Tanzania kuanza utekelezaji wa awali mradi wa gesi asilia Julai

Esau Ng'umbi 0924Hrs   Mei 31, 2023 Habari
  • Ni baada ya kukamilika kwa mazungumzo, mikataba pamoja na sheria ya mradi.
  • Unatarajiwa kubadili taswira ya uchumi wa Tanzania.

Dar es Salaam. Waziri wa Nishati January Makamba amebainisha kuwa Serikali inatarajia kuanza  utekelezaji wa awali wa mradi wa kuchakata na kusindika  gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) ifikapo Julai, 2023 kwa kuwa mikataba na sheria ya mradi huo ipo tayari.

Mradi huo utakaogharimu Dola za Marekani bilioni 42 sawa na zaidi ya Sh90 trilioni za Tanzania unatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi nchini kwa kuwa utaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zinazochangia katika usalama wa nishati duniani.

Makamba aliyekuwa akisoma bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2023/24 leo Mei 31, 2023 amewaambia Wabunge kuwa baada ya kukamilika kwa mazungumzo yaliyokwama kwa miaka saba, mikataba ya mradi huo itawasilishwa Baraza la Mawaziri Juni mwaka huu kwa ajili ya kuidhinishwa.

“Mikataba iliyokubaliwa itawasilishwa kwa Baraza la Mawaziri Mwezi Juni ili kuidhinishwa kabla ya kusainiwa, mradi huu utabadili sura na taswira ya uchumi wa nchi yetu, mikataba ina tija na maslahi kwa Taifa ambapo Kampuni ya Mafuta ya Taifa (TPDC) ni mbia na muwekezaji katika mradi huo,” amesema Makamba jijini Dodoma.

Ili kuhakikisha mradi huo unafuatiliwa, kuratibiwa na kuwezeshwa  kwa ukaribu imeanzishwa ofisi maalumu ya kusimamia na kutungwa kwa Sheria ya Mradi ambayo itawasilishwa bungeni kwa ajili ya kupitiwa na Wabunge.

Gesi asilia ni miongoni mwa rasilimali muhimu hivi sasa duniani kutokana na umuhimu wake ambapo baadhi ya matumizi yake ni kuzalisha nishati pamoja na mbolea.

Mradi huo unatarajiwa kuwa kichocheo cha uchumi kupitia sekta ya nishati hususani wakati huu ambao dunia inakabiliwa na muelekeo mpya katika sekta ya nishati kutokana na mabadiliko ya tabianchi.





Soma zaidi


Taifa la Urusi ni miongoni mwa nchi zinazoingiza fedha nyingi kwa kuuza gesi hiyo katika mataifa ya Umoja wa Ulaya ambapo kabla ya kuanza vita kati yake na Ukraine, taifa hilo lilikuwa linatoa zaidi ya asilimia 35 ya gesi katika nchi za umoja huo.

Kutokana na Tanzania kutokuwa na wataalamu wa masuala ya gesi na mafuta ambao watahudumu katika mradi huo, unaotarajiwa kuanza kazi mwaka 2025, Serikali imepanga kuanzisha chuo cha kufundisha masuala hayo kitakachokuwa na hadhi ya kimataifa mkoani Lindi.

Wananchi watanufaikaje?

Serikali itatoa elimu kwa wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ili waelewe nafasi yao katika mradi huo pamoja na kuanzisha ukanda maalumu wa kiuchumi.

“Ili kupanua fursa na kushamirisha maendeleo ya ajira na viwanda, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi itaanzisha eneo maalumu la kiuchumi katika eneo la mradi ili kuvutia viwanda na shughuli nyingine za uchumi,” amesema Makamba.

Tumefikaje hapa?

Mwaka 2012 aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini (kabla ya kutenganishwa) Profesa Sospeter Muhongo alithibitisha kuwa watafiti wamebaini uwepo wa gesi asilia katika Mkoa wa Lindi zenye ujazo wa futi trilioni tatu.

Hata hivyo, kwa nyakati tofauti utekelezaji wa mikataba ya kuanza kusindika gesi hiyo imekuwa ikipigwa danadana kutokana na Serikali kutofikia muafaka na wawekezaji mpaka walipofanikisha kusaini mkataba wa awali Juni mwaka 2022.

Itakumbukwa mwaka 2019 akiba nyingine ya gesi asilia iligundulika katika maeneo mengine manne ambayo ni Ntoria, Magharibi mwa Songosongo, Mnazi Bay kaskazini pamoja na Ruvu mkoani Pwani.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ugunduzi huo wa mwaka 2019 unaifanya Tanzania kuongeza akiba ya gesi asilia kutoka ujazo wa futi trilioni 57.5 za ujazo wa mraba hadi futi milioni 62.7 za ujazo wa mraba ambazo kama zikitumika vema zinaweza kumaliza kabisa tatizo la umeme nchini.

Related Post