Tanzania yazindua kiwanda cha kuunganisha malori, matipa

Esau Ng'umbi 0740Hrs   Mei 09, 2024 Habari
  • Kinaweza kuunganisha magari 45 kwa siku moja.
  • Kutoa zaidi ya ajira 2,000.


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezindua kiwanda cha kuunganisha malori na matipa ikiwa ni muendelezo wa juhudi za Serikali yake kuvutia uwekezaji mkubwa katika sekta ya viwanda inayotegemewa kuchagiza ukuaji wa uchumi nchini. 

Uzinduzi wa kiwanda hicho kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam unazidi kuongeza idadi ya viwanda vya aina hiyo hatua itakayosaidia kuongeza ajira katika jiji hilo la biashara. Kiwanda kingine cha kuunganisha magari kipo Kibaha mkoani Pwani. 

Kiwanda hicho kipya kinachomilikiwa na Kampuni ya Sturn Corporation, kinaunganisha malori na matipa aina HOWO na kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Rehmtullah Habib, tayari kampuni yake imeunganisha malori na matipa 150 tangu kuanza kufanya shughuli zake mwezi Machi 2024, ambayo tayari yameshanunuliwa.

Malori hutumika zaidi katika shughuli za usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi huku matipa yakitumika zaidi katika shughuli za ujenzi wa miundombinu na hivyo kuwa kiungo muhimu katika ukuzaji wa mnyororo wa uchumi.

Habib ameongeza kuwa kwa sasa kiwanda hicho kina uwezo wa kuunganisha magari 45 kwa siku, ikiwemo malori 30, matipa tisa pamoja na matela 6 huku kikiwa kimetoa ajira rasmi 250 na zisizo rasmi 1,800.


Ujenzi wa viwanda kama hicho cha kuunganisha malori unasaidia kuikuza sekta hiyo ambayo imekuwa na ukuaji wa kuasua tofauti na sekta nyingine kama za mawasiliano na teknolojia.

Kwa mujibu wa Waziri wa Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo aliyekuwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kiwanda hicho, sekta ya viwanda imekuwa na mchango chini ya asilimia 10 ya Pato la Taifa (GDP) katika miongo mitatu iliyopita.

Prof Kitila amesema changamoto lukuki ziliikumba sekta hiyo kama ukosefu wa umeme pamoja na miundombinu, kero ambazo zinaendelea  kutatuliwa jambo lililochochea kukua kwa uwekezaji katika miaka ya hivi karibuni.

“Katika miradi 526 iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania kwa mwaka jana pekee, miradi 237 ilikuwa ni ya uzalishaji viwandani… tunaonankwamba katika miaka michache ijayo uchangiaji katika sekta ya uzalishaji viwandani utazidi kuimarika na GDP yetu itachangiwa vizuri,” amebainisha Prof. Mkumbo.

Serikali kujadili kuongeza ushuru magari kutoka nje

Ili kulinda uwekezaji uliofanywa na kiwanda hicho, Habib ameiomba Serikali kuongeza kodi kwa magari yanayoagizwa kutoka nje, jambo ambalo Waziri wa Uwekezaji Dk. Ashatu Kijaji amesema linafanyiwa kazi.

“Tayari tuna kikao na Waziri wa Fedha ili ndugu zetu wanaofanya kazi eneo la sera za Sheria yetu ya Kodi walifanyoe kazi eneo hili kwa kina na waweze kukushauri Mheshimiwa Rais ili tuone namna ya kukilinda kiwanda hiki na viwanda vingine,” amesema Kijaji.

Related Post