Riba, viwango vya kubadili fedha, sababu madeni ya nchi za Afrika kukua kwa kasi

Esau Ng'umbi 0857Hrs   Machi 05, 2024 Habari
  • Awali ukuaji wa madeni ulikuwa unaendana na ukopaji tofauti na sasa.
  • Nchi za Afrika zakutana kutafuta mwarobaini.


Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa kuongezeka kwa viwango vya riba pamoja na viwango vya kubadilisha fedha duniani, ndio chanzo cha kushuka kwa thamani ya fedha za nchi za Afrika pamoja na kukua kwa kasi kwa madeni ya nchi hizo.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya, aliyekuwa akizungumza wakati wa mkutano wa 56 wa Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi kutoka nchi za Umoja wa Afrika amesema awali ukuaji wa deni ulikuwa unaendana na ukopaji lakini kwa sasa imebainika kuwa kuna sababu zingine zinazochochea kuongezeka kwa deni hilo.

“Sababu hizo ni pamoja na mabadiliko makubwa ya viwango vya kubadilisha fedha na riba hivyo kuzifanya nchi za Afrika kutafuta njia mbadala ya kutatua changamoto hiyo,” amesema Mwandumbya aliyemuwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba jijini Victoria Falls, nchini Zimbabwe.

Mwandumbya ameongeza kuwa katika kulihudumia deni “dept service” lililoongezeka, kumekuwa na changamoto kubwa kwa sababu nchi nyingi bado hazina uwezo wa kukusanya mapato ya kutosha kugharamia huduma mbalimbali.


Soma zaidi: Serikali yajipanga kuongeza viwango vya ukusanyaji kodi Tanzania


Aidha, Mwandumbya amebainisha kuwa, katika kukabiliana na changamoto za ukuaji wa madeni hususani kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya tabianchi ni muhimu kwa nchi za Afrika kuwa na mkakati wa kuhakikisha zinapata rasilimali fedha ili mipango inayotekelezwa iweze kukidhi mategemeo ya wananchi.

“Changamoto kubwa ambayo tunaiona hapa kwa nchi zetu za Afrika ni ile haja ya kuendelea kukusanya mapato ya kutosha ili kujihakikishia kwamba tunaweza kupata rasilimali za kuweza kuhudumia deni lakini pia tunaweza kulipa mishahara pia kuhudumia gharama mbalimbali za kibajeti,” ameongeza Mwandumbya.

Kwa mujibu wa Mwandumbya, miongoni mwa ajenda kubwa zinazojadiliwa katika mkutano huo ni kupata suluhu ya namna gani nchi zitaboresha viwango vya ukusanyaji wa mapato ili kutoka kwenye viwango vya chini ya asilimia 11 na 12 ya ukuaji wa mapato ya ndani (GDP) kwenda viwango ambavyo vinavyokubalika kuanzia asilimia 16.

Itakumbukwa Mwezi Februari, Makamu wa Rais wa Tanzania Dk. Philip Mpango alibanisha kuwa Serikali ipo mbioni kutafuta suluhu itakayoongeza viwango vya ukusanyaji wa kodi hadi kufikia asilimia 15 ya pato la Taifa ili kuwezesha shughuli za maendeleo na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Mkutano huo wa 56 unaratibiwa na Uneca, jukwaa lililoanzishwa na Umoja wa Mataifa ili kuzisaidia nchi za Afrika kufanya mijadala na tafiti mbalimbali ili kuzalisha na kufanya ubunifu utakaokuza uchumi hivyo kutengeneza fursa ya kujadiliana na kuhakikisha ushauri unaotolewa unaendana na mazingira halisi.

Related Post