Megawati 300 za umeme wa upepo kuchagiza ukuaji wa viwanda Tanzania

August 17, 2018 6:21 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Watazalisha megawati 100 katika hatua za awali zitakazoingia kwenye gridi ya Taifa.
  • Mradi huo utafanya Makambako kuwa kitovu cha uzalishaji umeme upepo.
  • Utasaidia kuboresha huduma za jamii ikiwemo afya na elimu.

Dar es Salaam. Tanzania itaanza kufaidika na ukuaji wa sekta ya uzalishaji viwandani kutokana na Serikali kuipata leseni kampuni ya Windlab Developments Tanzania kuzalisha umeme wa upepo katika mji wa Makambako mkoani Njombe utakaoingizwa kwenye gridi ya Taifa.

Kampuni hiyo kutoka Australia imepata cheti cha tathmini ya mazingira na athari za kijamii (ESIA) kwa ajili ya mradi wa uzalishaji wa umeme wa upepo wa Megawati 300 katika shamba la ‘Miombo Hewani Wind’ lililopo mji wa Makambako katikati ya makutano ya mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya.

Kwa mujibu wa kampuni ya Windlab, mradi huo utatekelezwa kwa awamu mbalimbali ambapo katika hatua za awali wamewekeza Dola za Marekani 300 milioni zaidi ya Sh680 bilioni ili kuzalisha megawati 100 katika shamba la upepo ambalo litakuwa na mashine 34 na nyaya za kusambaza umeme zitakazoungwanishwa katika kituo kidogo cha gridi ya umeme ya  Taifa cha Makambako.

Cheti cha tathmini ya mazingira kilitolewa Mei 30 mwaka huu na Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba na ilikuwa leseni ya kwanza kutolewa nchini kwa ajili ya shamba litakalotumika kuzalisha umeme wa upepo.

Uamuzi wa kufungua shamba hilo kati mji wa Makambako ni kutokana na sifa yake ya kuwa na miti mingi ya miombo ambayo ina mchango mkubwa wa kudhibiti mwelekeo wa upepo.

Ikiwa Tanzania itafanikiwa kutekeleza mradi huo, itaungana na Kenya ambayo ina shamba kama hilo katika mji wa Turkana linalozalisha megawati 300 za umeme wa upepo ambao unatumika katika shughuli mbalimbali za viwandani na nyumbani.

Taarifa zilizopo zinaeleza kuwa lengo la mradi huo wa Miombo Hewani Wind ni kuharakisha ujenzi wa viwanda na kukuza sekta ya uzalishaji nchini. Hadi kufikia Septemba mwaka huu shamba hilo litaanza kutoa umeme wa megawati 100 kwenye gridi ya Taifa.

Utekelezaji wa mradi huo ni jitihada za Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland na Windlab kutumia nishati mbadala kutunza mazingira na kukuza uchumi wa wananchi.

Akihojiwa na Jarida la Afrika Mashariki, Mkurugenzi Mtendaji wa Windlab, Roger Price amesema katika kutekeleza mradi wa Miombo Hewani, kampuni yake itatumia uzoefu ilioupata katika usimamiaji wa miradi zaidi ya 50 ya umeme wa upepo katika mabara ya Amerika Kusini, Australia na Amerika Kaskazini.

“Mwenendo wa rasilimali ya upepo unatumika zaidi kuzalisha umeme wakati wa usiku na kipindi cha kiangazi, na kuchangia ziada ya uzalishaji wa sasa wa gridi ya taifa,” amenukuliwa Price.

Awamu ya kwanza ya Miombo Hewani inatarajia kuongeza umeme katika gridi ya taifa kwa asilimia tano na kuunganisha kaya 1,000,000 nchini.

Umeme upepo ni miongoni mwa nishati mbadala ambayo ikitumia vizuri inaweza kusaidia kuhifadhi mazingira na kuongeza uzalishaji viwandani. Picha| netgazeti.net

Kulingana na takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) za mwaka 2016 ni asilimia 36.6 ya watanzania ndio wameunganishiwa umeme katika nyumba zao hii ikiwa na maana kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watanzania hawapati umeme na kulazimika kutumia mafuta ya taa, kuni, mkaa kama vyanzo vya nishati ambavyo sio rafiki kwa mazingira.

Ujio wa Windlab huenda ukaamsha matumaini mapya ya kuondokana na utegemezi wa umeme wa maji unaothiriwa zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa na kuzigeukia rasilimali zingine za gesi, jua, mafuta na makaa ya mawe.

Windalab watafanya kazi kwa karibu na wizara ya Nishati, Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), na Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) ili kuhakikisha mradi huo unakuwa sehemu ya uhifadhi wa maendeleo ya Taifa.

Enable Notifications OK No thanks