Bei ya nyama ya kuku, ng’ombe haishikiki Mwanza

Mariam John 0850Hrs   Aprili 10, 2024 Habari
  • Bei ya kuku mmoja yapanda kutoka Sh10,000 hadi 20,000.
  • Baadhi ya wakazi washindwa kumudu gharama za vitoweo hivyo.

Dar es Salaam. Wakati waumini wa dini ya kiislamu wakisheherekea sikukuu ya Eid al-Fitr, baadhi ya wakazi jijini Mwanza wamelalamikia kupanda kwa bei za bidhaa za chakula ikiwemo nyama ya ng'ombe na kuku.

Wakizungumza na Nukta habari kwa nyakati tofauti wakazi wa jiji hilo wamesema bei ya bidhaa za vyakula imepanda kulinganisha na miezi kadhaa iliyopita hali inayofanya baadhi yao kushindwa kumudu gharama hizo.

"Bei za vitoweo zipo juu, kuku wamepanda sana bei na hii inasababisha na kuzidi kwa mvua hivyo kusababisha wafugaji kushindwa kuzalisha kwa wingi," amesema Ahmed Nchora Mwenyekiti wa Soko Kuu Mwanza.

Mwenyekiti huyo amebainisha kuwa walianza kushuhudia kupanda kwa bei za chakula  miezi mitatu iliyopita na kusababisha baadhi ya bidhaa ikiwemo kuku kupanda bei kutoka Sh10, 000  hadi sasa hivi kuku mmoja huuzwa kwa Sh20,000.


Soma zaidi: Nyama, mayai na maziwa: Virutubisho vinavyohitajika zaidi na mwili wa binadamu


Naye Asha Shaban, mkazi wa jiji hilo anaeleza jinsi alivyoshindwa kununua kuku kutokana na gharama yake kuwa juu kuliko ilivyokuwa miezi michache iliyopita.

"Nilikuja kuangalia kama naweza kupata mboga kwa ajili ya sikukuu lakini nimeshindwa bei ni kubwa ambapo naelezwa kuku mmoja Sh20,000 wakati ni kuku tu wa kawaida," amesema Asha.

Baadhi ya wauzaji wa vitoweo hivyo wamesema kwa sasa kuku hawapatikani kwa wingi na kuwa wanalazimika kununua na kuwauza kwa  bei kubwa iliwaweze kupata faida.

Wakazi hao pia leo wamenunua nyama ya ngombe kwa Sh8,000 kutoka Sh7000 waliyotumia kununua kitoweo hicho wiki kadhaa zilizopita.

Aidha, bidhaa nyingine za chakula kama kitunguu nayo zimepanda bei kutoka Sh2,000 iliyokuwa ikitumika kununua  kwa kilo moja hadi Sh3,000.

Kupanda kwa bei za bidhaa za chakula huzuia baadhi ya wananchi kumudu maandalizi ya chakula ambacho hukamilisha sikukuu au sherehe .Picha|Daudi Mbapani/NuktaAfrica

Mchele, maharage vyashuka bei

Kuhusu bei za vyakula vya nafaka ikiwemo mchele imeshuka bei ambapo kilo moja ya mchele ‘super’ iliyouzwa Sh3,000 sasa unauzwa Sh1,800 hadi Sh2,400.

"Mchele utaendelea kushuka kwa kuwa mwaka huu wakulima wamezalisha Kwa wingi zao hilo  pamoja na maharage ambayo pia yameshuka kutoka Sh3,000 na kufikia sh 2,000," amesema Nchora.

Related Post