25 wajeruhiwa, mmoja afariki gari ikitumbukia mtoni Mwanza

December 13, 2023 4:14 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Mmoja bado haonekani, juhudi za kumtafuta zinaendelea.
  • Majeruhi wanne waruhusiwa, 21 wanaendelea na matibabu. 

Mwanza. Watu 25 wamejeruhiwa huku mmoja akithibitika kufariki kufuatia ajali iliyotokea leo Disemba 13, 2023 katika Kijiji cha Busalanga baada ya basi dogo la abiria kampuni ya Batco, lililokuwa linatokea Bariadi kuelekea Mwanza kuacha njia na kutumbukia ndani ya Mto Simiyu.

Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Magu Dk Eusebius Chanjali majeruhi wanne kati ya waliopokelewa kutokana na ajali hiyo wameruhusiwa na wengine 21 wanaendelea na uangalizi wa kitabibu.

Baadhi ya mashuhuda  wa ajali hiyo wameiambia Nukta Habari kuwa walisikia kishindo cha gari na baada ya kufika walikuta gari linaseleleka kuingia ndani ya mto.


Soma zaidi : Kutana na Timotheo Kaombwe mfungwa aliyegeuza gereza kuwa darasa la ujuzi


Wilson Makoye anayefanya shughuli zake za kilimo kando ya mto ameambia Nukta Habari kuwa baada ya gari hilo kuzama waliwahi na wenzao na kuanza kufanya kazi ya uokoaji.

“Nilipofika pale nilifanikiwa kutoa watu saba na mwanaume mmoja ambaye tayari alikuwa ameshafairiki dunia,” amesema Makoye 

Mmoja haonekani

Pamoja na kuwa ni mtu mmoja pekee aliyethibitika kupoteza maisha hadi sasa, kuna hofu ya kutokea kwa kifo cha pili kwa kuwa mpaka sasa mtu mmoja ambaye ni mtoto wa mwaka mmoja hajulikani alipo.

Mkuu wa Zimamoto na Uokoaji Wilaya Magu Mkaguzi Msaidizi wa Zimamoto Gaston Tigulebwa amebainisha kuwa shughuli za kutafuta mwili wa mtoto huyo anayedhaniwa kupotea zinaendelea.


Soma zaidi : Punda wanavyorahisisha maisha ya wakazi Iziwa, Mbeya


Tibulegwa ametaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni usukani wa gari la hilo kukatika na dereva kushindwa kuiongoza hali iliyopelekea gari kurudi kwa nyuma na kudumbukia katika Mto.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mtafungwa amesema ajali hiyo imesababishwa na uzembe wa dereva ambao wanaendelea kutafutwa kwa mahojiano na kisha kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Enable Notifications OK No thanks