TAMASHA LA NISHATI LA WANAHABARI 2018: Wadau wataka changamoto za nishati jadidifu ziangaliwe upya

November 29, 2018 10:02 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Changamoto hizo ni pamoja na wanasiasa kuingilia maamuzi ya sera inayohusu nishati jambo linaloathiri utekelezaji wa miradi mbalimbali inayolenga kuwainua wananchi kiuchumi.
  • Wadau mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari kukaa na Serikali kuangalia namna nzuri ya kuondoa migongano wakati wa kuwahudumia wananchi. 

Arusha. Wakati Tamasha la Nishati la Wanahabari 2018 linaingia siku ya nne, wadau wa sekta ya nishati jadidifu wameeleza changamoto mbalimbali ikiwemo wanasiasa kuingilia utekelezaji wa sera zinazosimamia sekta hiyo, jambo ambalo linahitaji suluhisho la kudumu kuendeleza nishati katika jamii. 

Tamasha hilo la siku tano limeandaliwa na shirika la Hivos East Africa kwa kushirikiana na kituo cha kijamii cha Energy Change Lab na kampuni ya Nukta Africa Limited lilizinduliwa Jumatatu (Novemba 26, 2018) Jijini Arusha na linawakutanisha wadau na wanahabari kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Lengo ni kubadilishana uzoefu na kujifunza namna nzuri ya kuripoti habari za nishati jadidifu ili kuzisaidia jamii zinazowanguka kuwa na vyanzo mbadala vya nishati hasa katika maeneo ambayo hayajafikiwa na umeme wa gridi ya Taifa.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Nishati Jadidifu Tanzania (TAREA), Prosper Magali amesema Tanzania ina sera na sheria nzuri zinazosimamia nishati lakini changamoto inajitokeza katika utekelezaji wake ambapo huingiliwa na wanasiasa kwa kutoa matamko ambayo huathiri utekelezaji wa miradi ya nishati jadidifu katika maeneo husika hasa vijijini. 

“Miradi yetu inaathiriwa na shughuli za kisiasa kwasababu maamuzi ya kusambaza umeme hayafanyiki kwa kuangalia mahitaji ya wananchi wa eneo husika,” amesema Magali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Miradi kutoka kampuni ya Ensol Limited.

Sambamba na hilo ni kushindwa kuoanisha mipango ya Serikali na kazi za taasisi zinazozotoa huduma ya nishati jadidifu na kusababisha mgongano wa maslahi wakati wa uzalishaji na usambazaji wa umeme

Hali hiyo inachagizwa na kutokuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na wadau wote hujikuta wakipeleka umeme sehemu moja kwa gharama kubwa bila kuzingatia uhitaji na uwezo wa watu kutumia umeme.

“Tutaendelea kufanya kazi pamoja na Serikali kuishauri maeneo yenye gharama kubwa ya kupeleka umeme watuachie sisi tuwahudumie wananchi,” amesema Magali.


Zinazohusiana:


Kwa mujibu wa wizara ya nishati, uwezo wa nchi kuzalisha umeme umefikia megawati 1,560 ambapo chanzo kikubwa ni umeme unaotokana na maji, gesi na makaa ya mawe. Matumizi ya nishati jadidifu ni mkombozi kwa wananchi wanaosubiri umeme wa gridi ya Taifa.

Wadau wengine wameelezea kuwa ukubwa wa nchi ya Tanzania ukiambatana na vijiji vingi kuwa pembezoni ambapo ni vigumu kufikiwa kirahisi kutokana na ubovu wa barabara na usafiri wa magari kutopatikana kwa wakati.

Meneja Masoko wa kampuni ya Mobisoli Tanzania inayotoa huduma ya umemejua, Seth Mathemu amesema changamoto hizo huwapa wakati mgumu kuwafikia wanavijiji wote kwa wakati mmoja, jambo linaloongeza gharama za uendeshaji kampuni kutokana na umbali na muda unaotumika kufikisha huduma kwa jamii.

“Ukubwa wa nchi na umbali wa nyumba moja hadi nyingine ni changamoto katika vijiji huongeza gharama za muda na usafiri kuwafikia wateja wetu,” amesema Mathemu. 

Mathemu amebainisha kuwa utofauti wa kodi za matangazo (branding fees) kutoka eneo moja hadi lingine, nayo ni sababu ya sekta ya nishati jadidifu kutokukua kwa kiwango kinachostahili licha ya Serikali kuondoa kodi kwenye vifaa vya sola vinavyoingia nchini. 

Ameongeza kuwa pia vipato vya wananchi wengi wanaoishi vijijini sio vya uhakika kwasababu hutegemea msimu wa mavuno ya mazao na shughuli ndogo ndogo za uzalishaji mali. Hali hii utatiza  malipo ya mikopo na gharama za kuendeleza vifaa wanavyotumika kupata umeme katika nyumba zao. 

Hata hivyo, amesisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha maeneo yote ambayo umeme wa gridi haujafika watapeleka umemejua ili kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi na kuchangia katika ujenzi wa viwanda. 

Matumizi ya nishati jadidifu ni mkombozi kwa wananchi wanaosubiri umeme wa gridi ya Taifa. Picha| OGPE Africa.

Kulingana na takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) za mwaka 2016 ni asilimia 36.6 ya watanzania ndio wameunganishiwa umeme katika nyumba zao hii ikiwa na maana kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watanzania hawapati umeme na kulazimika kutumia mafuta ya taa, kuni, mkaa kama vyanzo vya nishati ambavyo sio rafiki kwa mazingira.

Msimamizi wa kituo cha kuzalisha na umeme wa gridi ndogo ya Taifa kutoka kampuni ya Power Corner Limited, Elisha Mathew amesema sekta ya nishati jadidifu bado ina safari ndefu ikizingatiwa kuwa bado watu wengi hawana uelewa wa matumizi ya nishati hiyo, jambo linalofanya umeme huo kufika kwa watu wachache ikilinganishwa na mahitaji ya umeme.

Amesema ili changamoto hizo zitatuliwe ni vema wadau mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari kukaa na Serikali kuangalia namna nzuri ya kuondoa migongano wakati wa kuwahudumia wananchi. 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Teknolojia na Habari ya Nukta Africa Limited, Nuzulack Dausen amesema vyombo vya habari ni sehemu ya jamii, hivyo vinawajibika kuwahudumia wananchi kwa kuwapa taarifa sahihi za matumizi ya nishati jadidifu ili kufungua fursa mbalimbali ikiwemo kutengeneza kipato na kuboresha huduma za kijamii.

Hii ni mara ya tatu kwa Tamasha la Nishati kufanyika ambapo mara ya kwanza lilifanyika mwaka 2015 na mara ya pili ilikuwa Januari mwaka huu na kuwakutanisha wadau mbalimbali kujifunza na kuchukua hatua za kuisaidia jamii hasa watu waishio vijijini kutumia nishati mbadala wakati wakisubiri umeme wa gridi ya taifa.

Enable Notifications OK No thanks