Watu zaidi ya 57 wamefariki dunia baada ya lori la mafuta kuwaka moto Morogoro

Mwandishi Wetu 0320Hrs   Agosti 10, 2019 Habari

Baadhi ya mabaki ya pikipiki za bodaboda baada ya roli la mafuta kulipuka eneo la Msamvu mkoani Morogoro. Picha|Mtandao.


  • Watu hao wamepoteza maisha baada ya roli la mafuta kulipuka katika eneo la Msamvu mkoani Morogoro.

Dar es Salaam. Jeshi la polisi mkoani Morogoro limesema watu 57 wamepoteza maisha baada ya roli la mafuta kuwaka moto asubuhi ya leo katika eneo Msamvu, kituo cha redio cha Taifa, TBC Taifa kimetangaza. 

TBC Taifa imesema watu wengine 65 wamejeruhiwa katika ajali hiyo mbaya kuwahi kutokea miaka ya hivi karibuni.

"Hali ni mbaya sana hapa. Watu wengi wamekufa hata wale ambao walikuwa hawajihusishi na wizi wa mafuta wakiwemo wapita njia na wanaofanya biashara eneo hilo," amesema Daniel Ngogo, mmoja wa mashahidi wa ajali hiyo.

Ngogo amesema hata uokoaji umekuwa mgumu kwa sababu moto ulikuwa ni mkubwa na waokoaji walifanikiwa kuwaokoa watu kati ya  65 hadi 70.

"Maafa ya maafa yamekuwa makubwa kwa sababu hii ni sehemu yenye shughuli nyingi na pana kijiwe cha Bodaboda pembeni," amesema.

Msemaji Mkuu wa Serikali Dk Hassan Abbasi amesema taarifa za hivi karibuni ni kwamba watu 60 wamepoteza maisha na miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Dk Abbasi amesema mbali na marehemu hao, watu wengine 70 wamejeruhiwa katika ajali hiyo na wanaendelea na matibabu.

"Serikali mkoani Morogoro na katika ngazi ya Taifa inaendelea kuratibu kuhakikisha miili inahifadhiwa...lakini pia ndugu wanaendelea kutambua marehemu," Dk Abbasi ameiambia TBC Taifa.

Amesema jeshi la polisi limekuwa likitoa elimu juu ya kujiepusha na majanga ya aina hiyo lakini kwa bahati mbaya baadhi wameshindwa kuzingatia.

Naye, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema ajali hiyo ni msiba mkubwa kwa Taifa na ametoa pole kwa wafiwa na majeruhi wote wa jali. 

"Habari za kutisha na kusikitisha sana kutoka Morogoro. Msiba mkubwa sana huu kwa Nchi yetu. Moyo wangu unauma kuona makumi ya Watanzania wakiteketea kwa moto wa mafuta. Maneno hayawezi kueleza uchungu mkubwa niliopata asubuhi ya Leo. Mungu awape subra wafiwa wote," ameandika Zitto katika ukurasa wake wa Twitter. 

Related Post