Rais Samia awafunda wakuu wa mikoa, awataka kusimamia haki, kupunguza migogoro ya ardhi

Lucy Samson 0534Hrs   Machi 13, 2024 Habari
  • Asema wakuu wa mikoa ni maraisi katika maeneo wanayoyaongoza.
  • Awataka kushughulikia malalamiko ya wananchi pamoja na kuongeza ukusanyaji mapato.


Dar es Salaam.Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wakuu wa mikoa nchini kutatua changamoto za wananchi, ikiwemo migogoro ya ardhi pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato yatakayochangia pato la Taifa na upatikanaji wa huduma za kijamii.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika hafla ya kuwaapisha wakuu wa mikoa wapya leo Machi 13, 2024 jijini Dar es Salaam amesema wakuu wa mikoa ndio watatuzi wakubwa wa matatizo yanayowakumba wananchi katika maeneo waliyopewa kuongoza.

“Nataka niwakumbushe ninyi ndio maraisi wa maeneo yale, shida yoyote ya maeneo yale ni shida yako…kuna Maras (Makatibu Tawala wa mikoa) na Madas ( Makatibu Tawala wa Wilaya ) hao wote wamewekwa wakusaidieni, mpaka apite Makonda watu walie? Hivyo sivyo,”amesema Rais Samia.

Maagizo ya kiongozi huyo yamekuja wakati ambapo kuna malalamiko mbalimbali ya wananchi ikiwemo migogoro ya ardhi, ubovu wa miundombinu, na huduma za kijamii kutoka kwa wananchi.

Kutokana na kutosikilizwa na viongozi wao kwa ngazi za wilaya na mikoa siku za hivi karibuni wananchi hao wamekuwa wakiwasilisha malalamiko yao kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Paul Makonda kupitia ziara zake anazofanya katika mikoa mbalimbali.


Soma zaidi:Rais Samia afanya tena mabadiliko ya mkuu wa mkoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri


Rais Samia amewaambia wakuu wa mikoa kuwa kutowasikiliza wananchi kunawafanya baadhi yao kukosa imani na Serikali iliyopo madarakani jambo linaloweza kuathiri uchaguzi wa Serikali za mitaa unaofanyika mwaka huu na uchaguzi mkuu mwaka 2025.

“Wasiposikilizwa zile ndizo kura zetu, akipita mwingine akiwaambia mie nikiingia nitawasikiliza watampa kwa sababu sisi tumewapuuza hatuwasilikizi, kule ndipo ulipo ushindi wa chama kilichowawekeni madarakani…niwasisitize sanaa kuwasiliza wananchi,” amesema Rais Samia.

Mbali na maagizo hayo Rais Samia amesisitiza suala la ukusanyaji wa mapato ambalo kwa baadhi ya halmashauri bado lipo nyuma licha ya kupokea fedha nyingi za maendeleo.

Aidha, amewataka viongozi hao wateule wa mikoa walioapa leo na wale ambao wapo madarakani kusimamia lishe kwa kuzalisha mazao ya kutosha ya chakula, usimamizi wa fedha pamoja na kupuguza migogoro isiyo ya lazima baina yao na viongozi wengine.

Viongozi mbalimbali (Wakuu wa Mikoa na Naibu Katibu Mkuu (Muungano na Mazingira), Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi yaendayo Haraka (UDART) wakila kiapo cha maadili kwa viongozi wa umma.picha|Ikulu Mawasiliano.

Tutawachukulia hatua wanaofanya kazi kimazoea

Awali Mohamed Mchengerwa, Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa amewarai viongozi wateule kufanya kazi kwa bidii kwa kushirikiana na viongozi wengine na kusema watakaokiuka watachukuliwa hatua.

“Hatuta sita kuchukua hatua kali dhidi ya watendaji ambao utendaji wao ni wakimazoea lakini  wanakwamisha utendaji kazi wa shughuli mbalimbali,” amesema Mchengerwa.

Mchengerwa amebainisha kuwa wizara yake tayari imewachulia hatua baadhi ya watendaji wa Serikali ambao walibainika kufanya ubadhilifu miaka iliyopita na wameshafikishwa mahakamani.

Related Post