Kimbunga Hidaya chaua watu 10 Kilwa, Ifakara

Sayuni Kisige 0503Hrs   Mei 09, 2024 Afya & Maisha
  • Saba kati ya hao wamefariki dunia katika mji wa Ifakara mkoani Morogoro.
  • Serikali yaendelea na jitihada za uokoaji na kutoa huduma kwa waathirika. 


Dar es salaam. Watu 10 wamefariki dunia kutokana na athari zilizosababishwa na kimbunga Hidaya ikiwemo mvua zilizoambatana na upepo mkali jambo ambalo limeifanya Serikali kuchukua hatua ikiwemo kuwahamisha waathirika kwenye maeneo hatari na kutoa misaada ya chakula.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Kassim ameliambia Bunge leo Mei 9, 2024 jijini Dodoma kuwa watu hao wamefariki dunia katika maeneo ya Ifakara mkoani Morogoro na Kilwa mkoani Lindi. 

Mbali na vifo, Majaliwa amesema kimbunga Hidaya kilileta madhara mengine yakiwemo uharibifu wa miundombinu ya afya, shule, barabara, kusimama kwa shughuli za uchumi, uharibifu wa chakula na madhara ya kisaikolojia.


Soma zaidi:Kimbunga Hidaya chawatesa wavuvi nane baharini Dar es Salaam


Kiongozi huyo alikuwa akiwasilisha taarifa kuhusu kimbunga Hidaya kilichosababisha mvua kubwa na upepo mkali katika mikoa ya Pwani, Lindi, Mtwara na Morogoro na maeneo jirani.

“Katika wilaya ya Kilwa, vijiji 13 kata 11 madhara mbalimbali yametokea yakijumuisha vifo 3 vya watu, huku kaya 178 zenye watu 941 zimezingirwa na maji, shule moja imezingirwa na maji…

…barabara kuu ya Lindi kuelekea Dar es Salaam imekatika katika kipande cha Somanga chenye urefu wa mita 200 kilichosababisha kukwama kwa magari takriban 126 ikiwemo mabasi ya abiria, malori na magari binafsi,” amesema Majaliwa.

Mapema Mei 1, mwaka huu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitangaza uwepo wa kimbunga Hidaya hususan maeneo ya Pwani ya Afrika Mashariki kutokana na mgandamizo mdogo wa hewa katika bahari ya Hindi ambacho kiliendelea kuimarika na kusababisha mvua na upepo mkali hususan maeneo ya pwani na yale ya jirani. 

Majaliwa amesema vifo vingine vya watu saba vilitokea Ifakara ambapo kata 4 za viwanja 60, Mbasa, Kibaoni na Katindiuka, zimeathirika kwa kiasi kikubwa baada ya mafuriko yaliyosababisha Mto Lumemo kujaa na kumwaga maji kwenye makazi ya watu katikati ya mji wa Ifakara.


Waziri huyo ameongeza kuwa, watu takriban 2,534 walikwama, baadhi ya abiria na magari wamerudia njiani kupitia njia ya Lindi mjini, wengine wamesafiri kupitia njia ya Songea kuelekea Dar es Salaam huku  wengine kurudi Dar es Salaam kutokea Somanga.

“Taasisi za umma, binafsi, makazi na wananchi walizingirwa na maji ikiwemo kituo cha Songas watu 31 walizingirwa na maji katika mtambo wa kuchakata gesi,” ameeleza Majaliwa.

Madhara mengine yaliyojitokeza ni kubomoka kwa nyumba takriban 43,512 ambazo  zilizingirwa na maji na kuharibiwa.

“Kwa miundombinu ya barabara zinazounganisha wilaya na wilaya, barabara za vijiji na mitaa, pamoja na miundombinu ya reli ya TAZARA, makalvati katika wilaya ya Ifakara kutopitika kabisa kutoka na kujaa maji,” ameeleza Majaliwa.

Sambamba na hayo imeripotiwa kuwa, mazao mbalimbali yenye jumla ya ekari 23,501 yameathirika yakiwemo mahindi, mpunga, mazao mchanganyiko na mifugo.

Serikali yaendelea na uokoaji

Ili kukabiliana na madhara ya kimbunga hicho, Majaliwa amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau muhimu imechukua hatua za haraka kudhibiti madhara ya kimbunga hicho. 

“Katika mkoa wa Lindi wilaya ya Kilwa ni kuendesha zoezi la utafutaji na uokoaji ambapo jumla ya watu 4,080 wameokolewa katika maeneo mbalimbali, kurejesha hali ya miundombinu ya barabara kuu ya Lindi Dar es Salaam…

…juhudi zinafanyika za urejeshaji wa daraja la Somanga Mtama ili magari yaliyokwama yaweze kuendelea na safari,” amesema.

Katika mji wa Ifakara uliopo wilayani Kilombero,  juhudi zinafanyika ikiwemo kuhamishwa kwa waathirika katika maeneo ambayo ni salama wakati ambao nyumba zao zimebomoka na kuzingirwa na maji na kupatiwa vyakula, vifaa vya malazi na kukarabati miundombinu iliyoharibika.

Related Post