Umemejua ulivyobadilisha maisha ya mwanamke mjasiriamali Lindi

Esau Ng'umbi 1032Hrs   Mei 30, 2023 Habari
  • Ni baada ya kupata mafunzo ya namna ya kutumia umeme jua kwenye shughuli za uchumi.
  • umemuwezesha kujiajiri pamoja na kutoa fursa ya ajira 
  • Gharama ya nishati hiyo pamoja na upatikanaji bado ni kikwazo

Dar es Salaam. “Nishati ya umeme  ni rafiki wa mwanamke, kwa sababu mwanamke ana mambo mengi sana ya kufanya yanayoweza kumuinua kiuchumi na jamii ikaendelea,”

Ni kauli ya Ashura Huruko, mkazi wa kijiji cha Namtumbwa, Kata ya Mbaya, Mkoa wa Lindi akielezea matamanio yake ya kuona nishati ya umeme ikiwafikia wanawake wengi zaidi ili wajikwamue kiuchumi, kutokana na fursa zinazopatikana katika nishati jadidifu. 

Hata hivyo, siyo wanawake wote hasa waishio vijijini wamefikiwa kikamilifu na umeme wa gridi ya Taifa, jambo linalowazuia kujiajiri katika shughuli mbalimbali za uzalishaji zinazotegemea umeme. 

Kwa Watanzania wanaoishi maeneo ya vijijini  matumaini yao ya kupata nishati yanategemea zaidi nishati jadidifu ambayo inatajwa kuwa ni safi, salama, rafiki wa mazingira, ni endelevu na suluhisho la athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame na ongezeko la joto duniani. 

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Biashara (ITA), zaidi ya asilimia 97 ya nishati Tanzania inazalishwa kwa kutegemea gesi, maji na mafuta huku nishati jadidifu ikichangia asilimia mbili tu katika gridi ya Taifa. 

Mpango wa Nishati Vijijini wa mwaka 2022-2030 umebainisha kuwa takribani vijiji 2,865 vya Tanzania havina kabisa nishati ya umeme na haviko kwenye programu za kupata nishati hiyo.

Kutokana na hilo nishati jadidifu ukiwemo umemejua, biogesi, jotoardhi, kingamotaka na umeme wa upepo vinasalia kuwa mkombozi kwa wakazi wa vijijini kupata mwanga, nishati ya kupikia na kuendesha shughuli za uchumi.

Ashura (34) ni ushuhuda tosha kwa wakazi wa Kijiji cha Namtumbwa, ambapo aliamua kutumia fursa ya umemejua unaosambazwa na kampuni ya PowerCorner kijijini hapo kufanya shughuli za kiuchumi ambazo zinamuingizia kipato kinachoendesha maisha, huku akimudu gharama za kumsomesha mwanae elimu ya sekondari.

“Nishati ya umemejua imenibadilishia maisha, baada ya kupata elimu ya namna nishati hiyo inavyotumika nilinunua mashine ya kuuunga vyuma, mashine ya kukaanga bisi pamoja na mashine ya kuranda mbao, ambazo zimegeuka kuwa  chanzo cha kipato changu ninachopata maradufu zaidi ya awali,” anasema Ashura.

Ashura ambaye awali alikuwa akiuza vitafunwa katika mgahawa wake huku akijihusisha na kilimo, alipata mafunzo ya kina kuhusiana na namna nishati ya umemejua  inavyoweza kutumika katika shughuli mbalimbali za uzalishaji.

Mafunzo hayo yalitolewa kwa nyakati tofautina  mashirika yanayojihusisha na nishati jadidifu kijijini kwao likiwemo la Elico Foundation ambalo limekuwa likichangia kuboresha maisha ya watu vijijini kwa kuchagiza matumizi ya teknolojia ya kisasa ya nishati jadidifu. 


Zinazohusiana


Kwa sasa, Ashura aliyepata mafunzo hayo mwaka 2020 anaendesha mradi wa kuunga vyuma ambao ana uhakika wa kujingiizia faida ya zaidi ya Sh130,000 kwa mwezi.

