Wahitimu kidato cha nne 2023 ruksa kubadili tahasusi, chuo

Lucy Samson 0656Hrs   Machi 20, 2024 Habari
  • Ni baada ya Serikali kuongeza tahasusi mpya 49 na kufikisha 65.
  • Usajili wa wanafunzi katika tahasusi hizo utafanyika kwa njia ya mtandao kuanzia leo Machi 20 hadi Aprili 30, 2024.
  • Serikali yasema haitatoa muda wa ziada baada ya usajili kufungwa. 


Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imefungua usajili wa tahasusi mpya kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga wa kidato cha tano mwaka 2024 katika mwaka wa masomo utakaoanza Julai 2024 huku ikitoa nafasi ya kubadili tahasusi kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka 2023.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),  Mohamed Mchengerwa aliyekuwa akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo Machi 20, 2024 amesema fursa hiyo itawaandaa wanafunzi kuwa wataalamu katika fani mbalimbali wanazozipenda.

“Tamisemi imetoa fursa kwa wanafunzi kubadili machaguo yao ili kutoa nafasi kwa wanafunzi kusoma tahasusi au kozi itakayomuandaa kuwa na utaalamu stahiki katika maisha yake ya baadae…

….Ni matumaini yangu kuwa wahitimu wote watatumia kwa ukamilifu fursa waliyopewa ya kubadilisha tahasusi na kozi kulingana na ufaulu waliopata na kutumia fursa ya uchaguzi wa tahasusi mpya zitakazoanza kufundishwa mwezi Julai mwaka 2024,” amesema Mchengerwa.


Soma zaidi:Tanzania yajipanga kukabiliana maafa ya mionzi na kemikali


Kwa mujibu wa Mchengerwa usajili wa wanafunzi katika tahasusi hizo utafanyika kwa siku 40 kunzia Machi 20 hadi Aprili 30 mwaka 2024, ambapo wanafunzi watapata nafasi ya kuchagua kati ya tahasusi mpya 49 na kufanya mabadiliko ya zile walizochagua awali kwa njia ya mtandao.

Usajili wa wanafunzi katika tahasusi hizo mpya 49 ni sehemu ya maboresho ya mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023 ambayo imelenga kuongeza ubora wa elimu kwa kuzingatia mahitaji ya sasa.

Katika maboresho hayo Serikali imeanzisha  tahasusi mpya zilizojikita katika maeneo saba ikiwemo sayansi ya jamii, lugha, masomo ya biashara, sayansi, michezo, sanaa, na elimu ya dini ambapo tayari maandalizi ikiwemo walimu na vifaa vya kufundishia yamekamilika.


Jinsi ya kubadili tahasusi au chuo

Ili kubadili au kuchagua tahasusi mpya Mchengerwa amesema mwanafunzi atalazimika kutumia mfumo wa uchaguzi wa wanafunzi (MIS) unaopatikana kupitia kiunganishi cha Selform.Tamisemi.go.tz.

Baada ya kuingia katika kiungo hicho mwanafunzi atahitajika kutumia namba ya mtihani, jina lake la mwisho, mwaka wa kuzaliwa na alama za ufaulu katika somo lolote ambalo mfumo utauliza ili kuanza kufanya uchaguzi wa tahasusi.

Aidha, Mchengerwa amewataka wanafunzi na wazazi kutumia muda uliotolewa vizuri kwa kuwa Tamisemi haitatoa muda wa ziada mara baada ya dirisha la kufanya uchaguzi kufungwa na ikiwa watakutana na changamoto yoyote watafute ushauri wa kitaaluma au kuwasiliana na kituo cha huduma kwa wateja cha wizara hiyo.

“Kubadilisha tahasusi ni bure na endapo wanafunzi wakipata changamoto wawasiliane na ofisi kwa barua pepe au kupitia kituo cha huduma kwa wateja kwa namba 255262160210 au 255735160210,” amesema Mchengerwa.

Related Post