Rais Samia ateua, atengua na kuhamisha viongozi wa mikoa, wilaya, halmashauri
- Wakuu wa wilaya sita na wakurugenzi 15 wahamishwa vituo.
- Ateua katibu tawala wa mkoa, wilaya na mkuu mpya wa wilaya akitengua mmoja.
- Uteuzi na uhamisho huo umeanza tangu Disemba 12, 2023.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ametengua, kuteua na kuhamisha viongozi wa ngazi mbalimbali za mikoa, wilaya pamoja na halmashauri nchini.
Huenda hatua hiyo ikawa ni miongoni mwa maandalizi ya uchaguzi wa wenyeviti wa Serikali za mitaa mwakani 2024, kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 2025 ambapo Septemba 1, 2023 Rais Samia alimuagiza Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( Tamisemi ) Mohammed Mchengerwa kusimamia suala hilo mara baada ya kumuapisha.
Taarifa iliyotolewa na Zuhura Yunus Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu leo Disemba 14, 2023 imebainisha kuwa, miongoni mwa walioteuliwa ni pamoja na Maryam Ahmed Muhaji anayekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara akichukua nafasi ya Karoline Albert Mthapula atayepangiwa kazi nyingine.
“Amemteua Zuhura Abdulrahman Rashid kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Ruangwa. Rashid ni Afisa Mwandamizi katika Mfuko wa Taifa wa Maji. Anachukua nafasi ya Shamim Sadiq ambaye atapangiwa kazi nyingine,” amebainisha Yunus.
Aidha, Rais Samia amemteua Michael Kachoma kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega akichukua nafasi ya Veronica Vicent Sayore ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Soma zaidi : Wizara ya Afya : Kuna ongezeko la visa Uviko-19, mafua Tanzania
Wakuu wa wilaya sita wahamishwa
Pamoja na uteuzi na utenguzi huo, Rais Samia amewahamisha vituo wakuu wa wilaya sita nchini Tanzania akiwemo Mayeka Simon Mayeka aliyehamishwa kutoka Wilaya ya Chunya kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa huku Remidius Mwema Emmanuel akihamishwa kutoka Wilaya ya Kongwa kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kiteto.
“Mhe. Mbaraka Alhaji Batenga amehamishwa kutoka Wilaya ya Kiteto kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhe. Kanali Hamis Mayamba Maiga amehamishwa kutoka Wilaya ya Rombo kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Misenyi,” amebainjsha Yunus katika taarifa yake.
Wakuu wa wilaya wengine waliohamishwa ni pamoja na Kanali Wilson Christian Sakullo kutoka Wilaya ya Misenyi kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro na Raymond Stephen Mwangwala kutoka Wilaya ya Ngorongoro kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rombo.
Rais Samia ameendelea kupanga na kupangua safu za uongozi katika ngazi ya mikoa na wilaya nchini huku baadhi ya watu wakihusianisha na maandalizi ya uchaguzi mkuu 2025. PichalIkulu
Panga pangua wakurugenzi watendaji wa halmashauri
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyotoka usiku wa kuamkia leo Disemba 14, 2023 Rais Samia amewahamisha wakurugenzi watendaji wa halmashauri 15 nchini Tanzania akiwemo Rose Robert Manumba kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi.
Soma zaidi : 25 wajeruhiwa, mmoja afariki gari ikitumbukia mtoni Mwanza
Aidha, Rehema Said Bwasi amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu huku Yefred Edson Myenzi akihamishwa kutoka Halmashauri ya Mji wa Mbulu kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Geita.
“Bi Zahara Muhiddin Michuzi amehamishwa kutoka Halmashauri ya Mji wa Geita kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara. Bi. Lena Martin Nkya amehamishwa kutoka Halmashauri ya Mji wa Ifakara kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma…
…Bw. Chiriku Hamis Chilumba amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma,” amesema Yunus.
Soma zaidi : Kutana na Timotheo Kaombwe mfungwa aliyegeuza gereza kuwa darasa la ujuzi
Wengine waliohamishwa ni Kisena Magena Mabuba kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Simon Sales Berege kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji.
Michael John Gwimile amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa huku Regina Lazaro Bieda akihamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Momba kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.
“Bi. Mwajuma Abasy Nasombe amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi…
…Bw. Rashid Karim Gembe amehamishwa kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga,” amebainisha Yunus.
Sambamba na hao Zahara Abdul Msangi amehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Philemon Mwita Magesa kutoka Halmashauri ya Mji wa Tunduma kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo.
Aliyetamatisha orodha hiyo ni Butamo Nuru Ndalahwa aliyehamishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba ambapo uteuzi na uhamisho huo ukianza tangu Disemba 12, 2023.