Dk Mpango atoa onyo kali kwa watumishi TRA

October 2, 2018 3:49 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ameagiza wafanyakazi wawili wa mamlaka hiyo waondolewe kwenye kazi wanazofanya sasa na kupangiwa kazi nyingine baada ya kuwepo kwa tuhuma za ulevi wa kupindukia na kuikosesha Serikali mapato.
  • Serikali haitomvumilia mtumishi yeyote atakayefanya kazi kinyume na maadili ili kujenga nidhamu kwa watumishi.
  • Awataka Mameneja wote wa TRA nchini watakaoshindwa wajitathmini kama wanatosha kwenye nafasi zao.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwachukulia hatua kali za kisheria na kinidhamu wafanyakazi wake wanaojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ikiwemo rushwa na kutumia njia zisizokubalika wakati wa kukusanya kodi za Serikali.

Dk Mpango ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza na wafanyakazi wa TRA Mkoa wa Tanga, ambapo ameagiza wafanyakazi wawili wa mamlaka hiyo, Robinson Munisi na Abraham Maleko waondolewe kwenye kazi wanazofanya sasa na kupangiwa kazi nyingine baada ya kuwepo kwa tuhuma za ulevi wa kupindukia na kujihusisha na mtandao wa wafanyabiashara unaotumika kuikosesha Serikali mapato yake

Amewataka watumishi wa mamlaka hiyo kuwa waadilifu kwa kujiepusha na vitendo vya rushwa na lugha za kuudhi kwa wateja wao ili kupunguza malalamiko kutoka kwa walipa kodi na kuonya kuwa serikali haitomvumilia mtumishi yeyote atakayefanya kazi kinyume na maadili ili kujenga nidhamu kwa watumishi hao na hatimaye kuongeza ufanisi katika ukusanyaji mapato ya Serikali.

“Mwambieni Kamishna Mkuu wa TRA (Charles Kichere) kuwa watumishi hawa siwataki, wapelekeni maeneo mengine mbali huko na muendelee kuwachunguza, na nataka kupata taarifa ya watumishi wanaokwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma ikiwemo kujihusisha na rushwa” amesisitiza Dk Mpango

 Aidha, amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James na Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere, kuhakikisha boti la doria katika Mwambao wa Bahari mkoani Tanga linapatikana haraka ili kuzuia biashara ya magendo inayoyofanywa kwa kutumia bandari bubu hivyo kuikosesha Serikali mapato yake.

“Ni lazima jambo hili lifanyike haraka kwa sababu ya umuhimu wake, si tu kwamba Serikali inapoteza mapato yake kutokana na vitendo hivyo vya kuvusha magendo kupitia bandari bubu lakini pia ni hatari kwa usalama wa Taifa kwa sababu maadui wanaweza kupitisha silaha” amesema Dk Mpango.

Akisoma taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu ya Mamalaka hiyo, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga Masawa Masawa alisema makusanyo ya mkoa huo yamekuwa yakiongezeka Mwaka hadi Mwaka kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Mwaka 2013 hadi 2017 ambapo katika Mwaka 2016/17 Mkoa ulikusanya Sh107.39 (Asilimia 82) bilioni kati ya Sh131.06 bilioni  ya malengo kwa mwaka huo.

Masawa amesema wanashirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutoa elimu kuhusu maadili mema ya kazi na kuwachukulia hatua kali watumishi wanaobainika kujihusisha na vitendo vinavyochafua taswira ya TRA. 

Enable Notifications OK No thanks