Tahadhari ya kuchukua kuepuka uume kuvunjika
- Kuvunjika kwa uume kunaweza kutokea wakati wa kufanya mapenzi, kujichua (masturbation), kupindishwa kwa lazima na kulala vibaya.
- Tatizo hutoke zaidi wakati wa kufanya mapenzi.
- Kuwa makini wakati wa kufanya mapenzi, na ukipata tatizo nenda hospitali.
Katika hali ya kawaida tumezoea na tunafahamu kuwa mifupa ndiyo huvunjika na kitaalamu inajulikana kama “fracture”.
Lakini ni mara chache kusikia uume wa mwanaume unavunjika kama inavyotokea kwa mifupa pale inapopata hitilafu au ajali. Kama ulikuwa hujui, basi uume nao unaweza kuvunjika na kwa lugha ya kitaalamu hujulikana kama “Penile Fracture”.
Kuvunjika kwa uume huchukuliwa kama ni dharula ya kitabibu katika idara ya urolojia inayohujika na matibabu ya magonjwa ya njia ya mkojo.
Kimsingi uume umeundwa kwa tishu ambazo ni nyama tupu mithili ya godoro. Tunaposema uume umevunjika ni kuchanika kwa tabaka (layer) la mishipa ya uume, kitaalamu huitwa corpus cavernosum.
Anatomia ya uume ina sehemu kuu tatu; mzizi, mwili na mrija wa mkojo. Mwili wa uume unachukua nafasi kubwa na umefunikwa na tabaka hilo la corpus cavernosum ambalo huufanya uume kusimama pale ambapo mishipa hiyo inapojaa damu.
Tabaka lingine ni la “corpus spongiosum” ambalo hufunikwa na tishu ngumu ambazo huitwa “tunica albuginea”. Kisha sehemu zote tatu zinafunikwa na nyuzi za tishu.
Zinazohusiana:
- Teknolojia ya kisasa kuongeza ufanisi matibabu ya figo Muhimbili
- MOI kuanza upasuaji wa ubongo kwa teknolojia ya kisasa
Shida inaanza uume unapokuwa umesimama
Katika hali ya kawaida uume unapokuwa umelala ni vigumu kuvunjika au kupata shida yoyote kwa sababu unakua mlaini na rahisi kujikunja. Pale uume unaposimama hapa ndipo shida inapoweza kutokea.
Damu huingia na kuufanya uume kusimama na kutokuwa na uwezo wa kujikunja kunja (low mobility). Tishu zinakua nyembamba na kupungua uwezo wake wa kuvutika na kuwa ngumu.
Ukiwa katika hali hiyo, uume iwapo utapindishwa au kukunjwa ghafla, tabaka lake la “tunica albuginea” ambalo liko kama mfuko linaweza kuchanika kwa takriban sentimita 0.5 hadi nne.
Msukumo ukiwa mkubwa unaweza kuchana matabaka mengine yaliyo chini hadi kufikia mshipa wa mkojo.
Kuvunjika kwa uume kunaweza kutokea wakati wa kufanya mapenzi, kujichua (masturbation) na vyanzo vingine kama kupindishwa kwa lazima na kulala vibaya.
Kama ulikuwa hujui, basi uume nao unaweza kuvunjika na kwa lugha ya kitaalamu hujulikana kama “Penile Fracture”.Picha|Mtandao.
Asilimia kubwa ya kuchanika kwa uume, hutokea wakati wa kufanya mapenzi hasa pale mwenzi wa kike anapokua juu. Uzito wote unakua juu ya uume. Ikitokea uume ukateleza nje na kugonga mfupa wa nyonga ya juu (symphysis pubis) basi uzito wa mwenza utakua juu ya uume na kusababisha kuchanika.
Ni muhimu kuwa makini wakati wa kufanya mapenzi hasa uume unapokuwa umesimama ili kujilinda na hatari yoyote inayoweza kutokea. Hakikisha uume umeingia vyema katika uke na kwamba uke uwe umelainika vya kutosha.
Ikitokea zoezi limekuwa refu na uke bado ni mkavu, badilisheni mkao wa mapenzi. Na ikitokea uume umevunjika fika hospitali ufanyiwe upasuaji ambao ni tiba ya tatizo hili.
Dk Joshua Lameck Sultan ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba katika Chuo cha Tiba na Sayansi Shirikishi Moshi (KCMC) pamoja na hospitali ya KCMC. Pia ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) ambapo hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.