‘Changing room: Mkombozi wa wasichana Sinde Sekondari mkoani Mbeya

Mwandishi Wetu 1025Hrs   Machi 13, 2024 Afya & Maisha
  • Itawasaidia kubadili nguo wakati wa hedhi.
  • Awali iliwalazimu kughairi masomo kutokana na kukosekana kwa chumba maalumu cha kubadili nguo.
  • Walimu wasema uwepo wake utachagiza ongezeko la ufaulu kwa wasichana.

Dar es Salaam. Huenda ufaulu kwa wanafunzi wasichana wanaosoma Shule ya Sekondari Sinde iliyopo jijini Mbeya ukaongezeka kwa siku za usoni mara baada ya kukamilika kwa mradi wa vyumba vya kubadilisha taulo za kike wakati wa hedhi, jambo lililokuwa linakwamisha mahudhurio ya masomo kwa wanafunzi hao siku za nyuma.

Awali zaidi ya wasichana 800 katika shule hiyo walikuwa wakisuasua kuhudhuria darasani kwa sababu ya kukosekana kwa chumba hicho ambapo walilazimika kubaki nyumbani kwa muda wa siku kadhaa mpaka kipindi cha hedhi kiishe jambo lililoathiri muda wao wa kupata masomo.

Shule hiyo iliyopo katika ya jiji la Mbeya inawakilisha shule nyingi ambazo hazina miundombinu rafiki kwa ajili ya kujisitiri wanawake wakati wa hedhi ‘changing room’.

"Kipindi cha nyuma tukiwa kwenye siku zetu hedhi tulikuwa tunakosa vipindi kwa sababu tulikuwa hatuhudhurii shule kutokana na mazingira yalivyokuwa, kwani kulikuwa hakuna sehemu ya kubadilishia pedi au kutupa taulo ambazo zimetumika," Isabela Adam mwanafunzi wa kidato cha nne shuleni hapo ameiambia Nukta Habari.

Chumba cha kubadilishia taulo za hedhi 'changing room' kinavyoonekana kwa ndani.Pichal Samuel Ndoni

Hata hivyo, kwa sasa hali ni tofauti shuleni hapo, kwa kuwa hivi sasa wasichana hawatalazimika tena kughairi masomo wakiwa katika kipindi cha hedhi bali watatumia chumba maalumu kilichotengenezwa shuleni hapo kwa ajili ya kubadili au kuvaa taulo za hedhi (pedi).

Chumba hicho kilichojengwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) ni sehemu ya sehemu program ya usafi wa mazingira, uhakika na upatikanaji wa maji 2019-2025 ambapo pamoja na chumba hicho yamejengwa matundu 16 ya vyoo kwa ajili ya wasichana.

Mhandisi mshauri wa maji, kutoka GIZ, Agnes Sigareti ameiambia Nukta Habari kuwa ujenzi wa chumba hicho umezingatia usafi, faragha pamoja na mazingira rafiki kwa watu wote.

“Ni chumba cha kisasa, kilichojengwa kwa ubora na utaalam wa hali ya juu ndani yake kina chemba ya kuchomea taulo ya kike ‘pedi’ mara baada ya kutumika, kuna kabati kwa ajili ya kutunzia taulo, kina dirisha dogo ambalo limeunganishwa na tanuri la kuchomea, kina maji pamoja na sabuni,” amesema Sigareti.

Sigareti ameongeza kuwa lengo la mradi huo ni kuboresha afya na usafi wa mazingira na kutokomeza magonjwa ya mlipuko katika Kata ya Sinde kwa kuzingatia miongozo ya Serikali.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Sinde Anatalia Luwungo mbali na kuishukuru GIZ kwa ujenzi wa mradi huo, amesema ana imani hali hiyo itainua taaluma kwa kuwa wanafunzi wengi walikuwa wakishindwa kuhudhuria darasani kutokana na kukosekana kwa miundombinu hiyo.

​Habari hii imeandikwa na Samuel Ndoni na kuhaririwa na Esau Ng'umbi


Related Post