Uchumi wa nywele: Mitindo, njia mbalimbali za kutunza nywele za asili

Rodgers George 0130Hrs   Agosti 12, 2020 Ripoti Maalum
  • Je, ni bidhaa za dukani au bidhaa asilia? 
  • Wanaoshindwa, waelezwa ni wapi wanapokwama.
  • Kwa kutunza nywele asili, unapata faida ya kuchagua kusuka, kubana na hata kuweka mitindo mingine ya rasta.

Dar es Salaam. Pamoja na urembo wa nywele asilia kuvutia watu wengi, uelewa mdogo kuhusu utunzaji wake huenda ikawa ni moja ya sababu  zinazowakwamisha wengine kuungana na wanawake wenye  nywele asilia. Mbali  na sababu hiyo, wapo wanawake ambao nywele zao wanaziona haziridhishi ikiwa ni pamoja na ukuaji na kujaa kwa nywele kichwani.

“Niliweka kila kitu. Kila dawa ninayomudu nimetumia lakini nikikutolea hili wigi, utashangaa kuona “tunywele” “nilitonato,” amesema Regina Simon mkazi wa jijini Arusha.

Jambo hilo huenda ni sababu ya baadhi ya wanawake kuamua kukata nywele au kuvaa mawigi yaliyotengenezwa kwa katani au nywele za watu kwa kuwa wanashindwa kujua njia inayofaa inafaa kutunza nywele asilia za kiafrika.

Baada ya kuona kwanini wanawake wengi wanapendelea nywele asilia kwa sasa, leo tunaangazia njia mbalimbali wanazotumia baadhi ya wanawake wenye nywele za asili.

Kila mwanamke ana njia yake ya utunzaji wa nywele za asili lakini sehemu kubwa wanatumia karibu njia na mitindo inayofanana.

Baadhi ya wanawake wenye nywele za asili na wataalamu wa nywele katika baadhi ya saluni jijini Dar es Salaam wameaimbia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa  baadhi ya wenye nywele asilia wanatumia maparachichi, vitunguu swaumu huku wengine wakitumia hadi mayai katika kuhakikisha nywele zao zinaendana na urembo wao wa usoni.

Mbali na waliochagua njia za asili kabisa, wapo ambao wanatumia vitu vya dukani kuhakikisha nywele zao haziharibiki.

Kila mwanamke ana njia yake ya utunzaji wa nywele za asili lakini zipo baadhi ambazo kundi kubwa wanatumia. Picha| Addiah Natural and Beauty Bar .

Ugumu wa kutunza nywele asilia upo wapi?

Ni vigumu kutumia bidhaa ambazo sio za nywele za kiafrika maarufu kwa Kiingereza kama ‘Kinky hair’ katika jitihada za kuzitunza. 

Mfanyabiashara wa mapambo na maua wa Morocco Jijini Dar es Salaam Salama Masoud amesema, kwa kawaida, mtu aliyeweka dawa (relaxer), anaweza kutumia bidhaa za dukani za mtu mwenye nywele asilia na sipate changamoto ya nywele zake kwani tayari mfumo wa nywele zake umeshabadilishwa lakini hali nitofauti kwa waliochagua nywele asilia.

Hali hiyo inalazimisha mtu kuhakikisha kuwa anazihudumia nywele zake yeye mwenyewe hasa kama hafahamu ni bidhaa zipi zinamfaa.

“Kuna bidhaa nyingi sokoni na kujua ipi ina kufaa ni mtihani. Utajaribu hii, itakataa, utajaribu ile itakataa pia. Kutunza nywele hizi, inahitaji uvumilivu sana na jitihada za kuomba ushauri kwa wataalamu wa nywele,” anaeleza Salama ambaye yeye, amefanikiwa kuzipata bidhaa zinazomfaa kufunza nywele zake za asili. 

Mbali na hilo, Salama amesema nywele za kiafrika zinahitaji unyevunyevu hivyo kwa mtu anayeshindwa kuzihudumia kwa namna hiyo, atalalamika kuwa nywele ni ngumu na zinajifunga funga ama kukatika.

“Mtindo huu unakuhitaji kutembea na chupa ya maji ya kujipulizia. Ni ngumu lakini ukizoea unaona kawaida,” anaelezea mrembo huyo.


Zinazohisiana


Bidhaa za dukani au za nyumbani: Nani rafiki wa kweli wa nywele za asili?

Katika utunzaji wa nywele za kiafrika, kuna aina mbili, moja ikiwa ni kutumia bidhaa za vyakula zikiwemo maparachichi na mayai na ya pili ikiwa ni kutumia bidhaa za dukani zilizotengenezwa maalum kwa kutunza nywele za asili ya kiafrika.

Simulizi za wanaotumia vitunza nywele vya dukani

Asimwe Ruta, ambaye amekuwa akitunza nywele zake asilia kwa miaka sita sasa, anasema hapendi kusuka hivyo mara nyingi huchana nywele zake na kuzibana kimtindo, jambo linalompunguzia gharama na hivyo kutumia Sh100,000 kwa miezi miwili na nusu. 

“Nikitaka kubana nywele zangu, ninazipulizia maji kidogo kisha ninazipaka mafuta (Aunty Jackie’s conditioner), ninazichana na kuzibana vema kwa mtindo wowote ninaoupenda,” anasema Asimwe.

Kwa wanawake kama Zamdazitta Kumbakumba, Mhandisi wa masuala ya usalama anayeishi wilayani Rufiji mkoani Pwani, mtindo rahisi kwake ni kuzisuka, kuchana na kuzibana au kuziweka katika mtindo wowote anaoupenda.

