Rais Samia: Tunahitaji mapato ili tupunguze kukopa
- Ataka Kamishna Mpya wa TRA kusimamia ukusanyaji na kuziba mianya ya wizi.
- Amwambia atafanya ufuatiliaji wa karibu kwa kumtumia Kidata.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amemtaka Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Juma Mwenda kusimamia ukusanyaji wa mapato nchini ili kuongeza upatikanaji wa fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo na kupunguza utegemezi wa mikopo.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika hafla ya kuwaapisha viongozi wateule leo Julai 5, 2024 Ikulu ndogo ya Tunguu Zanzibar amebainisha kuwa licha ya juhudi za ukusanyaji kodi zinazoendelea bado kumekuwa na mianya ya wizi wa mapato katika maeneo mbalimbali hivyo jukumu lake la kwanza ni kuiziba mianya hiyo.
“Nakupeleka wewe kijana wa Dar es Salaam mtoto wa mjini uhuni wote uliofanywa na TRA umefanyika na wewe ukiwa mle mle pengine uliparticipate (shiriki)…mipango yote ya kupenyeza unaijua Yusuph, nenda kaizibe, tunachohitaji ni mapato, tunachohitaji ni kupungua kukopa,” amebainisha Rais Samia.
Rais Samia amesema ili kuhakikisha mazingira kodi zinakusanywa Serikali yake imeshaweka mazingira wezeshi ikiwemo kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji.
“Kariakoo pale tatizo ni kodi, ukienda leo wanakwambia hiki kesho hiki, Kariakoo pale kuna mapato kama yatakusanywa vizuri kwa mwaka yanaendesha wizara tatu, lakini hamkusanyi kuingia serikalini huenda mnakusanya kuingia mfukoni nenda kazibe hiyo mianya,” amesisitiza Rais Samia.
Hata hivyo, Rais Samia amesema atafuatilia kwa ukaribu utendaji kazi wa kamishna huyo kwa kumtumia aliyekuwa Kamishna wa TRA Alphayo Kidata ambaye sasa atakuwa Mshauri wa Rais katika masuala ya kodi.
Rais Samia ametumia jukwaa hilo kumuagiza Waziri mpya wa Viwanda na Biashara Selemani Jafo kuendelea kutengeneza mazingira rafiki kwa wafanyabiashara nchini kwa kusikiliza na kutatua kero zao pamoja na kufanya mapitio ya biashara zinazoweza kufanywa na raia wa kigeni nchini Tanzania.
Viongozi waliopishwa leo na Rais Samia ni wale walioteuliwa Julai 2, 2024 akiwemo Selemani Jafo aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara akichukua nafasi ya Dk. Ashatu Kijaji ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
Wengine ni Mhandisi Yahaya Ismail Samamba aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Yusuph Juma Mwenda aliyeteuliwa kuwa Kamishna wa TRA pamoja na Alphayo Kidata aliyeteuliwa kuwa Mshauri wa Rais katika masuala ya kodi.