Unayopaswa kuzingatia kabla ya kufanyiwa “massage”

Joshua Sultan 0242Hrs   Juni 13, 2020 Maoni & Uchambuzi
  • Iwapo muhusika ana maambukizi ya ngozi, kidonda wazi au kidonda cha upasuaji si vyema kufanya huduma hii hasa bila utaalamu.
  • Isipofanyika vizuri inaweza kusababisha maumivu ya mgongo. 
  • Mazingira inapofanyika yanatakiwa yawe safi na vifaa vinavyokidhi vigezo vya kitaalamu.

Rafiki yangu mmoja mcheshi sana ananipigia simu, yupo katikati ya jiji huyu.

Ananiambia “daktari niko njiani nakuja, lakini kabla ya hapo acha nipitie mara moja saluni moja hapa ina kitengo cha “SPA” nikandwe kandwe misuli kidogo” akimaanisha kwa kwamba apate huduma ya kuchua au kama ilivozoeleka “massage”. 

Majuma mawili yaliopita, mhariri wangu wa makala haya alienieleza nae daktari naomba uongelee suala hili la “massage”. Nitatumia neno la massage badala ya kuchua ili tuende sawa kabisa maana ndilo neno lililozoeleka miongoni mwa watu.

Massage ni huduma inayohusisha uchuaji na unyumbulifu wa tishu laini za mwili yaani ngozi, misuli, tendoni, maungio na sehemu za mwili ila kuleta matokeo chanya katika utendaji kazi wa tishu hizi. 

Huduma hii ipo katika milengo miwili yaani ule wa tiba na ule wa kujiburudisha/maburudisho (recreation). Kuna wataalamu maalum ambao hutoa huduma hii ambao huitwa “masseuse” na wengine husomea utoaji wa huduma hii. 

Maduka mengi ya urembo hutoa huduma hii kwa lengo la maburudisho na mapumziko. 

Pamoja na faida chache kama hizo, kuna mambo muhimu ya kuzingatia. Iwapo muhusika ana maambukizi ya ngozi, kidonda wazi au kidonda cha upasuaji si vyema kufanya huduma hii hasa bila utaalamu. Picha| Elemental.


Faida zake

Kuna faida kadhaa zitokanazo na huduma hii. Massage huimarisha mzunguko wa damu na kuchochea uondoshaji wa taka zitokanazo na utendaji kazi wa seli. Hii hupunguza kukakamaa kwa misuli na hivyo kuimarika.

Massage pia huchochea kulegea kwa akili na kupumzisha mwili. Uchovu unaojengeka ndani ya mwili kutokana na utendaji kazi wa misuli unaohitajika kuondoshwa. Massage huleta msisimko wenye kupumzisha akili utokanao na kuguswa kwa neva juu ya ngozi. 


Zinazohusiana:



Unayopaswa kuzingatia

Pamoja na faida chache kama hizo, kuna mambo muhimu ya kuzingatia. Iwapo muhusika ana maambukizi ya ngozi, kidonda wazi au kidonda cha upasuaji si vyema kufanya huduma hii hasa bila utaalamu.

Pili ni uchaguzi wa aina za vilainishi, kuzingatia usafi na unadhifu wa mikono na kucha kwa muhusika anaefanya huduma hii. 

Tatu ni kuwa makini kutofanya katika majeraha mapya ya misuli au tishu zinginezo. Hali hii huchochea maumivu na kuweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi.

Nne, kuwa makini na maeneo ya mgongo. Nimeona baadhi ya sehemu inapotolewa huduma hii hukandamiza eneo la mgongo na uti wa mgongo. 

Kitendo hiki ni hatari iwapo kuna matatizo ya pingili ama diski za mgongo. Aghalabu inaweza tokea kusababisha ajali katika eneo hili na kusababisha madhara makubwa.

Ni vizuri kuwa na utaratibu wa kupata huduma hii, lakini katika hilo ni vyema kuzingatia viwango vya eneo hilo ikiwemo usafi wa mazingira, vifaa, mtindo pamoja na kanuni za kimaadili.

Nipo!

Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mazoezi tiba na mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.


Related Post