Mpiga picha aeleza alivyonusurika ajali iliyomhusisha Waziri Kigwangalla

Mwandishi Wetu 0547Hrs   Agosti 04, 2018 Habari
  • Asema urefu na uamuzi wa kubadilishana siti vyamuokoa katika ajali iliyotokea 12.30 asubuhi.
  • Mtu mmoja afariki, watano wanusurika akiwemo Waziri Kigangwalla.
  • Wanasiasa wajitokeza kumuombea Dk Kigwangalla apone haraka.

Dar es Salaam. Mpiga picha, Michael Mlingwa aliyekuwepo katika ajali iliyotokea leo asubuhi (4 Julai 2018) katika Kijiji cha Magugu mkoani Manyara ikimhusisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla amesema urefu wake ulisababisha aombe kubadilishana siti umemnusuru na kifo.

Katika ajali hiyo iliyosababisha kifo cha Mwandishi wa Habari, Hamza Temba, Mlingwa ameeleza katika akaunti yake ya Twitter kuwa alimuomba  marehemu wabadilishane siti kwa sababu ya urefu alionao na kitendo hicho ndicho kilichomkoa katika ajali hiyo.

"Hamza Temba Mungu amekupenda zaidi! Seat uliyokaa ilibidi nikae mie na ukaniomba ukae wewe kwa sababu ya urefu wangu! Rest In Peace Mtu wangu. Mungu akusamehe Dhambi zako!" ameeleza Mlingwa katika ukurasa wa akaunti yake ya Twitter wenye jina la @MxCarter


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Augustino Senga ameiambia Nukta kuwa gari hilo lilikuwa na watu sita wakiongozwa na Dk Kigwangalla, dereva wake anayejulikana kwa jina la Juma Swalehe na marehemu Temba.

Wengine ni Katibu wa Waziri Kigwangalla Ephraim Mwangolema; Mpiga picha, Michael Mlingwa na Mlinzi wa waziri aitwaye Ramadhani Magumba.

Amesema Dk Kigwangalla ameumia kwenye mkono wa kulia, shingo na kifua ambapo majeruhi wengine akiwemo Magumba na Michael walipelekwa katika Kituo cha Afya cha Magugu kupata matibabu ya awali.

Katika jitihada za kuokoa uhai wa majeruhi, Kamanda Senga amesema Waziri Kigwangalla na mlinzi wake Magumba  tayari wamepelekwa katika hospitali ya Mount Meru mkoani Arusha huku jitihada za kumpeleka Mlingwa katika hospitali hiyo zikiendelea ikizingatiwa kuwa amepata majeraha sehemu ya tumbo.

Twiga asababisha ajali

Kamanda huyo ameeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni jitihada za dereva wa gari hilo kumkwepa twiga aliyekuwa anavuka kutoka upande wa kulia kwenda kushoto katikati ya kijiji cha Minjingu na Magugu na kusababisha gari hilo kupinduka na kuacha njia. Eneo hilo ni sehemu ya mapitio ya wanyama.

Gari analotumia Waziri Kigwangalla likionekana baada ya ajali. Picha hii ilitumwa na Mlingwa baada ya ajali hiyo. Picha: @MxCarter/Twitter

Kufuatia ajali hiyo watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa wamejitokeza kumtumia salamu za pole Dk Kigwangalla na kumuombea apone haraka kupitia mitandao ya kijamii.

Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa ajali ni kitu cha kutisha na anamuombea waziri huyo apone haraka.

Mbunge wa Nzega Hussein Bashe ameandika kuwa ajali hiyo ni habari mbaya na amewataka watanzania kumuombea Waziri Kigwangalla na majeruhi wengine ili wapone haraka.

Naye Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji ameandika kuwa mikakati inahitajika katika kuzuia ajali za barabarani kwa sababu ajali sio suala la mwendokasi bali na uwepo wa alama za barabarani.

Ajali hiyo iliyoondoa uhai wa Mwanahabari Temba ni ya pili ndani ya siku nne baada ya mwanahabari mwingine Shadrack Sagati kufariki katika ajali ya gari na wafanyakazi wengine wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wakati wakielekea katika shughuli ya kikazi mkoani Geita. Sagati alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Habari wa wizara hiyo.

Habari zaidi na Daniel Samson


Related Post