Serikali yatoa maagizo mazito kwa wanunuzi wa korosho

Daniel Samson 0050Hrs   Novemba 10, 2018 Biashara
  • Yawataka waandike barua wakionesha tani wanazohltaji na Iini watazichukua.
  • Yasema zaidi ya hapo haitoruhusu kampuni yoyote kununua korosho tena.
  • Wakulima wa korosho waaswa kuwa wavumilivu na watulivu wakati ikiendelea kushughulikia suala hilo. 

Dar es Salaam. Sakata la bei ya korosho lachukua sura mpya wanunuzi  35 waliojiandikisha kununua zao hilo msimu huu wa mwaka 2018/201 wapewa siku nne kupeleka barua katika Ofisi ya Waziri Mkuu wakionesha kiasi cha tani wanazohitaji na lini watazichukua. 

Agizo hilo limetolewa na Waziri Mkuu Kassirn Majaliwa leo  Novemba 9, 2018 wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu ununuzi wa zao la korosho ofisini kwake Mlimwa, Jijini Dodoma, ikiwa ni hatua ya kumaliza utata wa kukwama kwa ununuzi wa korosho katika minada inayofanyika katika mikoa ya Mtwara, Lindi, na Ruvuma.

Amesema baada ya kupita siku hizo Serikali italazimika kufuta usajili kwa wote waliojisajili kununua zao hilo kwa sababu walikubaliana kwenda kununua lakini hali inayoonekana sasa ni kama kumkomoa mkulima jambo ambalo halikubaliki. 

                           

Amebainisha kuwa katika  msimu wa ununuzi wa korosho wa mwaka huu wa 2018/2019, walishuhudia kusuasua kwa minada, ambapo Serikali ilikutana na wanunuzi wa korosho Oktoba 28 mwaka huu katika kikao kilichoongozwa na Rais John Magufuli ambapo walikubaliana kununua kwa bei inayoanzia Sh3,000 na kuendelea. 

Ameongeza kuwa baada ya muda uliowekwa kupita Serikali haitoruhusu kampuni yoyote kununua korosho tena.

"Mjadala ulikuwa wa wazi na wafanyabiashara wenyewe walipendekeza bei ambayo ilikuwa inaanzia Sh3,000, hata hivyo baada ya kikao hicho ununuzi katika minada imeendelea kusuasua na hata tani zilizokuwa zikinunuliwa zilikuwa kidogo sana. Sisi tunaiona hali hii kama mgomo baridi ambao si sawa kwani malengo yetu sisi na sekta binafsi ni kumfanya mkulima apate bei nzuri,” amesema.


Zinazohusiana: 


Kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, baada ya kugundua bei imekuwa tatizo Serikali ilifanya jitihada za kupeleka wataalarnu wake katika masoko makuu duniani na kupata bei halisi ya Sh3,000 ambayo inamnufaisha mkulima na mnunuzi. 

Hatua hiyo imekuja baada ya zao la korosho kuendelea kununuliwa kwa bei ya chini na idadi ya wanunuzi kuwa ya chini licha ya uzalishaji wa mwaka huu kuwa mdogo ukilinganisha na msimu wa mwaka jana. 

Uzalishaji katika msimu wa mwaka jana ulikuwa zaidi ya tani 300,000 na mwaka huu zinatarajiwa kuwa tani zaidi ya 200,000 hivyo wafanyabiashara wanao uwezo wa kununua korosho zilizopo. 

Hata hivyo, Serikali imewataka wananchi hususani wakulima wa korosho nchini kuendelea kuwa wavumilivu na watulivu wakati ikiendelea kushughulikia suala hilo. 

Related Post