Mwaka mmoja kifo cha Magufuli: Serikali, Watanzania kuendeleza mema yake
- Serikali kukamilisha miradi yote aliyoianzisha.
- Watanzania wajivunia miundombinu aliyoiasisi ikiwemo barabara na reli.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendeleza mazuri yote yaliyoachwa na Rais wa awamu ya tano Hayati Dk John Magufuli pamoja na kuleta mema mapya.
Hayati Magufuli alifariki dunia Machi 17 mwaka jana alipokuwa akipatiwa matibabu katika moja ya hospitali jijini Dar es Salaam kutokana na maradhi ya moyo.
Rais Samia amesema hayo leo Machi 17, 2022 wakati wa maadhimisho ya kumbukizi ya mwaka mmoja wa kifo cha Magufuli Wilayani Chato, mkoa wa Geita huku akimwelezea Hayati Magufuli kuwa kiongozi aliyepinga rushwa, ubadhirifu na kusisitiza uchapakazi na uzalendo kwa Taifa.
“Hayati Magufuli alitamani kuiona Tanzania iliyojikomboa na kujitegemea kiuchumi, na mimi nikasema nitaliongoza Taifa katika muelekeo huo huo. Hotuba yangu baada ya kuapishwa nilisisitiza kwamba nitayaendeleza mema yote aliyotuachia na kuleta mema mengine mapya,” amesema Rais Samia.
Amesema Serikali anayoiongoza imedhamiria na kujidhatiti kuendeleza shughuli zote za maendeleo zilizoanzishwa na Hayati Magufuli na kutekeleza shughuli nyingine mpya itakazozifikiria kwa manufaa mapana ya Taifa.
Rais Samia amewaahidi wananchi wa Chato kuwa Serikali itakamilisha na kushiriki kuifungua miradi yote ya maendeleo ambayo imeshakamilika ikiwemo stendi mpya ya Chato, uwanja wa ndege wa Chato uliofikia asilimia 95 pamoja na kivuko cha Chato.
“Faraja yangu ni kwamba baadhi ya miradi tayari imemalizika ambapo hivi karibuni tutazindua daraja la Tanzanite ambalo ni ndoto ya Hayati Rais Magufuli kuona linakamilika na tumeendelea kuboresha na kuendeleza huduma za jamii ikiwemo afya, maji, elimu na umeme,” amesema Rais.
Rais Samia Suluhu Hassan akiweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa Rais wa awamu ya tano Hayati Dk John Pombe Magufuli mara baada ya Misa Takatifu iliyofanyika katika uwanja wa michezo wa Magufuli, Chato leo Machi 17, 2022. Picha| Ikulu
Watanzania kumuenzi Hayati Magufuli
Baadhi ya wakazi jijini Mwanza wamesema bado wanakumbuka mchango mkubwa alioufanya hayati John Magufuli enzi za uhai wake hasa wa kufanya mapinduzi ya kimaendeleo.
Wakizungumza na Nukta habari wakazi hao wamesema Rais Magufuli aliacha alama zisizofutika kwenye mioyo ya Watanzania wengi hasa wananchi wa kipato cha chini.
“Tunakumbuka mengi katika kipindi cha miaka mitano tumeshuhudia akifanya mambo makumbwa, ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja, masoko na stendi za mabasi,” amesema Lukas Shitungulu, mkazi wa Mwanza
Amesema uboreshaji wa barabara umewarahisishia katika kusafirisha mizigo wa mizigo
Mkazi mwingine, John John amesema wataendelea kumkubuka Rais Magufuli kwa kufuta ada na mirorongo ya michango mashuleni ambapo katika kipindi hicho walishuhudia wanafunzi wengi kuandikishwa tofauti na miaka iliyopita.
“Mfano hapa Mwanza zipo alama alizoweka ambazo zitazungumzwa kizazi hadi kizazi, ujenzi meli mpya inayoendelea, ujenzi wa daraja ndani ya Ziwa Victoria na miradi ya maji yote yamefanyika katika awamu ya tano, ” amesema John.
Soma zaidi:
Mwenyekiti wa Soko kudu, Ahmad Nchora amesema kwa mara ya kwanza katika uongozi wake walishuhudia nidhamu ya kazi maofisini.
“Alikuwa mkali hakupenda watu waonewe hasa wa hali ya chini na kiongozi asiyetekeleza wajibu wake alimtumbua, ” amesema Nchora
Baadhi ya wafanyabiashara wadogo maarufu wamesema wanamkumbuka namma alivyowapigania kuendelea kubaki kwenye maeneo yao kisha kuwatengenezea utaratibu wa vitambulisho.
Mwenyekiti wa wamachinga Mkoa wa Mwanza, Said Tembo amesema hayati Magufuli walikuwa mtetezi wao.
Habari hii imeandikwa na Daniel Samson na Mariam John.
Latest