Mbinu tano za kudhibiti matumizi makubwa ya intaneti kwenye ‘smartphones’

Nuzulack Dausen 0315Hrs   Januari 23, 2019 Teknolojia
  • Udhibiti wa matumizi holela ya intaneti yanaongoza gharama za maisha.
  • Kuzima data wakati hutumii intaneti ni moja ya njia rahisi za kudhibiti matumizi makubwa ya vifurushi vya mtandao.

Intaneti kwa sasa imekuwa ni sehemu ya maisha yetu. Matumizi ya teknolojia hiyo inayotuunganisha na ulimwengu kupitia mtandao yamekuwa muhimu kama ilivyo umeme, maji na chakula.

Kuna baadhi hawajisikii furaha wakikosa intaneti. Biashara zinakwama kwa kukosa intaneti. Baadhi ya ndoa zinavunjika kwa kukosa intaneti kutokana na umbali wa wanandoa na wanafunzi wanaweza wasifanye vema kwenye mitihani yao kwa kukosa huduma hiyo.

Kutokana na umuhimu huo wa intaneti, wengi sasa wanalazimika kutenga bajeti mahususi ya kuhakikisha hawakosi angalau kifurushi kidogo kitakachowafanya wawe hewani ili kujipatia habari mbalimbali na kufanya shughuli za kujiingizia kipato.

Hata hivyo, wakati matumizi ya intaneti miongoni mwetu yakiongezeka, tumejikuta pia gharama za maisha zikipaa na kufanya baadhi ya mambo ya msingi ya kimaisha yasifanyike ipasavyo.

Baadhi wamejikuta wakipunguza bajeti katika maeneo muhimu kama chakula, elimu au miradi mingine ya maendeleo ilimradi apate intaneti.

Kwa bahati mbaya siyo watumiaji wote hutumia ipasavyo huduma hiyo. Kuna baadhi hujikuta wakiacha intaneti ikipotea bila sababu za msingi kutokana na uelewa finyu wa teknolojia ama vifaa wanavyotumia.

Hata wakati matumizi ya intaneti yakipaa, uliwahi kujiuliza ni njia zipi zinaweza kusaidia kupunguza gharama za intaneti?

Kuna njia mbalimbali ambazo zinaweza kupunguza kiwango cha matumizi yasiyo ya lazima ya intaneti na kuokoa kiwango cha fedha. Yafuatayo yanaweza kusaidia jambo hilo hasa kipindi ambacho vyuma vimekaza:-


Zima intaneti wakati huna matumizi nayo

Kutokana na baadhi yetu kuanza kuwa mateja wa intaneti, tumejikuta tukiacha simu au tabiti (tablet) zikiwa mtandaonii muda wote hata nyakati za usiku wakati tumelala.

Tabia hiii, ambayo huenda imeanza kushamiri miongoni mwetu, inachangia kwa kiwango kikubwa kumaliza kifurushi cha intaneti na kuongeza matumizi.

Tufahamu kuwa wakati simu ipo mtandaoni kuna programu zinazotumia intaneti ambazo huendelea kufanya kazi nyuma ya pazia (background apps) ndiyo maana huona ujumbe kuwa app inataka kujiboresha au taarifa (notification) iwapo kuna ujumbe wa WhatsApp ama barua pepe unapoingia.

Programu hizo hutafuna kifurushi cha intaneti na kukufanya uvunje kibubu kila siku bila kujua. Njia rahisi ya kuzuia matumizi hayo yasiyo ya lazima ni kuzima data wakati unalala au huna matumizi nayo hata kama ni mchana.


Matumizi ya intaneti ni muhimu kwa binadamu kwa sasa kijamii, kibiashara na kiuchumi. Ili kufaidika zaidi na huduma hizo ni bora pia kudhibiti matumizi ya intaneti yanayotafuna fedha bila ulazima. Picha|Mtandao.

Dhibiti programu zinazofanya kazi nyuma ya pazia (Background apps)

Ili kuhakikisha unakua karibu na programu mbalimbali za simu yako, watengenezaji wa app huweka namna ambavyo inaweza kuendelea kufanya kazi nyuma ya pazi hata bila kuifungua ilimradi tu iwe kwenye mtandao.

Kwa muda wa miezi sita sasa nimekuwa nikufuatilia kwa karibu apps zangu zilizopo kwenye simu yangu. Nimegundua kuwa pamoja na kuwa huwa sizifungui apps hizo huwa zinakula kiwango kikubwa tu cha data kwa kuendelea kufanya kazi nyuma ya pazia ikiwemo kujiboresha (updates) bila kuziamuru kufanya hivyo.

Sehemu kubwa ya apps zilizopo kwenye mfumo wa Android zinaweza kufanya kazi nyuma ya pazi kwa kutafuta maboresho ya programu mtandaoni licha ya kuwa baadhi ya simu sasa zimekuja na huduma maalum ya kudhibiti apps hizi ili zisiendelee kukutafuna.


Soma zaidi: Jinsi ya kufanya mitandao ya kijamii isikuharibie mahusiano yako


Ni muhimu, kutafuta function ya ‘data saver’ (kiokoa data) hasa kwenye simu za Android na kukiwasha ili kudhibiti matumizi makubwa ya intaneti.

Kwa simu nyingi za kisasa, huduma hii inapatikana katika ‘Settings’ halafu nenda kwenye ‘Network na internet’ na chagua ‘data usage’. Ukifika hapo utaiona moja chaguo la data saver na kuamua app za kudhibiti kupitia ‘restrictions’. Huduma hii ipo pia kwenye iPhone kupitia settings halafu ‘general’ na kuchagua ‘restrictions’.

Jambo la muhimu kufahamu ni kwamba aina ya simu na programu endeshi zinatofautiana kila toleo. Jitahidi kuhakikisha umeelewa vyema namna unavyoweza kupata huduma hiyo.



Weka kikomo cha matumizi ya intaneti (data)

Njia mojawapo ya kudhibiti matumizi makubwa ya intaneti ni kuweka kikomo cha matumizi yako ya mwezi kwenye simu yako. Ukomo husaidia mtumiaji kujulishwa iwapo anakaribia kuvuka kikomo ili kuhakikisha anatumia huduma hiyo kwa mujibu wa bajeti.

Unaweza ukapandisha na kushusha ukomo kulingana na mipango ya matumizi yako. Uwekezaji wa kikomo unakusaidia kupanga bajeti ya intaneti kwa wiki au mwezi na kuepuka usumbufu wa kutumia nje ya ulichonacho.

Kwa mfano, licha ya shughuli zangu kutumia kiasi kikubwa cha intaneti simu yangu nimeiseti kutoa taarifa kila napofikia GB 2.15. Ukomo huu hunisaidia kupata onyo la matumizi makubwa ya intaneti na kufanya nijitathmini ni jambo gani kubwa limefanyika kiasi cha kunywa kifurushi kiasi hicho.


Dhibiti matumizi ya ‘mobile hotspot’

Moja ya sababu nyingine zinazosababisha matumizi makubwa ya intaneti ni kuacha huduma ya simu kugawia vifaa vingine mtandao kama Wi-Fi.

Baadhi yetu huacha huduma hiyo bila nywila yeyote ambayo inaweza kudhibiti wasiohusika kutumia intaneti yao bila kujijua. Huduma hii ni moja ya zile zinazotafuna zaidi kifurushi kwa kiwango kikubwa sanjari na WhatsApp, YouTube na nyinginezo.

Hakikisha unawasha tu pale unapotaka kuunganisha na kifaa kama laptop au simu nyingine. Weka nywila na ukomo wa watumiaji kama ni mmoja, wawili au watatu.

Chunguza mara kwa mara kuhakikisha wanaotumia intaneti ni wale wanaowafahamu pekee. Hii itakuhakikishia usalama wa mawasiliano yako kwa kuwa wengi wanaweza kuiba taarifa zako muhimu iwapo hutadhibiti.

Dhibiti apps zisipakue picha au video moja kwa moja

Baadhi ya programu kama WhatsApp au Telegram zina namna ambayo unaweza kudhibiti zipakue picha, video na nyaraka moja kwa moja pale utakapotumiwa. Huduma hii inasaidia kudhibiti matumizi ya intaneti kwa kiwango kikubwa.

Katika kipindi ambacho watu wengi wapo kwenye makundi ya mitandao ya kijamii kama WhatsApp ni vyema usiruhusu app hizo kufungua picha au video moja kwa moja kutunza data kwa kuwa kuna tabia ya vitu kujirudia.

Video moja ya MB5 unaweza kutumiwa katika makundi hata zaidi ya matano au 10. Kufungua mafaili hayo kwa wakati mmoja kunaweza kukufanya upoteze wastani wa MB50 ambazo ni nyingi kwa mtu wa kipato cha chini na zinagharimu fedha hata kama ni kifurushi.

Hizi ni sehemu tu ya njia za kudhibiti matumizi makubwa ya intaneti ili kuhakikisha tunatumia vema taknolojia hii bila kuathiri bajeti nyingine muhimu.

Naamini zipo nyingi. Tafadhali tujulishe unayotumia zaidi kwa faida ya wengine. 

Nuzulack Dausen ni Mwanahabari wa biashara, uchumi, takwimu na teknolojia wa nukta.co.tz. Kwa maoni ushauri wasiliana naye kupitia  ndausen@nukta.co.tz or +255764176793.

Related Post