Maumivu: bei ya petroli, dizeli ikipanda Tanzania

Lucy Samson 0533Hrs   Machi 06, 2024 Biashara
  • Petroli imeongezeka kwa Sh112  na dizeli kwa Sh97.
  • Hii ni mara ya kwanza ndani ya miezi saba kwa bei ya mafuta kupanda.

Dar es Salaam. Huenda watumiaji wa vyombo vya moto nchini Tanzania wakaanza mwei Machi kwa maumivu mara baada ya bei ya mafuta ya petroli na dizeli kuongezeka kidogo.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Tanzania (Ewura) leo 6, Machi 2024 inaeleza kuwa bei ya rejareja ya petroli iliyoingizwa kupitia bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kwa Sh112 huku dizeli ikiongezeka kwa Sh97.

Kutokana na bei hizo mpya lita moja ya petroli jijini Dar es Salaam inauzwa kwa Sh3,163 kwa lita ikiongezeka  kutoka Sh 3,051 iliyokuwa inatumika mwezi Februari na dizeli inauzwa kwa Sh3,126 ikiongezeka kutoka Sh3,029 iliyorekodiwa mwezi uliopita.

Bei ya mafuta ya taa inayotumika katika mwezi huu ni Sh2,840 ambayo ni sawa na ile iliyotumika mwezi Februari.


Soma zaidi:Riba, viwango vya kubadili fedha, sababu madeni ya nchi za Afrika kukua kwa kasi


Kwa upande wa mafuta yanayoingizwa kupitia Bandari ya Tanga  lita moja ya petroli inanunuliwa kwa Sh3,209, dizeli kwa Sh3,173  na mafuta ya taa kwa Sh 2,886.

Wanaotumia bandari ya Mtwara wananunua petroli Sh3,155 kwa lita, dizeli Sh3,070 na mafuta ya taa Sh2,913 kwa lita.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari Ewura imesema kupanda huko kwa mafuta kumetokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.

“Mabadiliko ya bei za mafuta kwa mwezi Machi 2024 yamechangiwa na ongezeko la bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia (FOB) kwa wastani wa asilimia 4.5 kwa mafuta ya petroli na asilimia 1.99 kwa mafuta ya dizeli na kupanda kwa gharama za uagizaji wa mafuta (premiums) kwa Bandari ya Dar es Salaam,” imesema taarifa ya Ewura.

Bei mpya ya petroli, dizeli na mafuta ya taa iliyotangazwa leo na Ewura inakuwa ni bei ya juu zaidi kuwahi kurediwa ndani ya kipindi cha miezi saba tangu Julai 2023.

Ndani ya kipindi hicho cha miezi saba bei ya mafuta ilikuwa ikishuka kidogo kidogo hali iliyoacha ahueni kwa watumiaji wa vyombo vya moto nchini.

Huenda kupanda kwa bei mpya za mafuta kukasababisha kupanda kwa nauli za vyombo vya moto kama dalalala ambazo hutumiwa na watu wengi hususan jijini Dar es Salaam.Picha|Lucy Samson.

Maumivu hadi mikoani

Wakati wakazi wa Dar es Salaam wakiendelea kusikilizia maumivu ya  kupanda kwa bei ya mafuta wakazi wa Kyerwa mkoani Kagera wao wananunua petroli kwa Sh3,401 ikiwa ni bei ya juu zaidi ya maeneo mengine nchini.

Bei hiyo inayotumika Kyerwa kwa mwezi machi ni ongezeko la Sh113 kutoka Sh3,288 iliyokuwa ikitumika mwezi Februari.

Wakazi wa Ukerewe jijini Mwanza wananunua dizeli kwa Sh3,336 ikiwa ni bei ya juu zaidi ya mikoa mingine nchini.

Kwa bei hiyo mpya mtumiaji aliyekuwa anapata lita 3.27  ya petroli kwa Sh10,000 sasa atapata lita 3.1 pekee kwa kiwango kile kilecha fedha.

Na aliyekuwa anatumia Sh10,000 kupata lita 3.3 za dizeli mwezi Februari mwezi huu atapata lita 2.8 kwa bei zilizotangazwa leo.

Related Post