Ajali za barabarani zaongezeka kiduchu, vifo vyafikia asilimia 63

Mwandishi Wetu 0751Hrs   Februari 21, 2024 Habari
  • Ajali zaongezeka kwa asilimia 0.1.
  • Zaidi ya nusu ya wanaopata ajali za barabarani hupoteza maisha.
  • Kamati ya NUU yatoa wito kwa wanajamii Serikali kukabiliana na ajali hizo.

Dar es Salaam. Wakati jitihada mbalimbali zikiendelea kukomesha ajali za barabarani, ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) inaonyesha kuongezeka kwa ajali hizo kwa asilimia 0.1 huku vifo vikifikia asilimia 63.

Katika mwezi Januari hadi Novemba mwaka 2023 jumla ya ajali 1,595 zilirekodiwa ikiwa ni ongezeko la ajali moja tu kulinganisha na ajali 1,594 zilizoripotiwa mwaka 2022.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Vita Kawawa aliyekuwa anawasilisha ripoti hiyo Februari 9, 2024 Bungeni jijini Dodoma amebainisha kuwa vifo vitokanavyo na ajali hizo vimeongezeka kwa asilimia tano ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

“Matukio ya ajali yaliyosababisha vifo katika kipindi hicho ni 1,020 ikilinganishwa na matukio 972 yaliyoripotiwa kipindi kama hicho mwaka 2022,” amesema Kawawa.  


Soma zaidi:Makosa dhidi ya binadamu yaongezeka kwa asilimia 26 Tanzania


Takwimu hizo ni sawa na kusema zaidi ya nusu ya matukio ya ajali za barabarani (asilimia 63) hupelekea vifo huku zaidi ya robo tatu (36) ya ajali hizo zikipelekea majeraha ya kudumu au ya muda mfupi.

Huenda kupungua kwa matukio ya ajali za barabarani ni matokeo ya uhamasishaji wa viongozi mbalimbali ikiwemo Rais Samia aliyemuagiza Inspekta Jenerali  wa Polisi (IGP) Camillus Wambura kushughulikia tatizo hilo.

Rais Samia alitoa maagizo hayo Julai, 2022 baada ya kuripotiwa kwa ajali za barabarani 3000 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Sababu za ajali za barabarani zatajwa

Kawawa aliwaambia wabunge kuwa uchambuzi uliofanywa na kamati yake umebaini sababu mbalimbali zinazopelekea ajali za barabarani ikiwemo  uhaba wa vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi  kama vile magari ya doria katika barabara kuu, taa za kuongoza magari, matumizi madogo ya teknolojia  na upungufu wa vipima mwendo (speed radar touch).

Mbali na uhaba huo wa vitendea kazi kamati imebaini sababu nyingine ambazo ni ukosefu wa maadili, kuingiliwa kwa utekelezaji wa Sheria za Usalama Barabarani pamoja na mitazamo ya kibinadamu inayoaminisha watumiaji wa vyombo vya moto na barabara kuwa ajali hizo hazizuiliki.

Kutokana na ripoti hiyo, kamati imetoa wito kwa  wanajamii pamoja na Serikalii kuchukua hatua zaidi katika kupunguza ajali za barabarani.

Related Post