Kutana na Timotheo Kaombwe mfungwa aliyegeuza gereza kuwa darasa la ujuzi
- Alitumia muda wa miaka 21 gerezani kujifunza kilimo, uashi, na ufumaji.
- Sasa anaendesha maisha kwa kutumia ujuzi aliojifunza gerezani.
- Airai Serikali, jamii kuwatizama wafungwa kwa jicho la tatu.
Mwanza. Wakati baadhi ya watu wakiamini gereza ni sehemu ya mateso, adhabu na shuruba,Timotheo Kaombwe (41) yeye anaamini tofauti, kwake gerezani ni sehemu ya kujikusanyia ujuzi na maarifa uliobadili maisha yake.
Kwaombwe mkazi wa jijini Mwanza, ametumia zaidi ya miongo miwili akiwa gerezani mara baada ya kushtakiwa kwa kosa la ung’anganyi wa kutumia silaha.
Disemba 9, 2022 wakati mamilioni ya Watanzania wakisheherekea maadhimisho ya uhuru wa Taifa lao, Kaombwe alikuwa akisheherekea uhuru wa maisha yake baada ya kupata msamaha wa Rais.
Ikiwa ni mwaka mmoja tangu atoke gerezani kwa msamaha wa Rais uliofupisha kifungo chake cha miaka 30 kuwa cha miaka 21, tayari Kaombwe anamiliki nyumba aliyoijenga mwenyewe na shamba ambalo humuwezesha kujipatia fedha zinazoendesha maisha ya familia yake.
“Ni kweli gereza ni utumwa lakini pia ni shule au chuo ambacho unaweza kujifunza na kupata utaalam wa mambo mbalimbali ambayo unaweza kuja kuyatumia huko mbeleni,” amesema Kaombwe
Timotheo Kaombwe akiwa shambani kwake anakolima kilimo mseto jijini Mwanza.PichalMariam John/Nukta
Ilikuwaje akawa mfungwa?
Akiwa na miaka 20 tu tayari Kaombwe alioa na kuanza kujishughulisha na biashara ya kuuza duka ambayo kwa wakati huo ilijulikana kwa jina maarufu la kioski lililosheheni mahitaji mbalimbali ya nyumbani.
Tuhuma za kuuza bidhaa kwa magendo zilimfanya ahukumiwe kifungo cha mwaka mmoja gerezani ambapo baadae hukumu ilibadilishwa na kuwa unyang’anyi wa kutumia silaha, kesi iliyobadili kifungo na kuwa cha miaka 30 kutoka mwaka mmoja.
” Nilipewa miaka 30 ya kutumikia kifungo changu, sikuwa na namna kwakuwa kesi kama hizo mara nyingi hazina dhamana na kifungo chake si chepesi,” amesema Kaombwe.
Soma zaidi: Punda wanavyorahisisha maisha ya wakazi Iziwa, Mbeya
Fursa mpya gerezani
Tofauti na ilivyo kwa baadhi ya wafungwa ambao hudhani gereza ni adhabu na mateso,Kaombwe aliamua kutumia muda mwingi kujifunza vitu vipya ambavyo aliamini vinaweza kumsaidia kwa siku za usoni.
Alianza kutumikia adhabu yake mpya kwa miaka sita akiwa katika Gereza la Uyui mkoani Tabora, baadae akahamishiwa Gereza kuu la Butimba Mwanza baada ya kubainika kuwa na bidii ya kufanya kazi kwa weledi.
Hata baada ya kufika huko aliendelea kujifunza vitu vingine kama kufyatua matofali, ujenzi wa nyumba, na kilimo mseto ambacho alikipenda zaidi akiamini kingemuingiza faida nyingi baadae.
“Tunaposema kilimo mseto ni kile kilimo cha kuchanganya mazao kama mahindi, maharage, au kunde, mboga mboga na miti ya matunda, kilimo hiki kikilimwa kwa kufuata kanuni kinaingiza pesa nyingi kwa wakati mmoja,” amesema Timotheo.
Maumivu, furaha mwaka mmoja nje ya gereza
Tofauti na matarajio yake Timotheo alipoachiwa huru kwa msamaha wa Rais mwaka 2022 alimkuta mke wake tayatri ana watoto watatu aliozaa na mwanaume mwingine baada ya yeye kukaa muda mrefu gerezani.
