Tanzania yajipanga kukabiliana maafa ya mionzi na kemikali

Mwandishi Wetu 1050Hrs   Machi 14, 2024 Habari
  • Yatoa mafunzo kwa vijana wa kitanzania dhidi ya dharura za kikemikali na kimionzi.
  • Waziri Majaliwa azitaka wizara zinazohusika kutekeleza miongozo ya kimionzi na kikemikali kwa  kwa vitendo.


Dar es Salaam.Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuimarisha usalama wa nchi na mipaka yake dhidi ya majanga mbalimbali ikiwemo yanayotokana na mionzi na kemikali.

Majaliwa ametoa kauli hiyo katika hafla ya ufungaji wa mafunzo ya zoezi la utayari dhidi ya dharura za kikemikali na kimionzi iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo Machi 14, 2024.

Hafla hiyo pia iliambatana na uzinduzi wa Mipango wa Kitaifa wa Maafa ya Kikemikali, Kibaiolojia, Kiradiolojia na Kinyukilia. (CBRN National Action Plan) na Mpango wa Kuitikia wakati wa Dharura za Kinyuklia na Kiradiolojia (Radiological and Nuclear Response Plan).

Aidha, Majaliwa amezitaka wizara zote na taasisi zinazohusika kuitumia kikamilifu na mipango hiyo na kusimamia utekelezaji wake.

“Miongozo hii isiwe ni nyaraka za makabatini tu bali iwe miongozo ya utekelezaji wa hatua thabiti za kuhakikisha tunajenga nchi imara na salama,” amesema Majaliwa.


Soma zaidi:Rais Samia awafunda wakuu wa mikoa, awataka kusimamia haki, kupunguza migogoro ya ardhi


Nyaraka zilizozinduliwa leo zimemeweka mikakati ya pamoja ya kitaifa ya namna ya kukabiliana na kujikinga na majanga yatokanayo dharura za kikemikali, kibaiolojia, kiradiolojia na kinyuklia. 

Kwa mujibu wa Majaliwa nyaraka hizo pia zimezingatia masuala muhimu ya kisera, uzoefu wa kukabiliana na majanga ya kitaifa na kimataifa pamoja na matakwa ya kisheria na itifaki za kimataifa.

 Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema mafunzo ya zoezi la utayari dhidi ya dharura za kikemikali na kimionzi yaliyofanyika kwa vijana wa kitanzania yalilenga kuwapa washiriki maarifa na ujuzi wa kukabiliana na vitisho vya kikemikali, kiradiolojia, kinyuklia pamoja na kusaidia juhudi kujiandaa na kukabiliana na majanga hayo nchini.

“Lengo kuu la mipango hii ni kuweka mikakati ya pamoja kama Taifa ya namna ya kukabiliana na kujikinga na majanga hayo,” amesema Mkenda.

Related Post