Wabunge walia ufinyu wa bajeti Wizara ya Maji 2024-25

Sayuni Kisige 0940Hrs   Mei 10, 2024 Afya & Maisha
  • Imepungua kwa asilimia 17 ikilinganishwa na iliyopitishwa katika mwaka wa fedha 2023/24
  • Serikali imesema itatumia vyanzo vya nje kupata fedha kutekeleza miradi ya maji
  • imetenga Sh68 bilioni kwa ajili ya malipo ya wakandarasi

Dar es Salaam. Suala la ufinyu wa bajeti ya Wizara ya Maji limeendea kuibua mijadala bungeni huku baadhi ya wabunge wakidai kuwa linaweza kuathiri utekelezaji wa miradi ya maji na kushindwa kufikisha huduma hiyo kwa  wananchi.

Mei 9,2024 Waziri wa Maji Juma Aweso aliliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Sh627.8 bilioni kwa ajili ya matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25.

“Kati ya fedha hizo Sh69.7 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida huku yakiongezeka kwa asilimia 1.2 sawa na Sh9.2 bilioni” alisema Juma Aweso Bungeni Dodoma.

Bajeti hiyo imepungua kwa asilimia 17 sawa na Sh128.4 bilioni ikilinganishwa Sh756.2 bilioni iliyoidhinishwa mwaka wa fedha 2023/24.

Mara baada ya kuwasilishwa kwa bajeti hiyo wabunge wameibua hoja mbalimbali zilizolenga kupata majibu ya Serikali kuhusu ufinyu wa bajeti hiyo licha ya mahitaji ya maji yaliyopo nchini.

“Mheshimiwa spika nina wasiwasi na ufinyu wa bajeti hiyo, nilitegemea kwamba kwa sababu mahitaji ya maji yanaongezeka kila siku hivyo bajeti ingeongezeka lakini bahati mbaya imepunguzwa,” amehoji Charles Muguta(CCM) Mbunge wa Jimbo la Mwibara.


Soma zaidi:Kimbunga Hidaya chaua watu 10 Kilwa, Ifakara


Naye Mbunge wa Mbinga Vijijini, Benaya Kapinga (CCM) amesema hataunga mkono kupunguzwa kwa bajeti hiyo kutokana na uwepo wa mahitaji makubwa ya maji hususani katika jimbo lake.

“Jambo ambalo sitaliunga mkono ni hili la kupunguziwa bajeti, mheshimiwa spika katika jimbo langu kuna vijiji 40 havina maji mpaka leo na tumekubaliana kufikia mwakani angalau vijiji vifikie asilimia 85 lakini kwa mwendo huu nahofu kwamba halitofikia”,  amesema Kapinga.

Mbali na ufinyu wa bajeti wabunge walilalamikia ucheleweshwaji wa malipo kwa wakandarasi wa miradi ya maji jambo ambalo limechangia kutokukamilika kwa miradi mbalimbali nchini.

Boniventura Kiswaga (CCM) Mbunge wa Magu ameitaka Serikali kuongeza bajeti hiyo ili kuwezesha miradi ambayo fedha zake zimecheleweshwa kuendelea.

“Kuna miradi ambayo imesimama hata mikataba yake imeisha lakini kwa sababu ya kukosa fedha ya kuendesha miradi jimbo la Magu lina mradi wa nyang’anga ambao kwa asilimia 77, magu lugehe 44 miradi hii inahitaji fedha kukamilika” amesema Kiswaga.


Waziri Aweso avunja ukimya

Waziri Aweso aliyekuwa akijibu hoja za wabunge hao amesema wizara yake imejipanga kutumia vyanzo vya nje na kushirikisha wadau wa maendeleo ili kupata fedha zaidi zitakazowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wizara hiyo.

“Chanzo kingine ni kuandika maandiko kuhamasisha na kuongeza mahusiano hivi karibuni tumeanza ziara nje ya nchi kupitia wadau wetu mbalimbali tuliwenda katika Shirika la Fedha Ufaransa (AFD) baada ya kuzungumza na kuonesha maandiko yetu wametuma Euro milioni 70 (Sh195.4 bilioni) kuhakikisha tunakwenda kutekeleza miradi ya maji,” amesema Aweso.

Aidha, amesema tayari mchakato wa kulipa wakandarasi ili kuendeleza baadhi ya miradi ambayo imecheleweshwa kutokanana kukosa fedha.

“Tumekaa na mheshimiwa Waziri wa Fedha… katibu mkuu wangu wa Wizara ya Maji amenieleza tumepatiwa Sh68 bilioni twende tukawalipe wakandarasi wetu ili huko maeneo ya kazi kuweza kuchangamka,” amesema Waziri huyo.

Related Post