Daladala zagoma Mwanza, wananchi wahaha kusaka usafiri

Mariam John 1052Hrs   Machi 11, 2024 Habari
  • Miongoni mwa mambo yanayolalamikiwa na madereva hao ni pamoja na utitiri wa faini na kuingiliwa rutii na bajaji.
  • Mkuu wa Wilaya aagiza kusitishwa kwa mgomo.

Mwanza.Daladala zinazofanya kazi katika jiji la Mwanza na maeneo jirani zimeanzisha mgomo wa kusafirisha abiria kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo faini za mara kwa mara kutoka kwa askari wa usalama barabarani.

Wakizungumza na Nukta habari leo Machi 11, 2024 baadhi ya madereva wamesema wamechukua uamuzi huo baada ya malalamiko yao kutosikilzwa licha ya kuyafikisha kwa uongozi.

Miongoni mwa mambo yanayolalamikiwa na madereva hao wa daladala mkoani Mwanza ni pamoja na kupigwa faini za mara kwa mara kutoka kwa askari wa usalama barabarani na bajaji kuingilia ruti za daladala hali inayopelekea kukosa abiria.

“Bajaji zinasumbua mno, kama zina uhalali wa kufanya kazi wazipe njia pia kingine suala la faini unakuta gari ina faini ya kosa moja ukifika kwenye kituo kingine unapigwa faini ile ile zaidi ya mara nne,” amesema Gabriel Stanslaus konda wa magari ya Nyashishi-Kishiri mkoani humo.

Baadhi ya madereva wa daladala wamelalamikia kulipishwa Sh 60,000 kwa kupakia abiria katika maeneo ambayo bajaji zikipakia hazilipishwi huku wakitozwa ushuru wa Sh7,000 kila siku kwa kuingiza magari katika vituo vya daladala jambo linalowakosesha mapato.

Hii si mara ya kwanza kwa daladala kugoma nchini Tanzania huku sababu za migomo hiyo zikijirudia, itakumbukwa mwezi Agosti mwaka 2023 daladala mkoani Arusha zilizogoma kutoa huduma huku sababu ikitajwa kuingiliwa ruti na waendesha bajaji.


Soma zaidi:Tanapa yakamilisha ukarabati wa barabara hifadhi ya Serengeti


 Wananchi wahaha kusaka usafiri 

Wakati madereva wa daladala wakigoma, wananchi mkoani Mwanza wamelazimika kutoboa mifuko yao ili kukodi usafiri wa ziada utakaowafikisha katika shughuli zao huku baadhi yao wasiokuwa na kipato wakilazimika kutembea kwa miguu.

Tausi Mussa, mkazi wa Butimba jijini Mwanza amesema kwa siku ya leo amelazimika kutumia kiasi cha Sh2,000 tofauti na nauli ya kawaida ambayo ni Sh600 kufika Buhongwa.

Mbali na gharama hiyo pia amechelewa kufika eneo lake la kazi kutokana na uhaba wa vyombo vya usafiri barabarani na uwepo wa vurugu nyingi zilizosababisha msongamano.

Akizungumzia adha hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amekiri kuwepo kwa mgomo huo na kuagiza wamiliki wa daladala kuendelea kutoa huduma wakati Serikali ikishughulikia malalamiko yao.

“Sisi tumewaomba na tumewataka ndani ya masaa mawili daladala zote ambazo zimepaki zirudi barabarani na wamiliki kupitia uongozi wao wametuelewa…wakati wanarudi kamati ikae mezani iandae mapendekezo na kutuletea,” amesema Amina.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa waendesha daladala, Mjarifu Mnyasi amewarai wamiliki wa daladala kuendelea kutoa huduma za usafiri na kuiamini ahadi ya utatuzi wa malalamiko yao iliyotolewa na Serikali.

Related Post