Wakulima wa mahindi walivyopoteza zaidi ya Sh10,000 kwa gunia Tanzania

Daniel Samson 0126Hrs   Novemba 30, 2021 Biashara
  • Bei ya zao hilo kwa mwaka mmoja unaoishia mwezi Septemba imeshuka kwa asilimia 18.6.
  • BoT yasema hali hiyo inatokana na kuwepo kwa chakula kingi sokoni. 

Dar es Salaam. Wakulima wa mahindi nchini Tanzania wamepoteza zaidi ya Sh10,186 kwa kila gunia la kilo 100 ndani ya mwaka mmoja uliopita, huku bei ya zao hilo la chakula ikishuka kidogo kwa mwezi mmoja uliopita.  

Ripoti ya Mapitio ya Uchumi kwa mwezi Oktoba 2021 (Monthly Economic Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza kuwa wastani wa bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi mwaka kwa ulioishia Septemba 2021 ilikuwa ShSh54,551 ikiwa imeshuka kutoka Sh44,365 iliyorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

Bei hiyo ya Septemba mwaka huu ipo chini kwa asilimia 18.6 ikilinganishwa na ya mwaka jana.

Hii ni sawa na kusema wakulima wa mahindi wamepoteza Sh10,186 kwa kila gunia la kilo 100 mwezi Septemba mwaka huu ikilinganishwa na walichouza Septemba 2020. 

Uchambuzi zaidi wa takwimu hizo za BoT unaonyesha kuwa bei ya zao hilo umeshuka kidogo ndani ya mwezi mmoja uliopita kutoka Sh44,811.7 Agosti hadi hadi Sh44,365 Septemba mwaka huu kwa bei ya jumla.

“Kushuka kwa bei ya mazao kunatokana na kuwepo kwa chakula cha kutosha masokoni kuliko changiwa na hali ya hewa nzuri katika msimu wa 2020/21,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo ambayo pia inapatikana katika tovuti ya BoT.Kushuka kwa bei hiyo ya mahindi kunawanufaisha zaidi wanunuzi hasa walaji kwa kuwa hawalazimiki kutoboa zaidi mifuko yao kupata chakula hicho muhimu na utengenezaji wa bidhaa viwandani. 

Lakini wakulima ambao wamewekeza kulima zao hilo, kwao ni maumivu  kwa sababu inawapunguzia faida ambayo wangepata endapo wangeuza kwa bei ya juu au sawa na ile waliyouza Septemba 2020. 

Mahindi ni miongoni mwa mazao makuu ya chakula nchini Tanzania yanayojumuisha mchele, maharage, viazi mviringo, mahindi, mtama, uwele, ulezi na ngano.

Bei za mahindi ndani ya mwaka mmoja uliopita zimekuwa zikipanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya uzalishaji, hali ya hewa na gharama za usafirishaji. 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa bungeni Septemba 2 mwaka huu alisema Serikali imeshatoa Sh15 bilioni kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili kununua mahindi kutoka kwa wakulima.

“Uzalishaji wa mahindi ni mkubwa lakini na sisi pia tumeimarisha hifadhi yetu ya Taifa ya chakula (NFRA) tumeipa fedha za kwenda kununua mahindi kwa bei ya kumuwezesha mkulima ili ajikimu hadi msimu ujao,” alisema Majaliwa. 

Hatua hiyo ililenga kuwapa ahueni wakulima ambao wamekuwa na malalamiko ya kuwa na mahindi mengi yaliyokosa soko na hivyo kuwaweka katika hatari ya kupata hasara.

Ununuzi huo umesaidia kuongea akiba ya NFRA. Hadi kufikia Septemba 2021, NFRA ilikuwa na akiba ya chakula tani 150,057 zikiwa zimeongezeka kutoka tani 123,635 za mwezi Agosti mwaka huu.

 

Bei za mazao mengine ya chakula

Pia katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita unaoishia Septemba 2021,  bei za mazao yote ya chakula zilishuka isipokuwa uwele na mtama. 

Bei ya jumla ya uwele hadi Septemba 2021 ilikuwa Sh54,093  ikipanda kutoka Sh123,233 iliyorekodiwa Septemba 2020. 

Mtama ulipanda hadi Sh90,696 kutoka Sh82,150 iliyorekodiwa kipindi kama hicho mwaka jana. 

Related Post