaidi kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa kupambana na Uviko-19.

Anasema Uviko-19 umemfunza kuwa na vyanzo zaidi ya kimoja cha mapato kama ilivyo kwa Magoroto ili biashara moja inapoathiriwa na majanga makubwa, nyingine iendelee kutoka huduma.

Mwonekano wa shamba la viungo vinavyolimwa katika msitu wa Magoroto. Mazao hayo yamesaidia kuingiza mapato ya kutunza msitu huo na kulinda ajira ambazo zingepotea kwa sababu ya kuyumba kwa utalii Tanzania. Picha zote|Gift Mijoe/Nukta.

Waangazia vyanzo vingine vya mapato

“Sasa hivi najiandaa kupata chochote ili niweze kufanya biashara ndogo inayoweza kunisogeza iwapo hali itazidi kuwa mbaya,” anasema Merina, ambaye ni mhudumu wa vinywaji katika kituo hicho cha utalii.

UNWTO imesema sekta ya utalii duniani itaimarika kwa asilimia 60 ifikapo mwaka 2022 huku Afrika ikitazamiwa kuimarika kwa asilimia 73.

Miongoni mwa njia zitakazosaidia kuimarisha sekta ya utalii, kwa mujibu wa UNWTO,  ni kampeni ya utoaji chanjo ya Uviko-19 kutokana na kupunguzwa kwa masharti ya safari za kimataifa. 

“Tuna imani kuwa janga hili litaisha. Kwa kasi hii ya utoaji chanjo, watu wameanza tena kutalii na kusafiri, tuna matumaini makubwa kwamba mwenendo huu wa utoaji chanjo ukiendelea, tutarudi kwenye mstari,” amesema Mchechu akionekana mwenye matumaini makubwa katika siku zijazo.

Mkoa wa Tanga umebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ikiwemo mapango ya Amboni, Mto Pangani, fukwe za bahari ya Hindi na majengo ya kihistoria na kitamaduni ambavyo huvuta watalii kila mwaka.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Nassib Mmbagga ameiambia Nukta kuwa katika kuhakikisha sekta ya utalii inaimarika wataendelea kutunza vivutio vilivyomo wilayani humo na kuhimiza wananchi kutembelea vivutio hivyo huku wakichukua tahadhari dhidi ya Uviko-19.

“Sisi kama Watanzania ni muhimu kushiriki kuimarisha utalii wa ndani ili tuweze kupambana na hali hii ya kiuchumi lakini hata sisi wa ndani tunapaswa kuchukua tahadhari zote ili kujikinga na janga hili,” anasema Mmbagga.

Mmbagga anawataka wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya Uviko-19, kunawa mikono kwa maji tiririka, kuvaa barakoa na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima. 

Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
15 Jul, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
15 Jul, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
15 Jul, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Kutana na ‘Poultry Plucker’, mashine inayonyonyoa kuku watatu kwa dakika moja

Kutana na ‘Poultry Plucker’, mashine inayonyonyoa kuku watatu kwa dakika moja

Nukta TV

Rais Samia: Kalamu yangu ina hatari, sijawahi kusaini mtu kunyongwa

Rais Samia: Kalamu yangu ina hatari, sijawahi kusaini mtu kunyongwa

Nukta TV

Rais Samia: Matumizi jina Samia, likiwa kila mahali inachosha, tafuteni wengine

Rais Samia: Matumizi jina Samia, likiwa kila mahali inachosha, tafuteni wengine

Nukta TV