Samia: Ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini

March 19, 2021 11:02 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Mama Samia ameapa leo Machi 19, 2021 kuwa Rais wa Tanzania, Ikulu mkoani Dar es Salaam. Picha| Steven Genya.


  • Amewataka Watanzania kujenga umoja na kuzika tofauti zao wakati Serikali ikitafuta namna ya kuwekana sawa kuhusu mambo muhimu ya Taifa. 
  • Amesema Serikali iko imara na itaendeleza kazi nzuri za Hayati Rais Magufuli. 

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema wataendeleza kazi alizoanzisha Hayati Rais John Magufuli huku akiwawataka Watanzania kujenga umoja na kuzika tofauti zao wakati Serikali ikitafuta namna ya kuwekana sawa kuhusu mambo muhimu ya Taifa.  

Mama Samia ambaye ameapa leo Machi 19, 2021 kuwa Rais wa Tanzania, Ikulu mkoani Dar es Salaam amesema Watanzania wanapaswa kuwa wamoja na kujenga mshikamano katika kipindi hiki cha maombolezo na kuzika tofauti zetu na kutazama mbele kwa matumaini makubwa.

“Ndugu viongozi na ndugu wananchi kabla sijahitimisha naomba niseme ndugu zangu Watanzania, huu ni wakati wa kusimama pamoja na kushikamana katika kipindi hiki cha maombolezo, huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu na kuwa wamoja kama Taifa.

“Ni wakati wa kufarijiana, kuonyeshana upendo, undugu wetu, kudumisha amani yetu, kuenzi utu wetu, uzalendo wetu na utanzania wetu,” amesema Rais Samia huku akisema “leo si siku nzuri kwangu ya kuhutubia Taifa maana nimeelemewa na kidonda kikubwa kwenye moyo wangu.”

Wakati huu siyo wa kutazama mbele kwa mashaka bali ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini kama Taifa, amesema Rais kwa unyenyekevu mbele ya viongozi mbalimbali wa Serikali waliohudhuria hafla ya kuapishwa kwake.  

“Si wakati wa kutazama yaliyopita bali ni wakati wa kutazama yajayo. Si wakati wa kunyoosheana vidole bali ni wakati wakushikana mikono na kusonga mbele. 

Ni wakati wa kufutana machozi na kufarijiana ili tuweke nguvu zetu za pamoja kujenga Tanzania mpya ambayo mpendwa wetu Rais Magufuli aliitamani,” amesisitiza Rais wa awamu ya sita wa Tanzania. 

Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuapishwa amekagua gwaride maalum katika viwanja vya Ikulu mkoani Dar es Salaam. Picha| Steven Genya.

Aidha, Rais amesema kutokana na msiba mzito wa Taifa, Serikali itatafuta muda mwingine kuzungumzia mambo muhimu ikiwemo tofauti zilizopo kwenye jamii ili kutengeneza mstakabali mzuri wa Tanzania.

“Tutafuta wasaa mwingine hapo baadaye tuzungumze tukumbushane na tuwakane sawa juu ya mambo mengi yanayohusu Taifa letu na mstakabali wake na matarajio yetu ya siku za usoni,” amesema Rais Samia aliyekuwa Makamu wa Rais kabla Magufuli hajafariki dunia Machi 17 mwaka huu. 


Kazi za Hayati Rais Magufuli kuendelezwa

Kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema Taifa liko imara kwa sababu lina viongozi makini ambao wataivusha Tanzania na kuendeleza mazuri aliyoyaanzishwa Rais Magufuli aliyefariki kwa maradhi ya moyo. 

Amewataka  Watanzania kuwa na moyo wa subira, kujenga umoja na mshikamano katika kipindi hiki kigumu.

“Niwahakikishie kuwa, tuko imara kama taifa na sisi viongozi wenu tumejipanga vizuri kuhakikisha kuwa tunaendelea pale mwenzetu (Dk Magufuli) alipoishia,” amesema. 

Samia ambaye anakuwa rais wa kwanza mwanamke Afrika Mashariki amesema Tanzania imempoteza kiongozi shupavu, madhubuti, mzalendo, mwenye maono, mpenda maendeleo, mwana mwema wa bara la Afrika na mwana mapinduzi wa kweli.

“Mheshimiwa Magufuli alikuwa chachu ya mabadiliko kwa kweli tumepwelea kwa kuondokewa na kiongozi wetu huyu hatuna cha kusema,” amesema. 


Soma zaidi:


Ugumu wa kiapo chake

Mama Samia ambaye ana Shahada ya Uzamili ya Maendeleo ya Uchumi wa Jamii, amesema kiapo alichoapa leo ni tofauti na viapo vingine alivyowahi kuvifanya siku za nyuma kwa sababu amekula kiapo akiwa na kidonda kikubwa moyoni mwake.

Amesema ni mara ya kwanza kwa Rais wa Tanzania kufarikia akiwa madarakani na Makamu wake kuteuliwa Rais kabla hajamaliza muda wa utumishi wake, jambo 

“Leo si siku nzuri kwangu ya kuhutubia taifa maana nimeelemewa na kidonda kikubwa kwenye moyo wangu. Kiapo nilichokula leo ni tofauti na viapo vyote nilivyowahi kuapa katika maisha yangu.

“Viapo vyote nilivyokula vilikuwa vya faraja, nderemo, vifijo na bashasha tele, leo nimekula kiapo cha juu zaidi kwenye nchi yetu nikiwa na majonzi tele na nchi ikiwa imetandwa wingi jeusi na simanzi kubwa,” amesema  Samia.

Habari hii imeandikwa na Daniel Samson na Rodgers George.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...