Ripoti: unyanyasaji wa kijinsia janga jipya kwa wanahabari wanaume Tanzania
- Wanahabari wanaume wawili kati ya 10 walinyanyaswa kijinsia kati ya Septemba hadi Novemba 2023.
- Wadau wa habari wabainisha mbinu za kutatua tatizo hilo.
Dar es Salaam. Wakati juhudi mbalimbali za kukomesha ukatili wa kijinsia zikiendelea kupigiwa chapuo hususan kwa wanawake, utafiti mpya wa maoni ya wanahabari Tanzania umebainisha kuwa karibu nusu ya wanahabari hukutana na unyanyasaji huo huku wanaume wakiathirika zaidi.
Ripoti ya utafiti huo uliofanywa na Twaweza, inabainisha kuwa asilimia 21 ya wanahabari wanaume wamepitia unyanyasaji wa kijinsia kati ya mwezi Septemba hadi Novemba 2023.
Hiyo ni sawa na kusema wanaume 120 kati ya 572 waliohojiwa katika utafiti huo uliohusisha wanahabari 1,202 kutoka vyombo vya habari mbalimbali nchini wamefanyiwa ukatili wa kijinsia.
Idadi hiyo ni asilimia mbili zaidi ya wanawake wanahabari ambao wameripoti kutokea kwa vitendo hivyo kati ya Septemba hadi Novemba mwaka jana.
Soma zaidi:Mbinu tatu za kukwepa maumivu ya mikopo umiza Tanzania
Ndani ya kipindi hicho ni asilimia 19 tu ya wanawake walioripoti unyanyasaji wa kijinsia katika vyombo vyao vya habari.
Aidan Eyakuze, Mkurugenzi wa taasisi ya Twaweza aliyekuwa akizungumzia takwimu za utafiti huo leo Februari 16, 2024 jijini Dar es Salaam amesema kuwa taasisi yake italichambua upya suala hilo kuona ikiwa linaweza kuainishwa kama miongoni mwa rushwa ndani ya vyombo vya habari.
“Hili suala la unyanyasaji wa kijinsia inabidi tukalichambue zaidi…kwanini tunaona hata wanaume wananpitia unyanyasaji wa kijinsia na hatujawajumuisha katika aina za rushwa ndani ya vyombo vya habari kwa ujumla,”amesema Eyakuze.
Takwimu hizo za wanaume wanabahari wanaonyanyaswa kijinsia zinakuja wakati kukiwa na vuguvugu kubwa la utetezi wa wanawake katika katika vyombo vya vya habari likilenga kuwakomboa katika aina zote za unyanyasaji ikiwemo wa kijinsia na rushwa ya ngono huku kundi la wanaume likisahaulika.
Eyakuze amebainisha kuwa kilichowasaidia kuwabainisha wanaume hao wanaonyanyaswa kijinsia ni mahojiano kwa njia ya simu kutokana na wengi wao kuogopa kuripoti polisi au katika madawati ya kijinsia ili kupewa msaada.
“Mara nyingi hutaona wanaume wanaonyanyasika wakienda kuripoti lakini kwa njia ya simu wanaweza kusema mambo ambayo wanajua hawatasikilizwa na watu wengine kwa kuhofia watamcheka,”amesema Eyakuze.

Baadhi ya wadau wa habari waliohudhuri katika uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa maoni ya wanahabari Tanzania.Picha|Twaweza
Mbali na unyanyasaji wa kijinsia wanahabari wanaume wanakumbana na vizuizi vingine vinavyokwamisha shughuli zao zaidi ya wanahabari wanawake.
Mathalan asilimia 55 ya wanaume wamekutana na vitisho kulinganisha na asilimia 43 ya wanawake waliokutana na tatizo hilo pamoja na asilimia 30 ya wanaume kushilikiwa au kukamatwa na mamlaka kulinganisha na asilimia 13 ya wanawake.
Kwa upande mwingine wanaume ndio waliokutana na vitisho kutoka kwa familia kwa ukubwa zaidi kwa asilimia 17 kulinganisha na asilimia 9 za wanawake.
Zinazohusiana:MCT yalaani unyanyasaji waandishi wa habari Tanzania
Ni nini suluhu?
Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Kenneth Simbaya, ameiambia Nukta habari kuwa kitakachosaidia kumaliza tatizo la unyanyasaji wa kijinsia kwa wanaume ndani ya vyombo vya habari ni kulifahamu tatizo kwa undani na kutoa uelewa kwa jamii.
“Cha kwanza hakuna tiba muhimu kama uelewa, kabla hakujatokea mabadiliko yoyote ni lazima jamii iwe na uelewa kusu tatizo hilo…
…Cha pili ni kuwa na usawa katika vyombo vyetu vya habari, kama ambavyo tunashughulika kumaliza unyanyasaji kwa wanawake hivyo hivyo tuwashughulikie wanahabari wanaume,” amesema Simbaya.
Naye Risha Chande, Mkurugenzi wa Uchehemuzi na Mahusiano kutoka Twaweza, amebainisha kuwa miundombinu ya kuripoti ukatili wa kijinsia ndani ya vyombo vya habari na nchi nzima kwa ujumla ikibadilika itaweza kuwapa nafasi wanaume wengi zaidi kuripoti matukio hayo.
“Mimi nafikiri kama tukitumia “anonymous ways” (njia za kumficha mtoa taarifa) kama simu au mtandao kukusanya taarifa tunaweza tukapata takwimu nyingi zitakazotuwezesha kulifahamu tatizo kiundani kisha tukafahamu jinsi ya kulitatua,”amesema Risha.
Aidha, Eyakuze amesema kuwa licha ya elimu kwa umma kitakachowasaidia wanahabari kupambana na unyanyasaji wa kijinsia ni kutumia kalamu zao kueleza ukubwa wa tatizo na namna gani linaathiri utendaji kazi wao.