Dk. Jafo: wasiofufua viwanda kukutana na mkono wa Serikali
- Ni kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuongeza wigo wa ajira kwa vijana nchini kupitia viwanda.
Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Suleiman Jafo amewataka wote waliopewa viwanda na kushindwa kuviendeleza, kuvifufua viwanda hivyo kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuongeza wigo wa ajira kwa vijana nchini kupitia viwanda.
Dk Jafo aliyekuwa akiwaambia wanahabari mafanikio ya sekta ya viwanda katika kipindi cha miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani amesema Serikali itaingilia kati iwapo viwanda hivyo havitafufuliwa.
“Niwaombe, fufueni hivi viwanda kwa hiari yenu kabla Serikali haijaingiza mkono wake” amesisitiza Dk. Jafo leo Mei 15, 2025 jijini Dodoma.
Dk. Jafo ameeleza kuwa zoezi hilo la litaratibiwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kutambua umiliki na kujua iwapo wahusika wameuziwa viwanda hivyo moja kwa moja.
Hata hivyo, ni kwa muda sasa Serikali imekuwa ikipigia chapuo kufufua upya viwanda hasa vilivyokuwa katika mikoa ya Tanga na Morogoro ikiwemo kiwanda cha nguo cha Morogoro Textile Mills na kiwanda cha nondo cha Morogoro Iron and Steel Company.
Aidha, Agosti 6, 2024 Rais Samia aliyekuwa ziarani mkoani Morogoro alisema Serikali yake itahakikisha mkoa huo unarudi kwenye hadhi ya viwanda kama ilivyokuwa hapo zamani ili kukuza uchumi wa mkoa huo na Tanzania kwa ujumla.
“Tunataka kurudisha hadhi ya Morogoro ya viwanda, na tunaka Morogoro ikashindane na Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam. Tayari Waziri wangu wa viwanda nimeshamuelekeza kuhakikisha viwanda vilivyopo havifi, lakini vile vilivyokufa basi vifufuliwe hata kama havitazalisha yale mazao yaliyokuwa yakizalishwa, lakini viwanda vile vifufuliwe vizalishe mambo mengine viendelee na kazi,” alisema Rais Samia.
Huenda juhudi za kufufua viwanda zikasaidia kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa ambapo Kwa mujibu wa Wizara ya Viwanda na biashara mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa uliongezeka kiduchu mwaka 2024 na kufikia asilimia 7.3 kutoka asilimia 7.0 mwaka 2023.
Wakati huo huo, ukuaji wa sekta ya viwanda ulikuwa asilimia 4.8 mwaka 2024 ikilinganishwa na asilimia 4.3 mwaka 2023
Aidha, mchango wa sekta ya biashara kwenye pato la Taifa kwa mwaka 2024 ulikuwa asilimia 8.6 ikilinganishwa na asilimia 8.4 mwaka 2023 n huku kasi ya ukuaji wa sekta ya biashara nayo ikiongezeka kiduchu na kufikia asilimia 4.8 mwaka 2024 ikilinganishwa na asilimia 4.2 mwaka 2023.
Ukuaji huo unatajwa kuwa huenda umechangiwa na uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara.
Itakumbukwa kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara iliomba Bunge lidhinishe bajeti ya Sh135.79 bilioni kwa mwaka wa fedha 2025/26, ikiwa ni ongezeko la asilimia 22.4 kutoka Sh110.9 bilioni zilizotengwa mwaka wa fedha 2024/25 ili kukuza viwanda na kuongeza thamani ya bidhaa nchini.
Latest



