Rais Samia ataja mafunzo matano kwa viongozi wa sasa kujifunza kwa Hayati Msuya

May 13, 2025 8:08 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na  kupenda maendeleo ya Taifa na kuwa na msimamo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao kwa maslahi ya nchi.
  • Hayati David Msuya anatajwa kama miongozi mwa viongozi waliohudumu katika nyakati ngumu zaidi nchini

Kilimanjaro. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka  Watanzania waliopewa dhamana ya uongozi katika nyadhifa mbalimbali kutumia maisha ya Hayati David Msuya kama funzo la kuboresha utendaji kazi wao ikiwemo kupenda maendeleo ya Taifa na kuwa na msimamo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao kwa maslahi ya nchi.

Rais Samia aliyekuwa akiwahutubia Watanzania katika ibada ya mazishi ya Hayati Msuya aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa kwanza wa Rais  iliyofanyika leo Mei 13, 2025 katika kanisa la Usangi wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro amesema kiongozi huyo ameacha mafunzo yatakayoishi kwenye akili, mioyo na maisha yao.

“Tuwe wapenda maendeleo na kutoacha kusimamia kile tunachokiamini bila kuyumbishwa na chochote, huyo ndio alikuwa mzee Msuya, alifanya kila namna kufanya kile anachikiamini ambacho kitakuwa na manufaa kwa jamii, miradi mingi na mabadiliko alisimamia,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema funzo la pili ni kufanya kazi kwa uzalendo, uaminifu, uadilifu ambapo Hayati Msuya aliamini katika matumizi sahihi ya rasilimali za Taifa kuleta tija kwa wananchi.

Mafunzo mengine ni kutumia ujuzi na wataalamu katika kufanya maamuzi ya maendeleo kwa kuwasikiliza na kutumia ushauri wao kama muongozo na kutokuwa waoga wa mabadiliko, kwa kuyatizama kama hatua ya maendeleo.

Kwa mujibu wa Rais Samia katika kusisitiza hilo Hayati Msuya aliirai timu inayoandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 – 2050 kuhakikisha nchi inakuwa na wataalamu ambao wanaweza kutafsiri mazingira ya nchi pamoja na changamoto zilizopo ili kubuni mipango inayoendana na uhalisia wa nchi kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Aidha, funzo la tano ambalo Rais Samia amewataka viongozi kujifunza kwa Hayati Msuya ni kuwa na uvumilivu katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuhimili changamoto watakazokutana nazo.

Hayati David Msuya anatajwa kama miongozi mwa viongozi waliohudumu katika nyakati ngumu zaidi nchini ikiwemo kuwa Waziri wa Fedha wakati wa mdororo wa uchumi baada ya vita ya Tanzania na Uganda mwaka 1978 pamoja na kipindi cha mageuzi ya kiuchumi yaliyosababishwa na anguko la Umoja wa Kisovieti na vikwazo kutoka taasisi za kifedha za kimataifa.

Pamoja na hayo, Hayati Msuya alimpisha Hayati Edward Sokoine katika kiti cha Uwaziri Mkuu mara baada ya Sokoine kurejea kutoka masomoni ambapo Msuya aliendelea kuwa Waziri wa Fedha mpaka alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa kwanza wa Rais na Hayati Ali Mwinyi, Rais wa awamu ya pili wa Tanzania.

Rais Samia akiweka mchanga kwenye kaburi la hayati Msuya katika mazishi yaliyofanyika kijiji cha Usangi wilayani Mwanga. Picha l Ikulu

Kwa upande wake Rais wa awamu ya nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete amemuelezea Hayati Msuya kama binadamu aliyekuwa na ustahimilivu usiokuwa wa kawaida, uwezo mzuri wa kujenga hoja, mlezi pamoja na mshauri bora ambaye aliutoa hata bila kuombwa.

Kikwete amewataka Watanzania kutumia maisha ya Hayati Msuya kama funzo la kuweka jitihada la kujifunza mambo mbalimbali ambapo licha ya Msuya kutokuwa mtaalamu wa uchumi aliivusha nchi katika vipindi vigumu vya mdororo wa uchumi na kutayarisha mipango iliyochochea mageuzi ya kiuchumi nchini Tanzania.

Hata hivyo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjiri la Kilutheri Tanzania (KKKT) Alex Malasusa amewataka wakazi wa Mwanga pamoja na Watanzania kwa ujumla kuenzi tunu ya umoja na mshikamano iliyojengwa na Hayati Msuya kwa muda mrefu.

“Kwa sababu ya alama, upendo aliouweka kwa watu wawili wa chini, aliwafanya wengi watabasamu, viongozi tuwakumbuke wale ambao Mungu anawaweka chini yetu ili siku tukiondoka tuwe kielelezo chema kwa jamii,” amesema Askofu Malasusa.

Msuya ambaye alizaliwa mwaka 1931 katika Kijiji cha Chomvu, Usangi, wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, alifariki dunia Mei 7 mwaka huu kwa ugonjwa wa moyo wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mzena iliyopo jijini Dar es Salaam.

Hayati Msuya amezikwa leo katika kijiji cha Usangi, Wilaya ya Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo mazishi yake yameongozwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks