Wanafunzi wa NIT waja na gari la umeme kama Tesla

TULINAGWE MALOPA 0752Hrs   Septemba 07, 2018 Teknolojia
  •  Wanafunzi hao wana mpango wa kuliboresha gari hilo litumie umemejua ili kuwa sehemu ya uhifadhi wa mazingira kwa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.
  •  Ni changamoto kwa vijana kubuni teknolojia rahisi kurahisisha maisha.

Kama unadhani vijana wa Tanzania wamelala basi utasubiri sana. Kila siku wanaibuka vijana wenye uthubutu wa kubuni teknolojia rahisi ya kurahisisha maisha na kuzidi kuiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia. 

Safari hii ni wanafunzi 14 kutoka Chuo Cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT) wameamua kutengeneza gari linalotumia umeme wa betri zilizohuishwa ikiwa ni sehemu za kuendeleza ubunifu wa kutengeneza magari yanayoweza kuwa sehemu ya utunzaji wa mazingira. 

Iwapo watafanikiwa zaidi hapo baadaye kwa kuzalisha kibiashara,vijana hao watakuwa na mradi unafanana na uwekezaji anaofanya bilionea wa Marekani Elon Musk katika kampuni yake ya Tesla ambayo inafahamika zaidi katika utengenezaji wa magari yanayotumia umeme wa betri za kawaida za kuchaji vituoni na umemejua.

Gari hilo ni sehemu ya masomo ya vitendo kwa wanafunzi hao ambao wanatarajia kuhitimu katika fani ya uhandisi umeme. Mradi wa kutengeneza gari hilo la umeme umefanyika kwa muda wa miezi mitatu chini ya usimamizi wa wakufunzi mahiri wa NIT.

Mfumo wa gari hilo unatumia betri tano zenye jumla ya volti 60 zinazosambaza umeme kwenye injini tofauti na  magari ya kawaida yanayotumia mafuta ili yaweze kufanya kazi. Gari hilo linaendeshwa kwa mfumo wa vitendo (Manual) badala ya 'automatic' kama magari mengine.

Gari hilo lina wezo wa kusafiri kilometa 90 kabla ya betri kuchajiwa tena. Pia betri hizo zinatumia saa mbili ili ziweze kujaa na gari hilo liweze kutembea tena. 

Ili kuliongezea kasi na uwezo wa kutembea muda mrefu barabarani, wanafunzi hao wana mpango wa kuliwezesha litumie umemejua (Solar Energy).

Gari hilo limepewa jina la EV 01-2018 (Electric Vehicle First Generation 2018) kama gari linalotumia nguvu ya umeme na kwa mara ya kwanza litengenezwa katika mwaka wa masomo wa 2018 katika chuo hicho.

Mtatiro Boniphace ni mmoja wa wanafunzi waliobuni gari hilo anaeleza kuwa lengo kubwa la kuonesha uwezo wa teknolojia katika kubuni vitu mbalimbali vinavyoweza kusaidia watu katika shughuli mbalimbali za usafiri ikizingatiwa kuwa gari hilo lina uwezo kubeba watu wanne na kusaidia kutunza mazingira kwa kupunguza utoaji wa hewa ukaa.

“Gari hili limebuniwa kwa kukamilisha miradi yetu chuoni, lakini pia ni la msaada kwa wahandisi wadogo kubuni teknolojia zinazoweza kuleta tija katika nchi yetu na kwa watu kwa ujumla”. Amesema Boniphace.

Gari la namana hiyo siyo la kwanza kubuniwa duniani ambapo hivi karibuni vijana wengine nchini Kenya walibuni gari linalotumia umemejua. Wakati hayo yakifanyika Afrika, katika nchi zilizoendelea wameenda mbalimbali zaidi na kutengeneza magari ambayo yanatembea bila dereva.

Ni changamoto kwa vijana wa Afrika kuongeza kasi ya ubunifu ili kuhakikisha wanaenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia yanalenga kuboresha maisha ya watu.

     Gari la umeme la Tesla likiwa barabarani. Kampuni hiyo inafahamika kwa uvumbuzi wa magari yanayojiendesha na kutumia umeme wa betri za kuchaji na umemejua kama ambalo limesanifiwa na vijana wa NIT. Picha|Tesla.


Related Post