Rais Samia ahimiza umoja, amani na utulivu akiadhimisha miaka minne madarakani

March 20, 2025 4:39 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Awataka Watanzania kuungana kumuomba Mungu aendelee kuibariki Tanzania.

Arusha, Rais wa Tanzania  Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuendelea kudumisha umoja, amani na utulivu wakati wakiendelea kusherehekea miaka minne tangu aingie madarakani akipokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake John Pombe Magufuli,

Machi 19, 2021 ni miongoni mwa siku zitakazokumbukwa katika historia ya Tanzania baada ya  Samia Suluhu Hassan kuapishwa kuwa Rais mwanamke wa kwanza baada ya aliyekuwa Rais wakati huo John Pombe Magufuli kufariki kutokana na maradhi ya moyo.

Kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii ikiwemo X,  Machi 19, 2025 Rais Samia amewashukuru Watanzania wanaoendelea kutuma salamu za pongezi akihimiza umoja amani na utulivu.

“Tuungane pamoja kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuibariki nchi yetu, tudumu katika umoja, amani na utulivu. 

Tumuombe pia Mwenyezi Mungu aendelee kutuongoza katika utu na weledi kwenye utekelezaji wa majukumu yetu, na kuzibariki kazi tunazozifanya katika kuleta ustawi wa nchi yetu na Wananchi wote. Kazi na Utu, Tunasonga Mbele.” amesema Rais Samia.

Rais Samia anasheherekea miaka mine madarakani ikiwa imesalia miezi kadhaa kabla ya Tanzania kuingia katika uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani ambapo kama akichaguliwa ataiongoza tena kwa muda wa  miaka mitano.

Licha ya kushika hatamu ya kuongoza nchi katika wakati ambao Tanzania na dunia kwa ujumla ilikuwa ikikabiliwa na majanga mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa Uviko 19 na vita ya Urusi na Ukraine , Rais Samia amelisongesha gurudumu la maendeleo akifanikisha miradi mikubwa iliyoachwa na mtangulizi wake.

Miongoni mwa mafanikio makubwa yaliyofanyika ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia ni pamoja na kukamilika kwa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo reli ya kisasa SGR (Standard Gauge railway) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma iliyozinduliwa Agosti Mosi, 2024 ikigharimu zaidi ya Sh 7 trilioni kwa mujibu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC).

Mradi mwingine ambao umepigiwa chapuo na Serikali ya Rais Samia ni mradi wa mradi wa kufua umeme wa bwawa umeme wa maji la Julius Nyerere (JNHPP) ambao upo mbioni kukamilika, ununuzi wa ndege za Shirika la Ndege (ATCL) na Ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi.

Huenda kukamilika kwa kwa baadhi ya miradi hiyo pamoja na sababu nyingine kadhaa kumesababisha uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 0.6 kutoka asilimia 4.8 zilizokuwepo wakati anaingia madarakani mwaka 2021 hadi asilimia 5.4 mwaka 2024 ikitarajiwa kuongezeka zaidi mwaka huu.

Pamoja na mafanikio hayo yote ya kiongozi huyo bado rungu lipo kwa Watanzania watakaofanya maamuzi Oktoba mwaka huu ikiwa wanataka Rais Samia aendelee kuwepo madarakani kwa miaka mitano ijayo au wampe nafasi kiongozi mwingine watakayeona anafaa zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks