Rais Samia afanya tena mabadiliko ya mkuu wa mkoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri

Mwandishi Wetu 0101Hrs   Machi 12, 2024 Habari
  • Amemteua Mkuu mpya wa Mkoa wa Shinyanga, Wakuu wa Wilaya wawili na Wakurugenzi watatu wa halmashauri.
  • Wateule hao wataapishwa Machi 13, 2024.


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ameendelea kufanya panga pangua ya viongozi katika ngazi ya mkoa, wilaya na halmashauri mara baada ya kumteua Mkuu mpya wa Mkoa wa Shinyanga, Wakuu wa Wilaya wawili na Wakurugenzi watatu wa halmashauri.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya mawasiliano ikulu usiku wa kuamkia leo Februari 12. 2024 imebainisha kuwa Rais Samia amemteua Anamringi Macha kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambapo awali alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Macha amechukua nafasi ya Christina Mndeme ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira.

Mabadiliko haya yanakuja ikiwa zimepita siku tatu tu tangu Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dk. Moses Kusiluka atangaze mabadiliko madogo yaliyofanywa na Rais ikiwa ni sehemu ya kuboresha utendaji Serikalini ambapo pamoja na mambo mengine Rais Samia aliteua Wakuu wapya wa Mikoa na kubadili Mkurugenzi wa Mabasi yaendayo haraka Udart.


Soma zaidi:Daladala zagoma Mwanza, wananchi wahaha kusaka usafiri


Wakuu wa wilaya na wakurugenzi wapya

Wengine walioteuliwa ni na Rais Samia ni Japahari Kubecha Mghamba kuwa Mkuu wa Wilaya ya Lushoto ambapo kabla alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Busega.

Mussa Kilakala ameteuliwa kuwa  Mkuu wa Wilaya ya Pangan ambapo Kabla ya uteuzi huo alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Kaliua.

“Amemteua Robert Masunya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na Kabla ya uteuzi huu Bw. Masunya alikuwa Afisa Mwandamizi katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,” inaeleza taarifa ya Ikulu.

Aidha, Mwashabani Mrope ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe na Jacob Simon Nkwera ameteuliwa kuwa  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba. 

Sangai Mambai ameteuliwa kuwa  Katibu Tawala wa Wilaya ya Busega na  Raymond Mweli kuwa Katibu tawala wa Wilaya ya Kaliua.

Mbali na teuzi hizo wapo waliobadilishiwa vituo vya kazi akiwemo Frederick Dagamiko kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Tanga.

Wengine ni Bashir Muhoja aliyehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea na Tito Mganwa kutoka Halmashauri ya Mji wa Korogwe kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.

Licha ya kuwa taarifa ya ikulu iliyotolewa leo haijaweka wazi sababu ya mabadiliko hayo, huenda ikawa ni maandalizi ya  uchaguzi wa Serikali za mitaa unaofanyika mwaka huu 2024 na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani 2025.

Taarifa  ya Ikulu inabainisha kuwa Wakuu wa Mikoa na Naibu Katibu Mkuu wataapishwa asubuh8 ya Machi 13, 2024 Ikulu jijini Dar es Salaam.

Related Post