Ongezeko la ndege ATCL kufungua fursa za biashara Tanzania

Lucy Samson 0926Hrs   Machi 26, 2024 Habari
  • Waziri Majaliwa asema kuongezeka kwa ndege za ATCL kutaifanya Tanzania kukuza biashara ndani na nje ya nchi.
  • Ndege ya Boeing  737 - 9 Max iliyopokelwa leo inaifanya Tanzania kuwa na jumla ya ndege 15 tangu kufufuliwa kwa ATCL mwaka 2016.


Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema ongezeko la ndege kwa Shirika la Ndege Tanzania ( ATCL) litachochea uzalishaji na kufungua fursa za biashara na uwekezaji nchini.

Majaliwa aliyeongoza mamia ya Watanzania kupokea ndege mpya aina ya Boeing 737 - 9 Max katika hafla iliyofanyika leo Machi 26, 2024 jijini Dar es Salaam amewaambia Watanzania kuwa kuongezeka kwa ndege za ATCL kutaifanya Tanzania kukuza biashara ndani na nje ya nchi.

“Ongezeko la ndege na huduma za usafiri litaendelea kusaidia na kuongeza huduma za usafiri…ukweli huo umeifanya ATCL ipate ndege za kutosha za abiria na mizigo ili Taifa letu lipate manufaa makubwa ya kukuza biashara kati yake na mataifa mengine,” amesema Majaliwa aliyekuwa akihutubia katika hafla hiyo.

Hii ni ndege ya kwanza kupokelewa katika mwaka 2024 ambayo inaifanya Tanzania kuwa na jumla ya ndege 15 tangu kufufuliwa kwa ATCL mwaka 2016.


Soma zaidi:Hasara ya ATCL yapungua, Rais Samia aanika madudu mapya


Katika ndege 15 zilizopo nchini hadi kufikia leo, ipo ndege ya mizigo ya  Boeing 767-300F ambayo imechangia kupaisha usafirishaji wa mzigo ndani na nje ya nchi na kufikia tani 675 Februari 2023 kulinganisha na tani 213 za mwaka 2022.

Kwa mujibu wa Majaliwa Tanzania inatarajia kupokea ndege nyingine ya abiria mwezi Aprili 2024, itakayofanya kuwa na jumla ya ndege 16 ambazo pengine zitaongeza usafirishaji wa bidhaa na abiria maradufu zaidi ya hali ya sasa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji ATCL Ladislaus Matindi, ongezeko la ndege limesaidia kukuza uchumi wa Taifa kutokana na kuongezeka kwa usafirishaji wa bidhaaa ndani na nje ya nchi pamoja na usafirishaji wa abiria unaochangia kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni.

“Kwa mwaka 2021/2022 ATCL ilichangia ukusanyaji wa Dola za Marekani milioni 43.3 (bilioni 110) iliyoongezeka hadi kufikia Dola za Marekani milioni 79.2 (bilioni 203) mwaka 2022/2023,” amesema Matindi.

Matindi ameongeza kuwa mbali na faida hizo za kiuchumi, ATCL imesaidia kuongeza upatikanaji wa ajira nchini kutoka wafanyakazi 115 hadi 780.


Safari za Dubai, London zanukia

Matindi amesema ATCL imepanga kuongeza mawanda za safari zake katika mataifa ya Falme za Kiarabu na Uingereza ili kuongeza ushindani na faida kwa Taifa.

Amebainisha kuwa kuanzia Machi 31, 2024 ATCL itaanza safari zake Katika mji wa Dubai na baadae jijini London nchini Uingereza kisha kufuatiwa na nchi nyingine kama Nigeria, Kongo na Sudani.

Katika hatua nyingine Majaliwa ameagiza wizara, uongozi na wafanyakazi wa wa ATCL kufanya kazi kwa weledi pamoja na kuwafichua wale wote wanaofanya ubadhilifu wa uwekezaji huo nchini ili kuiwezesha ndege hiyo pamoja na nyingine kufanya kazi kwa ufanisi na kuleta matokeo tarajiwa.

Related Post