Rais Magufuli ataja sababu za kuwang’oa Kichere TRA, Kakunda wizara ya viwanda

Daniel Samson 1032Hrs   Juni 10, 2019 Habari
  • Amesema walishindwa kuwajibika katika nafasi zao ikiwemo kusimamia ukusanyaji wa kodi na uuzaji wa korosho. 
  • Viongozi wapya walioteuliwa nao watahadharishwa kutolewa katika nafasi zao. 

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais John Magufuli kumng’oa Charles Kichere katika nafasi ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kumfuta kazi Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda, leo ameeleza sababu za uamuzi huo ikiwemo kushindwa kuwajibika katika nafasi zao.

Rais Magufuli alimteua Innocent Bashungwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara akiziba nafasi ya Kakunda huku nafasi ya Kichere ikichukuliwa na Edwin Mhede.

Dk Magufuli amesema leo Ikulu Jijini Dar es Salaam, wakati wa kuwaapisha viongozi hao wapya na kupokea malipo maalum ya Sh3 bilioni kutoka kampuni ya Bhart Airtel ya nchini India baada ya maridhiano ya umiliki wa kampuni ya Airtel Tanzania, kuwa viongozi hao hawakuwajibika ipasavyo. 

Rais Magufuli amesema kutowajibika kwa Kichere na Kakunda kumeleta changamoto ya mazingira ya kufanyia biashara na ukusanyaji wa mapato ya kodi ya ndani.  

Amesema tangu Kichere ameingia TRA ameshindwa kuinua kiwango cha ukusanyaji wa mapato ya ndani, jambo lililosababisha shughuli nyingi za utoaji huduma za kijamii zikwame kutokana na kukosekana kwa mapato. 

“Alipokuwa Kaimu pale alipandisha  (Dk Philip Mpango) kutoka Sh850 milioni mpaka Sh1.3 milioni nikaona huyu safi anajua mipango nikampa uwaziri. Nimempromote (nimempandisha) kutoka pale TRA sasa wengine mmekuwa mkienda mnasismamia hapo hapo kana kwamba hiyo ni formula (kanuni),” amesema.

Rais amebainisha kuwa amekuwa akipokea malalamiko mengi ikiwemo makadirio ya kodi kwa wafanyabiashara yasiyoendana na biashara zao na kuyaelekeza kwa Kichere ayafanyie kazi lakini kila akifuatilia yamekuwa hayafanyiwi kazi.

“Haiwekani Mkurugenzi wako, Kamishna wa ukadiriaji anafanya estimates (makadirio) za kijinga kwa wafanyabiashara kuwafustrate (kuwachanganya) na wewe upo tu unamwangalia tu wakati ungemfire (ungemfukuza) the power to hire and to fire (Nguvu ya kuteua na kufukuza unayo) unashindwa kuitumia.

“Unaona kabisa collection (ukusanyaji) kodi ya ndani inashuka, halafu no action (hakuna hatua inayochukuliwa),” amesema Rais Magufuli.

Rais John Magufuli aliyekuwa akizungumza leo Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha|Mtandao.

Aidha, Rais amesema TRA imekuwa kikwazo kwa baadhi ya wawekezaji wanaokuja nchini kutokana na kushikiria vifaa na malighafi zao kwa sababu ya kutokuelewana katika ukadiriaji wa kodi. 

Akitolea mfano wa mwekezaji ambaye hajamtaja jina, amesema “alikuwa na vifaa vyake anakuja kuchimba dhahabu, vifaa vile vimekaa zaidi ya mwaka mzima. alikuwa anadaiwa Sh1 milioni akaongezewa nyingi tu badala ya kuangalia huyu atakapokuja kuwekeza hiki atacreate employment (atatengeneza ajira) na serikali itapata revenue kutoka kwenye dhahabu.”

Kutokana  na changamoto hizo zilizojitokeza kwenye mamlaka hiyo inayosimamia kodi, Dk Magufuli alifikia uamuzi wa kumuondoa Kichere na kumuweka Mhede ili akalete mwamko mpya wa utendaji ndani ya TRA ikiwemo kuboresha utendaji, kuondoa urasimu kwenye vituo vya mipakani hasa mpaka wa Tunduma mkoani Songwe na Sirali (Mara) na kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato.

Hata hivyo, amemuonya Kichere kuwa ameteuliwa kuwa Katibu Tawala mkoa wa Njombe lakini akishindwa kutimiza majukumu yake kikamilifu atamwondoa. 


Zinazohusiana:   


Waziri mpya wa viwanda na biashara atahadharishwa

Akielezea changamoto za Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo huenda ndiyo zimemuondoa Kakunda, amesema wizara hiyo imeshindwa kusimamia uuzaji wa korosho zaidi ya tani 220,000 ambazo ziko kwenye maghala ambazo zilinunuliwa kutoka kwa wakulima baada ya wakulima kuingia katika mvutano na wanunuzi binafsi. 

Amesema Wizara ya Kilimo ilitimiza wajibu wake wa kukusanya korosho lakini wizara ya viwanda imeshindwa kutafuta soko la zao hilo na kupitwa na baadhi ya nchi za Afrika ambazo zimeuza katika soko la dunia.

“Korosho hizo zimekaa wakati Tanzania tulikuwa wazalishaji pekee, tumesubiri mpaka mwezi wa tatu mpaka mwezi wa nne unaingia. Nchi zingine za Benin, Nigeria, Ivory Coast nazo zikazalisha bado hatujauza. Wapo ! Sasa unakuwa na wizara ya nini? Kupeperusha bendera barabarani? haiwezekani!,” amesema Rais. 

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemwambia Waziri mpya wa Viwanda na Biashara, Bashungwa kuwa asiridhike na pongezi anazopewa kwa sababu anaweza kuondolewa wakati wowote katika nafasi hiyo kama alivyofanya kwa Kakunda. 

Amemtaka Bashungwa kwenda na kusimamia vizuri wizara yake na kushirikiana na watendaji kuondoa changamoto zilizopo hasa uanzishwaji wa viwanda.


Related Post