Mustakabali wa kikokotoo cha mafao bado kizungumkuti Tanzania

May 2, 2024 4:53 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Serikali yasema inafanya tathmini na uchambuzi wa mabadiliko ya kikokotoo hicho.
  • Rais wa Tucta asema suala hilo bado lina malalamiko na manung’uniko kutoka kwa wafanyakazi.
  • Nyongeza ya mshahara yanukia.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema inafanya tathmini na  uchambuzi wa mabadiliko ya kanuni ya kikokotoo cha pensheni ya wastaafu kabla ya kutangaza uamuzi mpya baada ya wafanyakazi kulalamika kutoridhishwa na kikokotoo kinachotumika hivi sasa.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Philip Isdory Mpango aliyekuwa akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yaliyofanyika kitaifa katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, amesema suala la mabadiliko ya kikokotoo linahitaji tathmini ya kina.

“Uamuzi wa kubadilisha kikokotoo ni lazima utokane na tathmini ya kina ya kisayansi ya watakwimu bima, ni maoni yetu kuwa Tucta (Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi) itashiriki kikamilifu katika zoezi hilo na kuwasilisha maoni yatakayoimarisha zaidi mfuko,” amesema Dk. Mpango.


Soma zaidi:Ripoti: Afya ya akili chanzo cha watu kujiua, kuua Tanzania


Kwa muda sasa wafanyakazi wamekuwa wakilalamikia kikokotoo hicho cha mafao kilichoanza kutumika Julai 1, 2022, ambapo wastaafu hupewa asilimia 33 ya mafao na kiasi kinachobaki hulipwa kidogo kidogo.

Rais wa Tucta Tumaini Nyamekye, aliyekuwa akizungumza katika sherehe za Mei Mosi, 2024 amemwambia Makamu wa Rais Dk. Mpango kuwa suala hilo bado lina malalamiko na manung’uniko ya wafanyakazi.

Itakumbukwa kuwa Septemba, 2023 Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akizungumza katika mkutano mkuu wa mwaka wa Maafisa Wakuu Waandamizi wa Jeshi la Polisi Jijini Dar es Salaam alisema Serikali yake inafanyia kazi suala la kikokotoo baada ya kuibuliwa katika mkutano huo.

“Masuala ya kikokotoo haya si tu matakwa ya Serikali ni hali ya uchumi na mifuko yenu…kwa sababu kimepigiwa kelele sana si tu na jeshi la polisi lakini na wengine.

Tutakwenda kuangalia tuone njia nzuri tunayoweza kufanya ili kikokotoo kisilete maneno mengi,” alisema Rais Samia.

Hata hivyo, kwa siku za karibuni wabunge wamekuwa wakipigia kelele suala hilo, wakiitaka Serikali kutizama upya kikokotoo kwa kuwa ni haki ya wastaafu ambao walifanya kazi kuitumikia nchi yao.

Nyongeza ya mshahara yanukia

Akizungumza katika maadhimisho hayo Dk. Mpango amesema Serikali inaendelea kufanyia kazi maombi ya nyongeza ya mshahara ili kuwawezesha wafanyakazi hao kumudu gharama za maisha.

Mpango amebainisha kuwa ikiwa uchumi wa Tanzania utaendelea kukua kwa kasi basi Rais Samia Suluhu anaweza kutangaza ongezeko la mishahara hivi karibuni.

Aidha, wafanyakazi hao pia waliomba Serikali kuangalia upya suala la likizo ya uzazi hususani kwa wazazi wa watoto njiti ambao hawapewi muda wa likizo wa kutosha kuhudumia watoto hao.

Akijibu hoja hiyo Dk. Mpango amesema Serikali itafanyia marekebisho sheria ya ajira ili likizo ya uzazi kwa watoto njiti ianze pale mtoto atakapomaliza kipindi cha uangalizi maalum pale madaktari watakapothibitisha.

“Likizo ya uzazi itaanza pale mtoto atakapomaliza muda wa uangalizi maalum, mfanyakazi ataruhusiwa kutoka kazini saa saba na nusu kwa muda wa miezi sita ili kumpa fursa ya kwenda kunyonyesha,” ameongeza Dk. Mpango.

Mbali na hoja ya hizo wafanyakazi hao kupitia Tucta waliibua hoja nyingine ikiwemo vitita vipya vya bima ya afya, suala la mikataba ya kudumu na kodi ambazo zote zilipata majibu kutoka kwa Serikali.

Enable Notifications OK No thanks