Waombaji 30,675 Heslb wapata mkopo elimu ya juu awamu ya kwanza
- Kati ya idadi hiyo, wanaume ni 19,632 sawa na asilimia 64 ya waliopata mikopo ambao ni sehemu ya wanafunzi zaidi ya 45,000 ambao watapangiwa mikopo mwaka huu.
- Awamu ya pili ya waliopata mikopo itatangazwa wiki ijayo kabla ya Oktoba 25.
- Bodi hiyo imesema haitafunga mfumo wake wa kielektroniki ili kutoa fursa kwa waombaji ambao hajakamilisha maombi wakamilishe wakifika vyuoni.
Dar es Salaam. Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu (Heslb) imetangaza orodha ya kwanza ya majina ya wanafunzi 30,675 wa mwaka wa kwanza waliopata mikopo kwa ajili ya mwaka wa masomo wa 2019/2020 yenye thamani ya Sh113.5 bilioni.
Kati ya idadi hiyo, wanaume ni 19,632 sawa na asilimia 64 ya waliopata mikopo ambao ni sehemu ya wanafunzi zaidi ya 45,000 ambao watapangiwa mikopo mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Heslb, Abdul-Razak Badru aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo (Oktoba 17, 2019) jijini Dar es Salaam, amesema orodha iliyotolewa leo ni ya kwanza lakini mchakato wa kuwapangia wanafunzi mikopo utaendelea kulingana na uhitaji na uchambuzi wa taarifa za wanafunzi wanaodahiliwa vyuoni.
Katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, Serikali imetenga Sh450 bilioni kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu, ikiwa imeongezeka kutoka Sh427 bilioni zilizotengwa mwaka uliopita.
Badru amesema Sh125 bilioni tayari zimetolewa na Serikali ili kugharimia mkopo kwa awamu ya kwanza, ambapo Sh116 bilioni zimetengwa kwa ajili ya wanafunzi wa mwaka kwanza ambao wataanza masomo hivi karibuni.
Katika awamu ya kwanza, wanafunzi waliozingatiwa ni wale wenye mahitaji maalumu wakiwemo wenye ulemavu, yatima na wale waliopo kwenye kaya zinazofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).
Akizungumzia makundi hayo, Badru amesema kati ya wanafunzi waliopata mkopo, wanafunzi 6,142 ni yatima au waliopoteza mzazi mmoja, wenye ulemavu ni wanafunzi 280 na 277 wanatoka kwenye kaya zinazofadhiliwa na Tasaf.
Pia Bodi hiyo imeangalia wanafunzi ambao wamesoma kwenye shule binafsi kwa udhamini wa mashirika mbalimbali ambapo asilimia sita ya waliopata mkopo wanatoka kwenye shule binafsi.
Mwaka huu, bodi hiyo imepokea jumla ya maombi 87,747 ambapo kati ya maombi hayo, ni maombi 82,043 sawa na asilimia 93.4 yalikuwa yamekidhi vigezo vya maombi.
Zinazohusiana
- Waombaji 10,452 Heslb wapewa siku nne kurekebisha kasoro
- Heslb yaanika kozi zitakazopewa kipaumbele mikopo elimu ya juu 2019-2020
- TCU yaanika sifa za wanafunzi kujiunga vyuo vikuu Tanzania
Awamu ya pili kutangazwa wiki ijayo
Awamu ya pili ya wataopata mikopo itatangazwa wiki ijayo kabla ya Oktoba 25, baada ya kukamilisha uchambuzi wa maombi ya mikopo kwa wanafunzi waliochelewa kukamilisha taratibu za udahili vyuoni na maombi ya mkopo mtandaoni.
“Kuna fungu la mwisho ambalo lipo katika hatua za mwisho za kupitiwa hawa wanafunzi wenye sifa na uhitaji watajumuishwa katika kundi ambalo litapangiwa mkopo katika kipindi cha wiki ijayo,” amesema Badru.
Wanafunzi waliopata mikopo wanatakiwa kuingia katika akaunti zao walizotumia kuomba mikopo hiyo, ili kuangalia asilimia za mikopo waliyopata.
Mkurugenzi Mtendaji wa Heslb, Abdul-Razak Badru aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo (Oktoba 17, 2019) jijini Dar es Salaam, amesema orodha iliyotolewa leo ni ya kwanza lakini mchakato wa kuwapangia wanafunzi mikopo utaendelea kulingana na uhitaji na uchambuzi wa taarifa za wanafunzi wanaodahiliwa vyuoni. Picha|Rodgers Raphael.
Naye Mkurugenzi wa Uchambuzi na Upangaji Mikopo wa bodi hiyo, Dk Veronica Nyahende amesema bado kuna wanafunzi takribani 1,000 ambao hawajamalizia kukamilisha taarifa zao katika maombi waliyowasilisha.
Amesema wengi wamewasilisha fomu zao za kuombea mkopo zikiwa hazijakamilika huku baadhi ya tarifa muhimu zikikosekana zikiwemo sahihi na vyeti muhimu vikiwemo vyeti vya kuzaliwa na kuhitimu elimu ya sekondari.
Hata hivyo, baada ya kutoa orodha ya kwanza ya majina ya waliopata mikopo, bodi haitafunga mfumo wake wa kielektroniki ili kutoa fursa kwa waombaji ambao hajakamilisha maombi wakamilishe wakifika vyuoni.
Septemba 9, 2019, alipotembelea ofisi za bodi hiyo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha aliiomba bodi hiyo kuwasaidia waombaji ambao maombi yao hayajakamilika kwa sababu wapo baadhi wanakabiliwa na changamoto zao teknolojia, licha kuwa wana vigezo vyote vya kupata mikopo.
Mikopo hiyo husaidia wanafunzi kuweza kumudu gharama za masomo na maisha wakati akisaka elimu hiyo ya juu. Wangapi watatoboa kwenye orodha ya awamu ya pili ya Heslb? Usikose kufuatilia habari za Heslb katika tovuti ya www.nukta.co.tz na mitandao.