Hasara ya ATCL yapungua, Rais Samia aanika madudu mapya

March 29, 2023 1:24 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Hasara imepungua kwa Sh1.1 bilioni mwaka 2021/22.
  • Abaini upigaji wa Sh114.6 bilioni ununuzi wa ndege ya mizigo.
  • Awataka Mawaziri kusimamia kwa makini.

Dar es Salaam. Licha ya hasara ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kupungua kwa Sh1 bilioni ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/22 imeibua madudu zaidi kuhusu manunuzi ya ndege ya mizigo inayotarajiwa kuingia nchini hivi karibuni.

Mwaka 2021/22 ATCL imepata hasara ya Sh35.2 bilioni kutoka Sh36.2 bilioni iliyorekodiwa mwaka 2020/21, licha juhudi mbalimbali za Serikali kulifufua shirika hilo ikiwemo kulitua mzigo wa madeni ili lijiendeshe kibiashara. 

CAG Charles Kichere ameeleza leo Machi 29, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha ripoti za ukaguzi kwa mwaka 2021/22 kuwa ATCL inaingia kwenye orodha ya makampuni 14 yaliyopata hasara.

“Nilifanya tathmini ya miaka miwili, mwaka huu na mwaka wa nyuma yake na nikagundua mashirika haya 14 ya kibiashara yamepata hasara (ikiwemo ATCL),” amesema CAG

Mashirika mengine yaliyotajwa kupata hasara ni ni pamoja na Shirika la Reli Tanzania (TRC), Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na Kampuni ya Mkulazi.

Mpaka sasa shirika hilo linalomilikiwa na Serikali ya Tanzania lina jumla ya ndege 12  zinazofanya  safari za anga ndani na nje ya nchi.

Taarifa hiyo ya CAG inakuja katika kipindi ambacho ATCL imekuwa ikiwezeshwa kwa kiwango kikubwa katika kufanya biashara ikiwemo kupatiwa ndege mpya ili kuongeza wigo wa maeneo ya kuruka kupanua soko lake.


Soma Zaidi


Rais Samia aanika madudu ndani ya ATCL

Rais Samia aliyekuwa akizungumza mara baada ya kupokea ripoti ya CAG ameweka wazi madudu yaliyotaka kufanyika  kwenye awamu ya mwisho ya malipo ya ndege ya mizigo inayotakiwa kuingia nchini hivi karibuni.

Amesema  malipo ya mwisho ya ndege hiyo yalitakiwa kuwa  Dola za Marekani milioni 37 (sawa na Sh86.5 bilioni)  lakini ameshangazwa na kuletewa ankara ya  malipo ya Dola za Marekani milioni 86 (sawa na Sh201.1 bilioni).

Kiongozi huyo wa nchi ameeleza kuwa ongezo la Dola za Marekani 49 milioni (sawa na Sh114.6 bilioni) limetengenezwa hapa nchini kwani hawakubaliana kiasi hicho na mkandarasi wa ndege hiyo.

“Ukilitazama kwa undani hili ongezeko limeanzia ndani…hatuwezi kwenda hivyo,” ameeleza Rais Samia.

Rais Samia amesema viongozi wanaoruhusu kutokea kwa makosa kama hayo hawatakiwi kwenye Serikali yake pia amewaagiza  mawaziri husika kusimamia malipo yanayofanywa na Serikali kwa umakini.

“Haya yapo mengi, yapo mengi sana mawaziri tusaidieni wasiwadanganye,” ameongeza Rais Samia.

Enable Notifications OK No thanks