Gumzo Bungeni: Magari ya Serikali kuwepo maeneo ya starehe

Sayuni Kisige 0843Hrs   Aprili 08, 2024 Habari
  • Ni magari yanayopaki maeneo hayo baada ya muda wa kazi. 
  • Wabunge wahoji ni lini tabia hiyo itakoma.
  • Serikali yasema itachukua hatua. 


Dar es salaam. Serikali imetoa onyo kwa watumishi wa umma kutumia magari yake kwa matumizi binafsi ikiwemo kupaki sehemu za starehe mara baada ya saa za kazi kwani ni kinyume na sheria.

Naibu Waziri wa Ujenzi Godfrey Kasekenya aliyekuwa akizungumza leo Aprili 8, 2024 Bungeni jijini Dodoma amesema, Serikali kupitia Waraka wa Rais Na.1 wa mwaka 1998 wa kubana matumizi ilielekeza kuwa magari yote ya Serikali yanatakiwa kuwa yameegeshwa sehemu zilizotengwa ifikapo saa 12:00 jioni. 

Ameongeza kuwa kama siyo muda wa kazi  inatakiwa magari hayo yawe na kibali rasmi kinachoruhusu kuwepo barabarani baada ya saa 12:00 jioni.

“Serikali kupitia Kanuni namba 21 Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za mwaka 2009, imezuia watumishi wa umma kutumia magari ya Serikali kwa matumizi binafsi…

“… mtumishi anayekwenda kinyume na maelekezo hayo anatakiwa kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu,” amesema Kasekenya.

Naibu Waziri huyo ametoa ufafanuzi huo wakati akijibu swali la Mbunge wa Arumeru Magharibi Noah Saputu aliyetaka kujua ni lini Serikali itazuia kupaki magari ya Serikali sehemu za starehe baada ya saa za kazi.

Naye Mbunge wa Makete, Festo Sanga akiuliza swali la nyongeza amesema kanuni zipo lakini bado tabia hiyo haijakoma kwa baadhi ya watumishi. 

“Licha ya kwamba sheria na kanuni zimekuwepo zikizuia kama ambavyo mheshimiwa Naibu Waziri amesema lakini bado kwenye mitaa, kwenye baa na maeneo mengine magari ya Serikali yamekuwa yakionekana majira ya usiku.

“Upi mkakati wa Serikali kuhakikisha inazuia kabisa uwepo wa magari maeneo hayo kwa sababu imekuwa ni kero kwa wananchi lakini pia inaonesha ni matumizi mabaya ya fedha za Serikali?,” amehoji  Sanga.

Akijibu swali hilo, Kasekenya amesema kwa kuwa sheria, kanuni na taratibu zipo, wahusika wanatakiwa kusimamia ipaswavyo sheria hizo ili kudhibiti suala hilo.

“Tunawakumbusha na kuwasisitiza maafisa masuuli na waajiri wote wanaohusika waweze kuchukua hatua,” amesema Kasekenya.


Related Post