SanLG waonya hatari ya bodaboda feki zinazoingizwa Tanzania

Lucy Samson 1042Hrs   Machi 25, 2024 Habari
  • Zinaharibika mapema na kusababisha ajali kwa watumiaji.
  • Madereva wa bodaboda wasema ni ngumu kutofautisha kati ya boda boda feki na halisi. 


Dar es Salaam. Watengenezaji wa pikipiki za SanLG wamewatahadharisha watumiaji wa vyombo hivyo vya moto nchini Tanzania juu ya wimbi jipya la pikipiki feki zenye madhara makubwa kwa watumiaji ikiwemo kusababisha ajali.

Kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya pikipiki katika usafiri wa umma maarufu kama boda boda ambao umesaidia kupunguza adha za usafiri mijini na vijijini. 

Hata hivyo, mmoja ya watengenezaji wakubwa wa bodaboda hizo SanLG ameonya kuwa kuna baadhi ya watu wamenunua bidhaa zenye nembo zao kutoka China ambazo ni bandia. 

Bahari Leo, Mkurugenzi Mkaazi wa kampuni ya SanLG World Wide amewaambia wanahabari jijini Dar es Salaam leo Machi 25, 2024 kuwa kumekuwa na wimbi la ongezeko la bodaboda feki tangu mwaka 2019 hususani za kampuni ya SanLG.

“Kuna usafirishaji mkubwa wa bodaboda feki za SanLG kutoka China kuja Tanzania tangu mwaka 2019, watengenezaji wa boda boda hizo wanatumia logo sawa na hizi boda boda halisi (Original),” amesema Leo.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, watengenezaji wa bidha hizo huzisambaza kupitia mawakala katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania jambo lilalowakosesha mapato na kuathiri watumiaji.


Soma zaidi:Ajali za barabarani zaongezeka kiduchu, vifo vyafikia asilimia 63


Matumizi ya bodaboda feki huathiri watumiaji na kuweza kusababisha chombo kuwaka moto au kupata ajali kutokana na kutengenezwa bila kufuata viwango mahususi vilivyowekwa na mzalishaji husika kwa mujibu wa Kampuni ya Route Media Consultancy inayofanya kazi na SanLG. 

Anisa Nkulo, Mkurugenzi wa Masoko kutoka Kampuni ya Route Media Consultancy amesema kuna baadhi ya watu wanaotumia bodaboda feki hujikuta wanaanguka anguka na kupata ajali tu bila kujua kwa kuwa vyombo wanavyotumia ni feki na havijakidhi taratibu za kiufundi. 

Anisa amebainisha kuwa bodaboda feki zimeshamiri zaidi katika maeneo mengine ya pembezoni mwa miji na mikoani ambapo wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha.

Ili kukabiliana na wimbi la vyombo hivyo feki, amewataka wananchi kutoa ushirikiano wa kuripoti uingizwaji wa bodaboda feki ambapo atakayefanikisha kuripoti matukio hayo atapewa Sh200,000 huku wasambaji wakichukuliwa hatua mbalimbali ikiwemo kufikishwa mahakamani. 

Bodaboda feki za SanLg hazina logo ya chapa tatu (3D) na neno SanLG kwenye tairi ya mbele ya pikipiki.Picha|SanLG.

Ajali za barabarani zinazosababishwa na bodaboda ni moja masuala yaliyoibua mjadala wa kitaifa juu ya namna ya kulinda watumiaji wa vyombo hivyo ambao baadhi hupoteza maisha. 

Ripoti  ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU)  kati ya Januari na Novemba 2023 inaonesha kuongezeka kwa ajali za barabarani  kwa asilimia 0.1 huku vifo vikifikia asilimia 63.

Licha ya watengenezaji kuonya uwepo wa bodaboda feki mtaani baadhi ya watumiaji wamesema hawana elimu wa kubaini vyombo vya moto na halisi jambo linalofanya waendelee kununua kama kawaida. 

Ni ngumu kutofautisha bodaboda feki 

Mmoja wa waendesha bodaboda kati ya Mwananyamala na Posta jijini Dar es Salaam ambaye hakupenda jina lake kufahamika ameiambia Nukta Habari kuwa madereva wengi hupata shida kutofautisha kati ya feki na halisi.

“Kwa hapa mjini unaweza kukuta hata asilimia 80 zote zikawa ni bodaboda feki ila kwa haraka mtu hawezi kujua kwa sababu majina ya kampuni yanafanana ila muundo wa bodaboda ndio tofauti,” anasema dereva huyo.

Related Post