Mikopo bila maarifa: Mtego unaokwamisha maendeleo wanawake, vijana

April 17, 2025 4:02 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi yao wanachukua mikopo yenye masharti magumu.
  • Ukosefu wa elimu wachangia kuangusha biashara. 

Dar es Salaam. Katika harakati za kupambana na umasikini na kujikwamua kiuchumi, mikopo imekuwa moja ya silaha inayotegemewa na makundi mbalimbali hususan wanawake na vijana. 

Kwa baadhi ya watu, mkopo ni daraja la matumaini au fursa ya kujenga biashara au kuendeleza elimu. Kwa wengine, mikopo imekuwa ni mtego. Ni jinamizi linalowaingiza katika matatizo ikiwemo kufirisika. Hii husababishwa na ukosefu wa elimu ya mikopo katika biashara. 

Hali hii imeibua mjadala mpana nchini kuhusu athari za ukosefu wa elimu ya mikopo, hasa kwa wanawake na vijana wanaopambana kutoka katika umasikini.

Ndoto iliyozimwa na mkopo usio na huruma

Frida John (26), mkazi wa Kibamba, Dar es Salaam, ni mmoja wa vijana waliolazimika kujifunza kwa maumivu. Akiwa mfanyabiashara wa vipodozi Bomang’ombe, Kilimanjaro, alikopa Sh200,000 ili kuokoa biashara yake iliyokuwa ikiyumba. 

Hata hivyo, mkopo huo ulimgeuka adui mkubwa, Frida alitakiwa kurejesha Sh8,000 kila siku kwa siku 30, bila kusuasua.

“Nilichukua mkopo nikiwa na matumaini, lakini masharti yalinimaliza. Nikawa nalipa hata pale biashara inapoyumba, bila kujua kuwa naua mtaji wangu,” ameeleza kwa masikitiko Frida.

Unapokusudia kuchukua mkopo hakikisha biashara yako ina uwezo wa kurejesha mkopo bila kugusa mtaji, Picha | Kelvin Makwinya.

Kwa sasa, Frida ni wakala wa huduma za kifedha na muuzaji wa bidhaa za urembo. Ametumia maumivu ya zamani kutoa somo kwa wengine. 

“Usikurupuke kukopa. Hakikisha biashara yako ina uwezo wa kurejesha mkopo bila kugusa mtaji,” anashauri Frida.

Watoa mikopo wanatoa elimu au wanaweka mitego?

Sara Vicent (43), ambaye amekuwa Mwenyekiti wa kikundi cha kina mama wanaokopa kupitia ASA Microfinance Tanzania Ltd, anasema taasisi yao huchukua hatua za awali kutoa elimu na kufanya tathmini ya mkopaji kabla ya mkopo kuidhinishwa.

“Hatumpi mtu mkopo kama hana biashara au kitega uchumi. Tunatembelea eneo lake, tunampa ushauri, tunamweleza masharti kwa uwazi,” anasema Sara na kuongeza kuwa kwa mwanachama mpya, mkopo wa mwanzo ni Sh600,000 wenye riba ya asilimia 20 ambapo ndani ya miezi sita, mkopaji anatakiwa kurejesha Sh720,000.

Licha ya elimu inayotolewa na taasisi zinazotoa mikopo, bado baadhi ya wanawake na vijana hawatumii vizuri mikopo hiyo. Picha | ASA Microfinance Tanzania.

Licha ya elimu inayotolewa na taasisi zinazotoa mikopo, bado baadhi ya wanawake na vijana hawatumii vizuri mikopo hiyo.

Si kila mkopo ni msaada mwingine ni sumu

Mtaalamu wa uchumi na fedha, Profesa Alfred Kinyondo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anaonya kuwa mkopo si suluhisho la kila tatizo. 

“Tatizo si mkopo. Tatizo ni sababu ya kuchukua mkopo na aina ya mkopo unaochukua,” anasema Prof Kinyondo, mhadhiri wa UDSM. 

Prof Kinyondo anaamini kuwa watu wengi huingia katika matatizo kwa kuchukua mikopo ya haraka yenye masharti magumu ikiwemo inayolipwa kwa muda mfupi na yenye riba kubwa.

“Tatizo si mkopo. Tatizo ni sababu ya kuchukua mkopo na aina ya mkopo unaochukua,” anasema Prof Kinyondo. Picha | Wizara ya Fedha.

“Wengine wanachukua mkopo kufanya sherehe, kununua gari au simu mpya. Huo si uwekezaji. Mkopo unatakiwa uchukuliwe kwa lengo la kuzalisha fedha, si kutumia,” anasema mtaalam huyo. 

Elimu ya mikopo inapaswa kuwa msingi wa kwanza kabla ya kutolewa kwa mfanyabiashara au mjasiriamali. Bila elimu hiyo, mikopo inageuka kuwa mzigo siyo tu wa kifedha bali wa kisaikolojia na kijamii.

Uchambuzi unaonesha kuwa wanawake na vijana wengi hujikuta wakididimia zaidi kiuchumi kwa sababu ya masharti ya mikopo ambayo hayaendani na hali halisi ya maisha yao. Wengine hulazimika kuuza mali, kukimbia madeni, au hata kufunga biashara.

Nini kifanyike?

Ili mikopo iwe na manufaa, Profesa Kinyondo anashauri kuwa ni muhimu kukopa kwa ajili ya uwekezaji tu, na si matumizi ya kawaida. 

“Sheria namba moja ya kuchukua mkopo, unachukua mkopo ili kuwekeza, ili uwekezaji uweze kuzalisha na uzalishaji ule ndio uweze kurudisha mkopo,” anasisitiza Profesa Kinyondo. 

Pia anatahadharisha dhidi ya kukurupuka kuanzisha biashara na uwekezaji bila utafiti wa kina, akihoji kuwa, “lazima ujiulize, hata kama unachukua mkopo kufanya uwekezaji, je uko ninapotaka kufanya uwekezaji kuna lipa?”

Ili mikopo iwe na manufaa, ni muhimu kukopa kwa ajili ya uwekezaji tu, na si matumizi ya kawaida.  Picha | Kelvin Makwinya.

Aidha, Profesa Kinyondo anahimiza watu kuwa makini na aina ya mikopo wanayoichukua huku akishauri kuchukua mikopo yenye masharti rafiki ili kuepuka hasara na kurudi nyuma kimaendeleo.

“Mtu unaambiwa kwamba mkopo ukiomba unapewa ndani ya nusu saa… alafu unachukua mkopo wa Sh100,000 unaambiwa baada ya miezi mitatu au sita arudishe Sh200,000 maana yake huo mkopo una riba ya asilimia 100,” anafafanua Profesa Kinyondo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks