Mbinu zitakazolinusuru gari lako na majanga ya mvua

Rodgers George 0309Hrs   Disemba 19, 2019 Teknolojia
  • Mambo ya kuzingatia ni pamoja na kutumia barabara uliyoizoea na kuhakikisha kila kifaa cha gari lako kinafanya kazi.
  • Epuka kufuata mkumbo na kutaka kuonyyesha umwamba wa gari yako kwani ikiharibika gharama ni zako peke yako.
  • Kagua gari lako mara kwa mara na usipende kuosha gari lako na maji ya mvua.

Dar es Salaam. Kutokana na mvua za hapa na pale zinazoendelea kunyesha nchini huenda umeshakwama na chombo chako cha moto mahali fulani au hata kupata ajali. Matatizo yeyote katika chombo cha moto yatokanayo na maji humlazimisha mtumiaji kuingia gharama ambazo hakuzitarajiwa.

Hata hivyo, kama ni dereva au mmiliki wa gari, bajaji na hata pikipiki ni vyema kufahamu kuwa vitu hivyo vyote kama vyombo vya moto vinaweza kuathirika endapo maji yatafika sehemu ambazo hayatakiwi kufika au kama vikikaa kwenye maji kwa muda mrefu.

Unafanyaje kukilinda chombo chako?  Wataalamu na mafundi wa vyombo vya moto wameiambia Nukta mambo mbalimbali ya kuzingatia katika chombo chako ili kuepukana na gharama ambazo zitakazokuharibia bajeti yako msimu huu wa sikukuu na kukusababishia Januari iliyojaa msongo wa mawazo. 


Fahamu barabara unayopita

Fundi wa magari kutoka katika moja ya gereji za Mwananyamala ajulikanaye kama Fundi Yusuph anasema siyo vyema kujaribu njia mpya wakati wa kipindi cha mvua kwa kuwai unaweza kukwama kwa sababu ya kutokuifahamu barabara hiyo. 

“Barabara unayoipita kila siku ipo kichwani. Ramani yake ipo kwenye kumbukumbu kwa hiyo hata ukikuta maji utajua tu kwamba hapa gari yangu inapita au haipiti,” amesema Yusuph.

Maelezo yake yanaelezea kuwa, endapo mtu akitumia njia mpya, siyo rahisi kujikwamua hata akikwama kwani anakuwa mgeni wa mazingira na hajui kinachomkwamisha.


Fahamu “air cleaner” ya gari yako ilipo

Air cleaner” ni kifaa ambacho kinachuja na kuzuia uchafu kama vumbi, mchanga na vijikokoto kuingia kwenye injini ya gari yako. Kifaa hiki kama kikiingiwa maji husababisha injini kuvuta maji na kuathiri gari lako. 

Yusuph amesema kwa gari kama Toyota IST na zingine ambazo zipo chini ni muhimu kukwepa kabisa sehemu zenye madimbwi makubwa ambayo yanaweza kusababisha kifaa hicho kuingiwa na maji.

Huu sio msimu wa “kujimwambafai” bali ni msimu wa kuwa mpole ukifahamu kuwa gari yako ni ya tofauti na zingine. Picha| Euricaafrica.

“Sehemu ambayo ina maji ukipitisha gari ikanywa maji injini ina “knock” (injini kupata hitlafu),” amesema Yusuph.

Yusuph amesema ni bora kufahamu ukomo wa uwezo wa gari yako kwani kama gari yako inauwezo mdogo, usiilazimishe kufanya maajabu.


Epuka kufuata mkumbo wa magari mengine

Huu sio msimu wa “kujimwambafai” bali ni msimu wa kuwa mpole ukifahamu kuwa gari yako ni ya tofauti na zingine.

Kutokana na barabara nyingi kuharibika kipindi cha mvua, unaweza ukaona gari inapita mahala ambapo yako haipiti lakini kwaajili ya kuonyesha umwamba, ukataka kupitisha na wewe gari yako na hivyo kuishia kukwama.​

Yusuph amesema kamwe nguvu ya Prado haiwezi kulingana na IST au Passo, hivyo sio busara kwa mtu mwenye gari ndogo kutaka kufanya kile anachofanya mwenye gari kubwa.


Funika gari yako kama umeipaki nyumbani

Huenda ulifikiri ni ahueni mvua imenyesha ili gari yako ipate muosho wa bure lakini unafahamu kama maji ya mvua ni hatari kwa gari yako?

Mwandishi wa habari za Magari kutoka tovuti ya “carfromjapan” ambaye pia ni mmiliki wa duka la matengenezo ya magari Tsukasa Azuma amesema maji ya mvua yana asidi ambayo siyo rafiki kwa rangi ya gari yako.​

Unafahamu kama maji ya mvua ni hatari kwa gari yako? Picha| Trade me.

Hivyo ni busara ukaacha kufurahia muosho wa bure wa gari yako na kuanza kuifunika wakati wa mvua ili kuepukana na gharama za kuipaka rangi upya mara kwa mara.


Osha gari yako mara kwa mara

Wamiliki wengi wa magari wanayachukulia poa maji yaliyotuama. Lakini Azuma amesema, maji yaliyotuama yana madhara kwa magari kuliko inavyodhaniwa.

Fikilia hili. Kama maji yametuama na zimepita gari zaidi ya tano kabla yako hivyo kufanya vumbi au tope kuchanganyika na maji hayo unafikiri maji hayo siyo adui wa gari yako?

Kupitisha gari yako kwenye maji yaliyotuama kwenye tope hulifanya gari lako kukusanya uchafu mwingi kuliko hata kipindi cha kiangazi.

Inashauriwa kuliosha gari lako walau kila unaporudi nyumbani ili kulikinga na hatari ya kuharibika.

Hata kwenye kuosha, tumia sabuni nzuri ya gari kuepuka kuikwaruza gari yako kwa kuwa kipindi cha mvua, mchanga unakua ni mwingi na kulisugua bila vilainishi kunaweza kuchubua chombo chake cha moto.


Zinazohusiana


Zipo dondoo nyingi za namna ya kuhifadhi gari yako kwenye kipindi cha mvua kubwa zikiwemo kuhakikisha maji hayaingii ndani ya gari yako na kuhakikisha matairi ya gari yako yako vizuri ili kuepukana na ajali.

Kampuni ya magari ya Toyota ya Japan iimeainisha kuwa ni muhimu kiangalia gari lako na kulikagua kila mara kwani huenda lina hitlafu ambayo inaweza kukusababishia ajali.

Hakikisha unakuwa makini na ubora wa breki zako, ufaniisi wa taa zako na pia vipangusa vioo vyako vinatakiwa kufanya kazi bila kusahau kiyoyozi cha gari yako.

Endelea kusoma habari za Nukta kupata dondoo muhimu zinazokuhusu.

Related Post