Mwanamke huyo hutumia mashine inayoendeshwa na umemejua kuunga vyuma vinavyotumika katika shughuli za ujenzi kama nondo, madirisha, milango na vyombo vya usafiri.

Mashine hiyo tegemeo kijijini hapokwa kuwa  ina uwezo mkubwa zaidi wa kuchomelea hadi chuma cha nchi nane.

“Mashine yangu ni kubwa kidogo, awali nilikuwa nahudumia vijiji sita vilivyopo kwenye kata yetu kabla watu wengine wawili kuleta huduma hii ingawa hulazimika kuja kwangu kupata baadhi ya huduma kama kutoboa vyuma, kwani mashine zao ni ndogo,” anasema Ashura.

Amefungua milango ya ajira

Licha ya kuwa biashara yake haijaimarika sana na  kuwafikia watu wengi, amekuwa akitoa mafunzo kwa wanawake wenzake kijijini hapo ili wajiajiri na kujikomboa kimaisha kwa kutumia umemejua. 

Pia katika biashara ya kuchomelea vyuma ameajiri kijana mmoja wa kumsaidia kazi na ana mpango wa kuwaajiri wanawake wenzake endapo biashara yake itaimarika siku zijazo. 

Mashine ya kuunga vyuma inayotumia umeme jua inayotumiwa katika maeneo ya vijijini ambayo hayajafikiwa na gridi ya Taifa.PichalPowerconer

Safari yake ya kutumia umemejua

Miaka mitatu iliyopita ndipo alipoanza safari ya kujifunza kuhusiana na nishati jadidifu baada ya kutembelewa na wataalam wa nishati hiyo kijijini kwao ambapo walimchukua mpaka mkoani Dodoma alikojifunza zaidi namna nishati ya umemejua inavyoweza kutumika katika shughuli za uzalishaji.

Mafunzo hayo sio tu yalimbadilishia mtazamo na kutambua fursa za nishati jadidifu bali alifanikiwa kuwashawishi wanawake wenzake kijijini hapo kuunda kikundi cha kuoka mikate ili kujikwamua kiuchumi  baada ya Elico Foundation kuwakopesha mashine ambapo walitakiwa kulipa kidogo kidogo.

Kupitia mashine hiyo iliyokuwa ikitumia umemejua walikuwa na uwezo wa kuzalisha mikate 60 kwa siku na kusambaza kwa wanakijiji.

Kutokana na gharama za uendeshaji kuwa juu, na kusababisha wao kupata faida kidogo hawakuendelea kutumia mashine hiyo. Kwa sasa wanasubiri umeme unaotarajiwa kupelekwa kijijini kwao kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) ili waendelee na mradi huo.

Wakati wakisubiri umeme wa Rea, Ashura hakuacha fursa zimpite. Aliamua kufungua biashara ya kuchomelea vyuma na kulanda mbao za samani kama vile vitanda, viti, au meza, shughuli anazofanya mpaka. 

Pia ana mashine ya kukaanga bisi ambayo huitumia kama kuna mahitaji kijijini hapo hasa wakati wa sherehe hasa zinazohusisha watoto. 

Kibarua kilicho mbele yake

Changamoto kubwa wanayokabiliana nayo watumiaji wa umemejua kibiashara ni  mtambo yao kutokuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa kutosha kuendesha vitu vizito ifikapo majira ya jioni hivyo hulazimika kusitisha uzalishaji.

“Changamoto kubwa ya umeme huu ni ikifika saa 11 jioni huwezi kutumia vitu kama pasi, hita, au mashine nyingine yoyote inayotumia umeme mwingi, waboreshe mitambo yao ifanye kazi muda wote pia wapunguze gharama ziwe au ziendane na umeme wa Tanesco,” anasema Ashura ambaye ni mama wa mtoto mmoja. 