Pamoja na kuumizwa na jambo hilo hakuwa na budi kumsamehe mkewe ikiwa ni miongoni mwa mambo aliyojifunza gerezani.
” Kwa binadamu ni vigumu kusamehe, lakini mimi nilisamehe hasa baada ya kuwa huko gerezani tulifundishwa mambo mengi yakiwemo masuala ya kiroho, na ukizingatia kwamba huyu naye ni binadamu asingeweza kuvumilia kwa miaka yote 20 bila tendo, nililipokea na kuamua kusonga mbele,” amesema Kaombwe.
Mara baada ya kurudiana na mkewe, shemejiye alimpa kipande cha ardhi ambacho ndicho anachofanyia shughuli za kilimo zinazomuingizia kipato kinachotosha kuendesha familia yake ya watu wanne huku akiendelea na ujenzi wa nyumba ya vyumba vitatu, muashi akiwa yeye mwenyewe.
Soma zaidi : Mila, desturi zilizopitwa wakati, sababu ongezeko la VVU Mwanza
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza Justine Kaziulaya akizungumza na mwanahabari wa Nukta Habari.PichalMariam John
Serikali, jamii iwatazame wafungwa kwa jicho la tatu
Kaombwe ameiomba Serikali, kuwapatia angalau mitaji ya biashara wafungwa waliohukumiwa vifungo virefu gerezani pale wanapoachiwa huru ili angalau wawe na kitu cha kuanzia wanapoenda mitaani kuliko hivi sasa ambapo mfungwa hupewa nauli pekee.
Kwa mujibu wa Kaombwe, hiyo ni miongoni mwa sababu inayochochea wafungwa wengi wanaoachiwa huru kwa msamaha wa Rais kufanya tena vitendo vya kihalifu mara tu wanapofika uraiani.
“Kwasababu hakuna rasimali inayomfanya ajiendeleza ili apate pa kuanzia, mali ulizoziacha nyumbani utakuta zimeshatumiwa na ndugu zote ukifika ni kuanza sufuri kitu ambacho wengi wanashindwa na kujikuta anafanya uhalifu mwingine,” amesema Kaombwe.
Aidha, kutokana na jamii bado kuwa na mtizamo hasi kuhusu wafungwa, Kaombwe anarai kuwa ni wakati sasa wa wanajamii kuwatizama wafungwa kama binadamu wengine na kuwaruhusu kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kijamii na kimaendeleo ikiwemo kushiriki kwenye shughuli za siasa.
Rai hiyo inaungwa mkono na Abeid Omar Mkazi wa Mtaa wa Darajani anapoishi Kaombwe, akibainisha kuwa amekuwa mfano hasa kutokana na anavyojibiidiisha kutafuta kipato kwa shughuli halali.
“Wapo baadhi ya wafungwa hutoka gerezani na wanapofika mtaani, wanakuwa na mawazo na wengine hukosa cha kufanya lakini kwa Timotheo toka atoke gerezani hajawahi kuchoka anapambana kutimiza ndoto zake,” amesema Omar.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza Justine Kaziulaya, gerezani ni sehemu ya kujifunza ujuzi wa aina tofauti ambapo mfungwa atakapokuwa huru anaweza kuutumia ujuzi huo kujiingizia kipato.
Kaziulaya amebainisha kuwa mbali na kilimo pamoja na ujenzi, gerezani unaweza pia kusoma ufumaji wa mikoba na utengenezaji wa viatu na kozi nyingine za shahada na stashahada.
“Gerezani pia tuna chuo ambacho kipo Mbeya ambapo mhitimu anayehitimu mafunzo anatunukiwa cheti aidha ya shahada au stashahada kulingana na kozi aliyojifunza ili pale kifungo chake kinapoisha anakitumia kutafuta kazi,” amesema Kaziulaya.
Hata hivyo, kiongozi huyo ametoa wito kwa Serikali na jamii kuwasaidia wafungwa kupanga mipango bora itakayowasaidia kwa ajili ya maisha ya baadae.