Tusipowasaidia, Tanzania itawapoteza bodaboda wote

Nuzulack Dausen 0218Hrs   Agosti 29, 2019 Maoni & Uchambuzi
  • Tuwaelimishe na kuwakemea bodaboda pale wanapovunja sheria na kanuni barabarani.
  • Hakuna Mtanzania yeyote anayestahili kufariki kwa ajali za barabarani.
  • Bodaboda hawana haki ya kutumia barabara watakavyo kwa kuwa juu ya sheria. Hakuna. 

Takriban kila wiki huwa nashuhudia angalau ajali mbili au tatu za bodaboda katika safari zangu Jijini Dar es Salaam. Baadhi ya ajali hizo ni mbaya sana na nyingine ni ndogo lakini zenye madhara kwenye vyombo husika vya moto au kwa watumiaji wa barabara.

Miongoni mwa matukio mengi ambayo nimeshuhudia ni bodaboda kugonga magari au watembea kwa miguu. Sehemu kubwa ya ajali hizi hutokea karibu na taa za kuongezea magari au makutano ya barabara.

Mfano, leo (Agosti 29, 2019) nikiwa njiani kuelekea kwenye kibarua changu nimeshuhudia bodaboda akilivaa gari dogo aina ya Toyota IST lililokuwa limesimama likisubiri kuruhusiwa kupita na taa za kuongozea magari maeneo ya Morocco.

Bodaboda huyo ambaye alijibamiza kichwa hadi kofia ngumu aliyokuwa amevaa kupasuka vipande vipande, alikuwa katika mwendo kasi na alikuwa akilazimisha kupita licha ya taa kumzuia kufanya hivyo. Ndiyo maisha ya bodaboda.

Wao hawaoni umuhimu wa sheria na alama za barabarani. Kwao taratibu za usalama ni kwa ajili ya magari na watembea kwa miguu.

Wakati wasamaria wema wakimuonea huruma mwendesha pikipiki huyo, aliyekuwa amelala pembeni kwa maumivu makali baada ya ajali, mmliki wa gari hilo aliyekuwa anafuata taratibu za barabara alikuwa ameshaharibiwa gari lake kiasi cha kioo chake cha nyuma kupasuka. Dhambi aliyekuwa nayo dhidi ya bodaboda huyo ni kufuata kanuni za barabarani. Basi.


Zinazohusiana: 


Kwa takriban mwaka mmoja sasa usafiri wa pikipiki wa magurudumu mawili maarufu kama bodaboda umekuwa ni msaada mkubwa wa usafiri katika maeneo mengi yasiyokuwa na usafiri wa uhakika nchini.

Mbali na kutoa huduma za usafiri, bodaboda zimetoa ajira kwa vijana lukuki. Hakuna mtu anayeweza kupinga mchango huo mkubwa wa vyombo hivyo vya usafiri na madereva wake.

Tatizo kubwa ambalo ni hasi katika huduma hiyo ni uvunjifu mkubwa wa usalama barabarani na hatari inayoendelea kutengenezwa katika maisha ya watu na mali zao.

Licha ya takwimu rasmi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuonyesha kuwa vifo vitokanavyo na ajali vimepungua zaidi ya mara mbili ndani ya miaka sita iliyopita, bado Watanzania walikuwa hawastahili kufariki kwa sababu ya ajali za barabarani iwe kwa bodaboda ama gari.

NBS katika Ripoti ya Takwimu muhimu mwaka 2018 inabainisha kuwa vifo vitokanavyo na ajali vimeshuka kutoka 4,091 mwaka 2013 hadi vifo 1,912 mwaka  2018.

Pamoja na kwamba kuna mwelekeo chanya katika kupunguza vifo hivyo, hoja inabadki pale pale hakuna mtu anayependa kupoteza maisha kirahisi tu barabarani ama kwa kushindwa kuvumilia kusimama kwa sekunde kadhaa barabarani baada ya taa za kuongezea magari kuamuru hivyo au kwa uzembe wa kutotengeneza chombo chake.

Ajali za bodaboda zinahatarisha maisha ya Watanzania na nguvukazi ya Taifa. Usikubali bodaboda anayekuendesha ahatarishe maisha yako. Picha|Fichuo.

Tabia ya kutowakemea bodaboda katika matendo yao itazidi kuwaathiri Watanzania wengi na kwa bahati mbaya baadhi ya matukio ya ajali yanayotokea mitaani huwa hayarekodiwi na polisi kwa kuwa wahusika humalizana kimya kimya. Serikali inaweza kuchelewa kujua kuwa tatizo hili bado ni kubwa kutokana na data nyingine kutorekodiwa.

Ajali hizi zinazidi kugharimu maisha ya wengi. Ajali ya moto uliotokana na gari la mafuta na kugharimu maisha ya watu zaidi ya 100, huenda isingetokea iwapo mwendesha bodaboda asingesababisha ajali kama inavyodaiwa.

Zipo ajali nyingi zinazotokea kwa sababu tu madereva wa magari walikuwa wanahaha kuwakwepa bodaboda wenye tabia ya kujipenyeza kama paka barabarani.

Tunapoteza ndugu zetu wengi waliokuwa wanategemewa na familia zao na hata Taifa kwa ujumla kwa sababu ya kukubaliana na utukutu wa bodaboda. Watu wanaachwa na ulemavu wa kudumu kwa sababu ya kuwafumbia macho boda boda.

Tuwaelimishe na wanaokaidi wapewe adhabu kali kwa kufuata haki. Maboresho ya sheria zinazohusu usalama barabarani yanaweza kufanikisha hili.

Pia, suala ya kuwaelimisha bodaboda kufuata sheria na kanuni za barabarani lisiishie kwa la Jeshi la polisi pekee bali Watanzania wote.

Usikubali kupanda bodaboda bila kofia ngumu. Usikubali bodaboda akatize makutano ya barabara bila uangalifu au wakati taa zimezuia. Usikubali dereva wa bodaboda aendeshe mwendo mkali unaohatarisha maisha yenu kwa mbwembwe. Kumbuka. Tunaishi mara moja tu.

Nuzulack Dausen ni Ofisa Mtendaji Mkuu na Mhariri Mkuu wa kampuni ya Nukta Africa. Kwa maoni muandikie kupitia ndausen@nukta.co.tz au Twitter: @nuzulack. 

Related Post