Hatua zinazochukuliwa kuwainua wanawake kwa nishati

Mkurugenzi wa Elico Foundation, Sisty Basil ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa wamekuwa wakiendesha kampeni na elimu ya matumizi ya nishati jadidifu pamoja na fursa zake kiuchumi hususani katika maeneo ya vijijini.

“Tumekuwa tukizungumza na taasisi za kifedha kuwezesha upatikanaji wa mitambo ya umemejua kwa njia ya mkopo wenye masharti nafuu, kwa kiasi kikubwa imesaidia kuongeza matumizi ya nishati jadidifu ambapo kasi ya matumizi imechagizwa na mabadiliko ya tabianchi,” anasema Basil.

Basil anasema Serikali inaweza kushirikiana na wadau wa sekta binafsi  kutengeneza mazingira wezeshi ikiwemo kuondoa au kupunguza kodi kwa baadhi ya mitambo ya umemejua, ili iwafikie wananchi wengi  kwa gharama nafuu.

Wakulima wakioneshwa mashine ya umwagiliaji inayotumia nishati ya umeme jua, katika utekelezaji wa moja ya mradi wa Elico Foundation. PichalElico 

Elico Foundation imekuwa ikiendesha miradi mbalimbali ikiwemo ya umwagiliaji, usambazaji wa umemejua katika vituo vya kutolea huduma za kijamii ikiwemo afya vijijini katika mikoa ya Dodoma, Iringa na Lindi ambako wanufaika wakubwa ni wanawake.

“Kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati tunasambaza nishati ya umemejua katika maeneo ya vijijini ambao wananchi wanautumia katika maeneo tofauti ikiwemo, kupooza vinywaji, uungaji wa vyuma, mashine za kusaga nafaka pamoja na mashine za kurekebisha vipuri vya magari hiyo yote inawasaidia wananchi kujiingizia kipato,” anasema Basil. 

Basil ametoa wito kwa Serikali pamoja na sekta binafsi kufanya uwekezaji katika sekta ya nishati jadidifu kwani Tanzania ina utajiri wa vyanzo vingi vya nishati jadidifu ambayo bado haijatumiwa vyema.

Waziri wa Nishati Januari Makamba alipokuwa akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya nishati yaliyofanyika katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma Mei 30, 2023,  alibainisha kuwa Wizara hiyo inajipanga kutumia makundi mbalimbali kutoa elimu juu ya matumizi ya nishati jadidifu huku wakijiandaa kutoa dira ya nishati ya kupikia mwezi Julai 2023.

Aidha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maonesho hayo ametoa wito kwa Watanzania kugeukia matumizi ya nishati jadidifu huku akiitaka Wizara ya Nishati kuratibu mafunzo na kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya  nishati hiyo ikiwa ni utekelaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Serikali kupitia Wizara ya Nishati pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) kwa maelekezo ya Rais Samia imeunda kamati ya kitaifa inayoratibu utoaji elimu na kuonesha fursa za wajasiriamali ambao watahitaji kuingia kwenye sekta hii ya matumizi ya nishati mbadala," amesema Majaliwa.

Majaliwa ameshauri taasisi za elimu , majeshi, kambi za wakimbizi na kila mahali ambapo panakaliwa na watu zaidi ya mia moja  zipewe kipaumbele katika kupewa elimu na kuanza kutumia nishati jadidifu ili kuepuka kuharibu mazingira.

Iwapo nishati safi na salama itapewa kipaumbele nchini itachangia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchini na kuboresha afya za Watanzania wakiwemo wanawake ambao wamekuwa wahanga wa matumizi ya kuni na mkaa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, inakadiriwa kuwa watu 33,000 hufariki dunia nchini kila mwaka kutokana na magonjwa yatokanayo na matumizi ya kuni na mkaa. 

Tanzania imejiwekea malengo ya kuhakikisha kuwa inafikisha asilimia 80 ya matumizi ya nishati jadidifu ifikapo mwaka 2030.

Related Post