“Niliwahi kuweka dawa lakini nywele zangu ziliishia kuwa nyembamba sana. Sikuzipenda hivyo nilinyoa na kuanza upya,” amesema Zamdazitta ambaye mara nyingi huvalia hijab hivyo kulazimika kuzihudumia nywele zake asilia yeye mwenyewe.

“Pesa nayoikoa kwenda saluni inanisaidia kununua kila kitu kuanzia vitana, mafuta ya kimiminika, hairfood (mafuta yenye chakula cha nywele) na hata sabuni ya kuoshea nywele. Vinakaa hadi miezi mitatu,” analezea Zamdazitta ambaye ni mara chache sana huenda saluni kuhudumia nywele zake. 

Kuhudumia nywele asilia kunahitaji uvumilivu kwani zinachukua muda mwingi. Picha| Addiah Natural and Beauty Bar.

Matumizi ya bidhaa za dukani yanaweza kuongeza gharama za utunzaji nywele asilia. Wale wanaotumia vitunza nywele vyenye majina maarufu na wanaohudumiwa kwenye saluni gharama zao huwa juu kidogo kuliko wanaaotumia bidhaa zenye bei nafuu.  Hata hivyo, mara nyingi vitunza nywele vingi havitumiki siku moja tu bali ni miezi miwili au zaidi kulingana na matumizi yako.

Kwa mujibu wa Asimwe na Zamdazitta, kiungo muhimu katika kuhudumia nywele za asili ni maji kwa kuwa ndicho kitu ambacho watu wengi hawakijui na huwafanya wakate tamaa pindi wanapoona nywele ni ngumu na zinakatika au kujifunga.

“Nywele aina ya 'Kinky' (asili ya Kiafrika) ni ngumu kiasilia. Hivyo zinahitaji maji ili kuweza kuzimudu,” anasema Zamdazitta ambaye hupulizia maji nywele zake kila anapovua hijabu yake tayari kwa kulala.

‘Steaming’ za vitunguu swaumu, parachichi?

Salama anasema alishauriwa na wataalamu kuwa bidhaa za dukani kwa ajili ya nywele asilia zimetengenezwa na malighafi za chakula na siyo kemilali hivyo angalau ni salama kuliko zile za karikiti.

“Kuna steaming (Vivukizo)  za vitunguu swaumu, parachichi na vingine vingi. Japo mtu unaweza kuzitengeneza mwenyewe lakini kama huna muda hata vya dukani unaweza kutumia,” anaeleza. 

Kati ya wanawake waliochagua kujitengenezea steaming yao ya asilia wenyewe ni Mwalimu wa watoto kutoka Shule ya Maitarya Jijini Dar es Salaam, Flora Harrison ambaye anachanganya mayai, asali na parachichi kutengeneza chakula kwa ajili ya nywele zake.

Flora anasema kwa kufanya hivyo, inamsaidia nywele zake kutokukatika  na kuwa na afya pamoja na kuokoa gharama.

Kwa bei ya kawaida, mayai mawili ya kienyeji yanagharimu Sh1,000, maparachichi mawili kati ya Sh1,000 na Sh2,000 na asali inayogharimu Sh10,000 kwa nusu lita.

Hata hivyo, mbali na gharama za umeme fahamu kuwa hauwezi kuitumia asali yote kwa siku moja.

Hii ina maana kuwa ukijumuisha gharama za asali na mafuta ya nazi ya Sh10,000 ambayo Flora anatumia, kwa mwezi anagharamia Sh23,000 kutunza nywele zake nyumbani.

“Naziosha kila mara. Ninapozifumua, naziosha kwa maji ya bomba yasio na chumvi, nazipaka mafuta  na ninazinyoosha kwa kuwa zinakuwa zimejikunja kunja. Kila baada ya mwezi huwa nazifanyia “steaming,” amesema Flora aliyeelezea steaming au kujifukiza kuwa ni chakula muhimu cha nywele.


Matumizi ya baadhi ya bidhaa za chakula kutunza nywele yanaonekana kutumiwa na kina mama wengi wenye nywele hizo licha ya kuwa huduma zake kuchukua muda kidogo kwa baadhi ya mitindo

Mkazi wa Mbeya mjini Rachel Essau anasema nywele asilia kwake hazina gharama kama watu wanavyo dhani ikilinganishwa na nywele za dawa (relaxed hair) zaidi ya kuchukua muda wake kidogo katika kuziandaa.

Dada huyo, ambaye ameshasahu mara ya mwisho kutumia relaxers,  anasema matumizi ya bidhaa za chakula katika kutunza nywele zake ni salama kwa kuwa zinapatikana karibia kila sehemu na njia hizo hazina madhara kwa mtumiaji. 

Rachel ameiambia Nukta kuwa gharama pekee anayoiona katika utunzaji wa nywele asilia ni muda unaotumika kwa kuwa unatakiwa kutenga siku maalumu kwa ajili ya kuziosha nywele zako, jambo linaloweza kuwa changamoto kwa wanawake wengi wenye shughuli nyingi. 

Kufahamu kuhusu kuzitunza nywele zako za asilia kwa kutumia vyakula hatua kwa hatua ikiwemo kutumia muda mfupi kuziandaa, usikose kusoma mwendelezo wa makala haya Agosti 13, 2020. 

Kwa maoni kuhusu mfululizo wa makala haya tuandikie kwa baruapepe maoni@nukta.co.tz au Whatsapp +255 677 088 088. 

Related Post