Njia rahisi za kudhibiti joto kwenye gari lako

Rodgers George 0719Hrs   Januari 15, 2020 Maoni & Uchambuzi
  • Nunua vifaa vitakavyo kusaidia kupunguza joto hilo.
  • Unaweza kuokoa gharama hizo kwa kupaki gari lako kwenye kivuli.

Dar es Salaam. Ni dhahiri kuwa haufurahii pale unapofungua mlango wa gari lako na kukutana na  joto lililojikusanya kiasi cha kuligeuza gari lako kuwa  tanuru dogo.

Hali hiyo, siyo jambo la kushangaza kwa watu wenye magari binafsi hasa katika maeneo yenye viwango vya juu vya joto likiwemo jiji la Dar es Salaam ambalo mpaka jana lilifikia sentigrdi 33, kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)

Zipo njia mbalimbali za kuepusha gari lako lisipate joto sana hasa kama hujalitumia kwa saa kadhaa. Njia hizo hizi hapa;

  1. Nunua “Reflector” ya kioo cha mbele cha gari

Wataalamu wanasema kioo cha mbele cha gari kina uwezo wa kupitisha miale ya jua ambayo baada ya kuingia na kukutana na vifaa vya gari kama usukani na viti, miale hiyo haiwezi kurudi nje ya gari kupitia kioo na badala yake huendelea kubaki kwenye gari na kusababisha joto.

Hivyo namna ya kuepukana na hali hiyo ni pamoja na kununua “Reflector” ambacho ni kifaa maalumu cha kuweka kwenye kioo cha mbele ya gari ili  kuzuia miale ya jua kuingia kwenye gari.

  1. Fungua madirisha yako kidogo

Endapo unapaki gari yako juani, ni muhimu kuachia uwazi kidogo kwenye madirisha ili kuruhusu hewa kuingia ndani na kupunguza joto.

Unapofunga madirisha hadi mwisho, hewa ya ndani inakosa pa kwenda na hivyo inabaki ikijikusanya na kuongeza joto hasa pale gari yako linapokuwa juani.​

Kioo cha mbele cha gari kina uwezo wa kupitisha miale ya jua ambayo baada ya kuingia na kukutana na vifaa vya gari kama usukani na viti, miale hiyo haiwezi kurudi nje. Picha| Science news.

  1. Paki gari yako kwenye kivuli

Hauna haja ya kulianika gari lako juani kama vivuli vipo. Kama unavyotafuta kivuli wakati wajua kwa ajili yako, gari lako pia linahitaji kivuli. 

Mtaalamu wa masuala ya magari,  Alfred Kitula ameiambia www.nukta.co.tz  kuwa, kutokuweka gari kwenye kivuli siyo tu kunaongeza joto kwenye gari bali kunaweza kusababisha baadhi ya vifaa ikiwemo betri kupata hitilafu vikikaa juani muda mrefu. 

“Betri limetengenezwa na tindikali na maji, hivyo endapo joto likiwa kali sana, maji yanaweza kuanza kuevaporate (kugeuka mvuke) na hivyo inaacha “lead plates” zikiwa wazi. Na mara zingine gari yako inaweza kushindwa kuwaka kabisa,” amesema Kitula.

Alfed amesema “Lead plates” ni vifaa vinavyosaidia kutengeneza umeme kwenye betri unaotumika kuendesha vifaa vya gari yako.


Zinazohusiana


Angalizo

Kwa mujibu wa Kitulla, gari likikaa kwenye joto mara kwa mara hasa linatokana na jua linaongeza gharama za uendeshaji ikiwemo kulifanyia matengenezo ya mara kwa mara yasiyo ya lazima. 

“Mafuta yanatumika kwa wingi endapo gari likiwa limechemka sana. Na jua hili la Dar es Salaam, ukiacha gari yako kuanzia asubuhi hadi saa tisa fikiria linakua limechemka kiasi gani,” amehoji Kitula.

Mwanafunzi wa udaktari  anaye soma kwenye Chuo cha KCMC Moshi, Mlemeta Chilala amesema endapo mtu atatumia usafiri wake ilihari joto ni la juu sana anaweza kupata madhara hasa kama ana shida yoyote inayoweza kumsababishia homa kupanda.

“Joto siyo zuri kwa mtoto mdogo. Kwa watu wazima, inashauriwa kama gari yako ina joto sana, washa kiyoyozi au fungua madirisha ipoe kiasi kwani kama una shida inayoweza kukusababishia homa, unaweza kupata matatizo,” amesema Chilala.

Endelea kusoma tovuti hii kwa makala zinazoendelea kukuongezea ufahamu wako.

Related Post